Habari za Punde

Maalim Seif Akabidhi Fedha kwa Mwakilishi wa Mtoni

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi msaada wa fedha taslim shilingi milioni nne na laki nne kwa Mwakilishi wa jimbo la Mtoni, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Madrasa TWUWA iliyopo Mtoni Kigomeni katika jimbo hilo. (Picha na Salmin Said, OMKR).

Na Khamis Haji OMKR.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuongezeka kwa matendo maovu katika jamii yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya kunachangiwa na kuwepo vijana wengi waliokosa elimu sahihi ya malezi na misingi ya maadili mema.

Maalim Seif ameyasema hayo leo wakati alipokuwa akiwahutubia wazazi, walimu na wanafunzi wa Madrasa TWUWA ya Mtoni Kigomeni, Wilaya ya Magharibi Unguja, wakati alipofika kuangalia maendeleo ya Madrasa hiyo, pamoja kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Makamu wa Kwanza wa Rais amesema iwapo jamii itatoa kipaumbele kwa elimu ya maandalizi itakayo wajenga watoto katika misingi bora ya maadili mema, Taifa litaweza kuepukana matatizo mengi, ikiwemo balaa la vijana kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya.

Hata hivyo, Makamu wa Kwanza wa Rais amesifu juhudi zinazochukuliwa na walimu, wazazi na uongozi wa jimbo la Mtoni katika kusimamia elimu kwa watoto, bila ya kubagua elimu ya Dini au ya Dunia inayotolewa, kutokana na wazazi kuelewa umuhimu wa elimu hizo.

Katika risala yao, walimu wa Mdrasa wamesema miongoni mwa changamoto kubwa zinazo wakabili ni kuchakaa kwa madarasa, pamoja na kutokamilika kwa baadhi ya majengo ambayo yanahitajika kwa ajili ya kufundishia watoto wengi zaidi.

Akisoma risala yao, Mwalimu Semeni Abdallah amesema ipo haja kwa wazazi na wana jamii kuziona changamnoto hizo zinawagusa na baadaye waweze kusaidia juhudi za kuzipatia ufumbuzi.

Amesema Madrasa hiyo ni kituo muhimu cha taaluma kwa watoto na wananchi wengi wa eneo la Mtoni kwa sababu kuna wanafunzi wengi wanaonufaika, ikiwemo baadhi ya wazee ambapo pia hutumia fursa ya kuwepo kwa Madrsa hiyo kujipatia na kujiongezea elimu itakayo wasaidia hapa Duniani na Akhera.

Katika hafla hiyo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad alikabidhi jumla ya shilingi milioni 4.4 kwa Mwakilishi wa jimbo la Mtoni, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, kwa ajili ya kuendeleza shughuli za ujenzi wa Madrasa hiyo.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.