Na Khamis Haji, OMKR
Norway imeihimiza Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na maelewano yaliyopo,
ambayo ni matunda ya maridhiano ya kisiasa yaliyozaa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa.
Wito huo umetolewa na Balozi wa
Norway nchini Tanzania, Mhe. Hanne Marie Kaarstad wakati akizungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe.
Maalim Seif Sharif Hamad, ofisini kwake Migombani mjini Zanzibar.
Alisema kutokana na uzoefu wa
hali ya siasa huko nyuma, hivi sasa Zanzibar imepiga hatua kubwa katika
kudumisha amani, maelewano na utulivu, mambo ambayo yemejenga mazingira mazuri
kwa serikali kujikita kwenye maendeleo na kwa wananchi kufanya shughuli zao
bila matatizo.
Naye, Maalim Seif,alisifu
ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na Norway na ameahidi Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar itafanya kila jitihada kuona ushirikiano huo unazidi kuimarika.
Alisema Norway imetoa mchango
wa kipekee katika kuhakikisha Zanzibar inapata mafanikio makubwa katika nyanja
mbali mbali, ikiwemo kudumishwa utulivu wa kisiasa pamoja na kusaidia sekta
mbali mbali za kiuchumi, maendeleo na kijamii.
Alisema mchango wa serikali ya
Norway katika kufanikisha kufikiwa maridhiano ya kisiasa yaliyozaa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa na Zanzibar ni wa kipekee na njia muafaka ya kuuenzi ni
kuhakikisha Zanzibar hairudi tena kwenye siasa za chuki na uhsama.
Aidha, alisema ili maridhiano
hayo yaweze kudumu, kasoro zinazojitokeza ambazo zinaweza kurejesha nyuma
taswira na dhamira njema ya kufikiwa kwake, hazina budi kupatiwa ufumbuzi kwa
haraka pale zinapojitokeza, ili kuzidi kujengwa hali ya umoja na kuaminiana.
Alizitaja baadhi ya chanagamoto
zilizopo kuwa ni maridhiano na maelewano hayo kueleweka na kutekelezwa zaidi
katika ngazi za juu serikalini, ambapo mkazo zaidi unahitajika katika ngazi za chini.
Alisema ipo haja kwa serikali
na taasisi zote zinazosimamia haki kutekeleza wajibu huo na kila mtu aweze
kupata haki anayostahili, bila kujali itikadi yake kisiasa, kabila au dini
yake.
Alisifu mchango wa Norway kwa
Zanzibar katika kusaidia kukuza demokrasia, upatikanaji wa nishati ya umeme
vijijini, pamoja na kusifu mchango mkubwa wa nchi hiyo katika suala la uhifadhi
wa mazingira Zanzibar.
Alitoa wito kwa Noway kuzidi
kushirikiana na Zanzibar katika nyanja za uvuvi wa bahari kuu, sekta za elimu
na afya na kuendeleza elimu ya uhifadhi na mazingira, ili kuilinda Zanzibar na
hatari inayojitokeza ya eneo lake la ardhi kuliwa na maji ya bahari.

No comments:
Post a Comment