Na Hafsa Golo
MKUU wa wilaya ya magharibi Unguja,Ayoub Mohammed Mahamoud, amesema anakusudia kulipatia ufumbuzi tatizo sugu la ndani ya wilaya ya magharibi ambalo
limeonekanwa kudumu kwa muda mrefu.
Aliyasema hayo wakati
akizungumza na Zanzibar Leo mara baada ya
hafla fupi ya kumpongeza kuteuliwa kushika nafasi hiyo, katika hafla
iliyofanyika ofisi ya Mkuu wa mkoa Vuga.
Alisema migogoro ya ardhi
katika wilaya hilo ni makubwa ambapo
kuna zaidi ya kesi 27 zilizopo mezani zinazohitajia kusuluhishwa na kesi
zaidi ya 580 tayari zipo mahakamani.
Alisema migogoro hiyo imekuwa
endelevu kutokana na wimbi kubwa la ukuaji wa idadi ya watu ambapo, alisema
mwaka 2002 watu walikuwa wastani wa 180,000 ambapo hivi sasa imefikia wastani
wa watu 370,645, kati ya watu 568,688 waliomo mkoa wa mjini magharibi.
Alisema kutokana na ukubwa wa
migogoro hiyo italazimika kulitazama suala hilo kwa ukaribu zaidi kwa
kulitathimini kwa kina ili kuondosha mivutano hiyo ambayo imekuwa kukileta
matabaka miongoni mwa wananchi.
“Nitakutana na taasisi za
ardhi,kukaa pamoja na kamati za kijamii, masheha, wazee,vijana,asasi za kiraia
na wanasiasa kujaribu kulitafutia
ufumbuzi suala hili,” alisema.
Akizungumzia amani na utulivu,
alisema vitendo vingi vinavyosababisha uvunjifu wa amani vimekuwa vikitokea
katika wilaya hiyo hivyo ni vyema kushirikiana pamoja na vyombo vya ulinzi na
usalama kuhakikisha vitendo hivyo vinatoweka.
Alisema jambo jengine ambalo
amelikusudia kuliimarisha ni kuileta jamii pamoja na kushirikiana katika
masuala ya kijamii ili ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi uweze kuwanufaisha wote.
Kwa upande wake aliekuwa Mkuu
wa wilaya ya magharibi, Mussa Hassan Takrima, alimshauri kuwa makini juu ya
masuala ya ardhi kwani yamekuwa kero kubwa kwa wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa mjini magharibi,
Abbdala Mwinyi, alisema alimshauri mkuu huyo wa wilaya kutumia zaidi hekma za
busara wakati anapotekeleza majukumu yake.
No comments:
Post a Comment