Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Viongozi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja akiwa katika jitihada zake za kuimarisha Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Mkoa huo,(kulia) Naibu Katibu Mkuu CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, na wa kwanza (kushoto) Mjumbe wa Kamati Kuu CCM Taifa Khadija Hassan Aboud akifuatiwa na Mwenyekiti wa CCM Kaskazini A Unguja Ali Makame Khamis, sambamba na jitihada hizo leo anatarajiwa kuanza kuzungumza na Viongozi mbali mbali wakiwemo Mabalozi na Wenyeviti wa Maskani wa Chama hicho katika Mikoa ya Pemba. [Picha na Ikulu.]
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 30.11.2014

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar
Dk. Ali Mohamed Shein amewataka vijana kuheshimu jitihada za wazee na viongozi wao
sambamba na maendeleo yaliopatikana hapa nchini ambayo yametokana na Mapinduzi
matukufu ya Januari 12, 1964.
Hayo aliyasema leo huko Chaani Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Mkoa wa Kaskazini
Unguja mara baada ya kulikagua Tawi la CCM la Chaani Mchezashauri ambapo
alipata fursa ya kusalimiana na WanaCCM na wananchi wa eneo hilo na viunga
vyake.
Katika nasaha zake Dk. Shein alisema kuwa vijana wanadhima kubwa ya
kuheshimu maendeleo yaliopatikana ikiwa ni pamoja na kuwaheshimu wazee na
viongozi wao wa nchi na kuwataka vijana wasihadaiwe.
Alisema kuwa vijana wanajukumu kubwa la kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi
matukufu ya Januari 12, 1964 pamoja na kusisitiza haja ya kuutunza na kuulindda
Muungano uliopo ambao unahistoria na mafanikio makubwa na kuwashangaa
wanaoupinga Muungano huo.
“Vijana msidharau watu, msiwadharau wazee na
viongozi wa nchi hii hakuna sababu ya kutukana watu heshimu na wewe
uheshimiwe... watu hawajui watokako..mtu kwao ndio ngao”alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa jambo lolote lililoasisiwa na ASP kuna kila
sababu ya kuliendeleza na kueleza kuwa watu wa Chaani pamoja na watu wa Mkoa
huo wa Kaskazini Unguja wanaheshima kubwa katika ukombozi wa nchi hii hivyo ni
lazima kuwajengea heshima.
Kutokana na hayo, Dk. Shein aliwataka wazee na wazazi kuwaeleza vijana
historia ya nchini hii sambamba na juhudi zilizofanywa na wazee hao katika
kuiokomboa kwa kufanya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na hatimae hivi leo
wananchi wanajitawala wenyewe.
Akieleza kuhusu historia ya Tawi hilo ambalo ni miongoni mwa Matawi ya
mwanzo yenye historia kubwa hapa nchini, Dk. Shein alisema kuwa juhudi
zitaendelea kuchukuliwa na CCM kwa kushirikiana viongozi pamoja na wanachama wa
chama hicho katika kuhakikisha Matawi yake yote ya Unguja na Pemba yanaimarika
na kwenda sambamba na uimara wa chama hicho.
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alisema kuwa ASP ndio chama
kilichopigania ukombozi wa Zanzibar hivyo kuna kila sababu ya kuheshimu juhudi
zake zikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Matawi ulioanzishwa wakati huo wa kudai
uhuru.
Nao WanaCCM wa Tawi hilo pamoja na viongozi wa Mkoa huo wa Kaskazini Unguja
walitoa shukurani kwa Dk. Shein kwa juhudi zake katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi
ya Mwaka 2010-2015 sambamba na hatua anazozichukua katika kuwaletea maendeleo
endelevu wananchi wa Zanzibar.
WanaCCM hao wameeleza kuridhishwa kwao na uongozi wa Dk. Shein na kuahidi
kuendelea kumuunga mkono katika kuiletea nchi maendeleo pamoja na kukiimarisha
chama chao ili kiendelee kushika hatamu huku wakieleza kuunga mkono Katiba
iliyopendekezwa.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422
Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment