Na Khamis Haji, OMKR
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Fatma Abdulhabib Ferej, amesema serikali
inathamini mchango unaotolewa na jumuiya za kiraia pamoja na vyombo vya habari
katika kuielimisha jamii athari za mabadiliko ya tabianchi na kukabiliana nazo.
Aliyasema hayo jana alipofanya
mazungumzo na ujumbe kutoka Jumuiya ya Zanzibar Climate Change Alliance
ulioambatana na waandishi wa habari kutoka kituo cha TV cha East Africa
Televisheni (EATV) ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar.
Alisema kutokana na uhalisia
wake, Zanzibar ni eneo la visiwa hali inayosababisha kukumbwa na athari za
mabadiliko ya tabia nchi, ikiwemo maji ya bahari kupanda juu na kula sehemu za
ardhi inayotumika kwa kilimo na shughuli nyengine za kimaendeleo na kijamii.
Alieleza kuwa jukumu kubwa la
taasisi hizo pamoja na vyombo vya habari ni kuandaa vipindi ambavyo vitatoa
taaluma kwa wananchi kuweza kujiepusha na vitendo vinavyochangia athari hizo,
ili Zanzibar ibaki salama.
Aidha, ujumbe huo ulimweleza
Waziri Fereji kuwa wakiwa Zanzibar tayari wametembelea maeneo mbali mbali,
ikiwemo kisiwani Pemba kwa ajili ya kujionea athari za mabadiliko ya tabianchi,
pamoja na kufanya mahojiano na wananchi wa maeneo tafauti juu ya chanzo na
matokeo ya athari hizo.
Walisema lengo lao ni kuandaa
vipindi vitakavyo tolewa kwa watazamaji, ili wananchi waweze kuwa na uelewa
mpana zaidi juu ya mabadiliko ya tabianchi, athari zake na njia muafaka za
kuweza kuchukua kujilinda.
No comments:
Post a Comment