Na Kauthar Abdalla
IPO haja ya kurejeshwa malezi ya pamoja katika jamii
pamoja na kuimarisha ndoa ili kutunza familia na watoto kuepukane vitendo vya
udhalilishaji.
Mjumbe kutoka Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) Zanzibar, Sharifa Maulid, alisema hayo
katika kongamano la wazee juu ya hifadhi ya mtoto na mapambano ya udhalilishaji
katika ukumbi wa hoteli ya Mazsons Shangani mjini Unguja wakati akiwasilisha mada ya udhalilishaji.
Alisema mfumo wa malezi kwa
watoto umebadilika tofauti na ilivyokuwa zamani na kwamba ongezeko la talaka
kwa wanandoa linachangia kwa kiasi kikubwa kudhalilishwa watoto kwani wanakosa
matunzo yanayostahiki.
Aidha alisema vitendo vya
udhalilishaji kwa watoto vinawaathiri kiakili, kimwili na kisaikolojia hali
ambayo inampelekea mtoto kukosa haki zake za msingi.
Kaimu Mkurugenzi kijiji cha
kulelea watoto yatima (SOS) Salum Abrahman Salum, alisema ni wakati sasa kwa
taifa kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji.
Alisema kutokana na hali hiyo
taifa halitakuwa na mtetezi na siku zote litakuwa tegemezi hali ambayo
itapelekea kukosekana maendeleo endelevu nchini.
Hata hivyo, alisema kumekuwa na
changamoto ya baadhi ya taasisi na familia kuchukua madaraka waliyonayo kutatua
kesi hizo kwa njia ya kienyeji.
Baadhi ya washiriki wa
kongamano hilo, walisema ni bora wakarudishwa walimu wenye hisia za kidini
katika skuli za serikali na binafsi na katika vyuo vya madrasa ili wawafahamishe
watoto juu ya mwenendo mzima wa maisha unavyokwenda.
No comments:
Post a Comment