Habari za Punde

Dk Shein : Jitihada kubwa zimefanyika katika kutekeleza Miradi ya MCC



  
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                                                           23.10.2014
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza matumaini makubwa yaliopo kwa Tanzania ikiwemo Zanzibar katika uendelezaji wa awamu ya pili ya miradi inayodhaminiwa na Mfuko wa Changamoto za Millenia (MCC) kutokana na mafanikio ya awamu ya kwanza.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo kati yake na Balozi wa Marekani nchini, Tanzania Mhe. Mark Bradley Childress aliefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya mazungumzo na Mhe. Rais.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alimueleza Balozi Childress kuwa jitihada kubwa zimefanyika katika kutekeleza miradi ya MCC hapa nchini na kuweza kupata mafanikio makubwa, hivyo ni imani yake kubwa kuwa awamu ya pili ya mfuko huo itaendelezwa.

Hata hivyo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Marekani kutokana na misaada yake mbali mbali inayoisaidia Zanzibar ikiwemo miradi ya maendeleo kupitia Mfuko huo wa Changamoto za Millenia wa Watu wa Marekani (MCC) na miradi mengine.

Aidha, Dk. Shein alipongeza azma ya Marekani ya kujenga ghala la dawa huko kisiwani Pemba hatua ambayo aliielezea kuwa ni miongoni mwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya Unguja na Pemba.

Dk. Shein alieleza kuwa juhudi hizo vilevile, ni katika kuhakikisha huduma za afya zinawafikia wananchi wa Zanzibar kwa ukaribu na haraka zaidi sambamba na uhifadhi wa dawa hizo kitaalamu.


Pamoja na hayo, Dk. Shein alimueleza balozi huyo wa Marekani azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya umeme hapa nchini kwa kutumia rasilimali zisizorejesheka ikiwemo upepo na nyenginezo.

Kutokana na juhudi hizo, Dk. Shein alimueleza Balozi Childress kuwa azma ya Marekani katika kuunga mkono miradi mbali mbali ikiwemo ya umeme itasaidia katika kufikia malengo ya juhudi hizo katika kukuza uchumi na kuimarisha shughuli za kijamii.

Dk. Shein pia, alimueleza Balozi huyo kuwa Marekani inakaribishwa kuekeza hapa nchini na kueleza kuwa Mamlaka ya Maeneo Huru na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) imekuwa ikifanya juhudi za makusudi katika utoaji huduma mbali mbali kwa wawekezaji.

Nae Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Mark Bradley Childress alipongeza mafanikio yaliopatikana hapa nchini kupitia ufadhili wa Mfuko wa Changamoto za Millenia (MCC) awamu ya kwanza.

Balozi huyo alieleza kuwa juhudi kubwa zimefanywa katika kuhakikisha miradi hiyo inapata mafanikio makubwa hapa nchini.

Aidha, Balozi  Childress alieleza azma ya nchi yake kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika ujenzi wa ghala la dawa la kisasa huko kisiwani Pemba, mchakato ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Alieleza kuwa kama ilivyofanya nchi yake kupitia Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kuunga mkono ujenzi wa ghala jipya la dawa la kisasa lililojengwa huko Maruhubi nje kidogo ya mji wa Zanzibar pia, itafanya kama hivyo kwa upande wa kisiwani Pemba.

Sambamba na hayo, Balozi huyo alieleza azma ya nchi yake ya kuekeza hapa Zanzibar katika sekta ya ujenzi wa hoteli za kisasa za kitalii.

Pamoja na hayo, Balozi Childress alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.