Na Husna Mohammed
Uelewa mdogo wa wanawake katika
suala zima la mgawanyo wa mali hasa kwa wanadoa kwa kiasi kikubwa kunsababisha
kukosa haki zao mara baada ya ndoa kuvunjika.
Akizungumza na vyombo vya
habari ofisi ya Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanania (TAMWA)
Zanzibar, Ofisa miradi wa chama hicho, Asha Abdi Makame, alisema wanawake wengi
wanakosa haki zao hata kama wamechuma wote mali na mwanamme wakati wa ndoa.
Alisema sheria ya Kadhi namba 3
ya mwaka 1985 imekosa mashiko ya mgawanyo wa mali kwa wanandoa na hivyo
kusababisha malalamiko kwa wanandoa hasa wanapotengana.
“Tumepata habari kuwa hata hiyo sheria ya
kadhi iliyofanyiwa marekebisho haikugusia kwa undani kipengele hicho hivyo
tunataka taasisi husika kuliona hilo na kulifanyia kazi kabla ya kufikishwa
barazani kujadiliwa,” alisema.
Alisema wanaume wanaitumia
fursa hiyo kuoa kila siku na kuwatumia
baadhi ya wake zao kama kitega uchumi kwa kuwa hakuna sheria ya kuwadhibiti.
“Talaka zimekuwa kama njugu kwa
kuwa hakuna kidhibiti cha sheria kwa wanandoa wanaoachana jambo ambalo hata
wanaume hawatumii ihsani ya kumrudi mali mke huku akimwacha na watoto bila ya matunzo yoyote,” alisema.
Alisema mbali na mahakama ya
kadhi kutoa amri ya utunzaji wa watoto kwa mtalaka mwanamke, lakini mahitaji ni
madogo ikilinganishwa na huduma husika ya watoto anaoachiwa mwanamke.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti
mdogo juu ya uwelewa wa wananchi kuhusiana na mgawanyo wa mali, Mwajuma Juma,
alisema hali uelewa kwa jamii bado ni mdogo na taaluma inahitajika zaidi.
“Tumezungumza na makadhi na viongozi wa dini
ya kiislamu wanasema haki ya mali ni hiba tu kwa mwanamke au mtalaka wakati wa
kutengana na si sheria na kinyume na hivyo ni kwenda kinyume na sheria ya kadhi
inayoendana na misingi ya dini ya kiislamu,” alisema.
Alisema mwanawake mmoja kati ya
10 ndie anaejua suala la kuandikiana hasa kwa mali wanaochuma wote.
Nae Sada Said Issa, ambae ni Ofisa
Mipango wa ZAFELA, alisema chama hicho kiliipitia sheria hiyo na kutoa
mapendekezo yake ambapo kwa sasa yako katika mchakato wa Makatibu Wakuu kwa
ajili ya kuwasilishwa Baraza la Wawakilishi.
Sambamba na hilo alisema
kutokuweko kwa sheria ya ndoa Zanzibar,kwa kiasi kikubwa kunasababisha matatizo
mengi ya ndoa ikiwemo mgawanyo wa mali.
Alizitaja nchi za Malaysia,
Singapore, Indonesia na nchi nyengine za kiislamu zinatumia sheria kuweka
mazingira mazuri kwa wanandoa, jambo ambalo hata Zanzibar inaweza kuiga.
Mkutano huo uliandaliwa na
TAMWA ikiwa ni katika ukamilishaji wa mradi wa GEWE unaofadhiliwa na Shirika la
DANIDA ambao unaomaliza muda wake mwezi
huu.
No comments:
Post a Comment