Habari za Punde

DK. Shein Awahakikishia Wananchi :Tunashughulikia Suala la Ardhi.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                    24 Novemba, 2014
TAARIFA KWA VYOMBOVYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua za haraka shughulikia matatizo ya ardhi katika mashamba ya Selemu, Dole na Ndunduke katika wilaya ya Magharibi lakini kwa utaratibu unaozingatia sheria ya Ardhi ya Zanzibar.
 Aliwakumbusha wananchi kuwa sheria ya ardhi inatamka wazi kuwa ardhi yote ni mali ya serikali hivyo wananchi waliomilikishwa ardhi hiyo wanapaswa kutii sheria na masharti yanayoambatana na sheria hiyo kuhusu matumizi ya ardhi husika.
 Dk. Shein ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na viongozi wa mashina na maskani za Chama cha Mapinduzi wilaya ya Kichama ya Mfenesini Mkoa wa Magharibi katika siku yake ya nne ya kutembelea viongozi hao katika wilaya zote za Unguja na Pemba.
 “baadhi ya wananchi waliopata mashamba ya eka tatu wanayagawa viwanja, hii ni kinyume na sheria. Sisi tutalishughulikia tatizo hili kwa kufuata sheria na ikibidi tutafuta milki za baadhi ya watu hao” Dk. Shein alisisitiza.
 Katika risala ya viongozi hao pamoja na baadhi ya waliopata fursa ya kuzungumza katika mkutano huo walieleza tatizo la ardhi katika maeneo hayo hasa suala la baadhi ya mashamba hayo kugeuzwa maeneo ya makazi kinyume na matumizi yaliyokusudiwa.
 Katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Dk. Shein alieleza tangu kuingia madarakani amekuwa akiendesha serikali kwa kufuata Katiba na Sheria na kuongeza kuwa yeye si mgeni katika kuendesha serikali.
 Alibainisha kuwa mambo yote yanayotekelezwa na serikali hiyo yanafanyika kwa makubaliano likiwemo suala la Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambalo lilipitia hatua zote katika serikali na kutekelezwa kwa mujibu wa sheria hiyo hivyo haoni sababu kujitokeza mtu akasema serikali hiyo inaendeshwa kibabe.

 “Mimi si mgeni katika uongozi nimepitia ngazi mbalimbali kuanzia Naibu Waziri, nimekuwa Waziri kamili, Makamu wa Rais na kufanya kazi na Marais wa wawili kwa mafanikio hadi leo nimekuwa Rais wa Zanzibar hivyo si mgeni katia kuongoza nchi” Dk. Shein alieleza.
 Aliongeza kuwa kutokana na uongozi wake bora na makini, viongozi mbalimbali wanaofika nchini wamekuwa wakisifu uongozi wake na serikali kwa jumla kwa kuimarisha amani na utulivu ambao umesaidia serikali kutekeleza majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo.
 Matokeo yake alieleza Serikali imekuwa ikitekeleza vyema Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa hivyo anaamini kuwa wananchi wataendelea kukichagua chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.  
 Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai akimkaribisha Dk. Shein alieleza kuwa kumekuwepo na jitihada za makusudi za kupotosha wananchi juu ya Katiba Iliyopendekezwa kwa baadhi ya watu kueleza vitu ambavyo havihusiani na Katiba hiyo.
 “Tulikwenda katika Bunge Maalum la Katiba kuzungumzia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wala sio Katiba ya Zanzibar lakini wao wanaeleza mambo ambayo yanayopaswa kuzungumziwa na wananchi wa Zanzibar wenyewe wakati wa watakapozungumzia Katiba yao ya Zanzibar” alisema Naibu huyo huku akitolea mfano suala la ardhi.
 Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu pamoja na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.
 Dk. Shein anatarajiwa kuendelea na ziara yake kesho kwa kutembelea  wilaya ya Kati.     
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

                                               

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.