Habari za Punde

Waziri Mbarouk asifu uhusiano wa Z’bar, Oman

Na Mwandishi wetu, Muscat
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mhe. Said Ali Mbarouk, ameuelezea ushirikiano baina ya Oman na Zanzibar kuwa daima utakuwepo na utaendelea kukua kutokana na kutanuka kwa maeneo mapya ya ushirikiano katika nyanja mbali mbali za maendeleo.

Alisema ni jambo la faraja kuona hivi sasa Zanzibar na Oman zinatambua umuhimu wa kutanua maeneo hayo ya ushirikiano katika sekta za uchumi, utalii na michezo kwa lengo la  kuwanufaisha watu wa pande zote mbili.

Aliyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na Mawaziri  wa sekta za Habari, Michezo, Utamaduni na Utalii mjini Muscat Oman jana akiwa katika ziara yake ya siku nne ya kukutana na viongozi mbali mbali wa nchi hiyo kwa lengo la kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.

Abdulmunim bin Mansoor bin Said Al Hasani
Mapema akizungumza na Waziri wa Habari wa Oman, Sheikh Dk. Abdulmunim bin Mansoor bin Said Al Hasani,alitoa shukrani zake kwa serikali ya Oman kwa misaada yake kwa Zanzibar na kusifu nidhamu   ya vyombo vya habari vya nchi hiyo katika kuwaunganisha watu na kuwawezesha kujenga uchumi imara.


Alisema hatua hiyo ya  mfano wa kuigwa inatokana na usimamizi  madhubuti  kwa vyombo vya habari na kujali kuwajibika kwa jamii kwa vile vinatoa nafasi ya kuwapatia taarifa za kutosha juu ya harakati za kujiendeleza na kujenga ustawi na maendeleo   yao.

Alishauri haja ya kuwepo na utaratibu wa kubadilishana wataalamu na vipindi ili kila nchi iweze kujifunza kutoka upande mwengine kwa  kutambua maendeleo yanayofikiwa na kila upande na hivyo kutoa fursa za kuwawezesha vijana na vyombo vya habari kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao kwa pamoja hasa kwa vile ni tegemeo kubwa la taifa katika kujenga uchumi.

Katika ziara yake hiyo,Waziri Mbarouk pia alipata fursa ya kubadilishana mawazo na Naibu Waziri wa Utamaduni na Mambo ya Kale, Sheikh Hamad Hilal Al Maamari na Waziri wa Michezo, Sheikh Shallal Saad Mohammed Al Saad na kujikita  zaidi katika masuala ya kubadilishana wataalamu wa michezo na kuyahuisha majengo ya kihistoria yenye mnasaba na Oman.

Wakati huo huo,  ameiomba  Oman kufungua fursa nyengine kwa kuisaidia Zanzibar katika kuanzisha hoteli za kitalii za halali utaratibu ambao Oman tayari imeuanzisha na kupata mafanikio.

Alisema utaratibu wa hoteli kama hizo ni muafaka katika visiwa vya Zanzibar kwa vile zitaongeza soko la idadi ya watalii wanaohitaji kupumzika katika maeneo yenye utulivu wa maadili ya kidini na kiutamaduni.

Pia alipata fursa ya kushiriki katika  karamu rasmi iliyoandaliwa kwa ajili yake  na ujumbe  wa watu watatu aliyofuatana na mwenyeji wake Waziri wa Habari wa Oman, Sheikh, Dk. Abdulmunim bin Mansoor bin Said Al Hasani,iliyofanyika katika jumba la serikali la Opera mjini Muscat.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.