Habari za Punde

Akutwa amekufa ufukweni

Na Masanja Mabula, Pemba
Mtu mmoja amekutwa amekufa maji kando ya ufukwe wa bahari kufuatia chombo chake cha kuvulia  kupigwa na dhoruba kali na kisha kupinduka na kuzama baharini.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa kaskazini Pemba, Shekhan Mohammed Shekhan, tukio hilo limetokea siku ya Alkhamis ya Januari 15 mwaka huu  saa 7:00 mchana baada ya mtu huyo kutoonekana kwa muda mrefu.

Alimtaja mtu huyo kuwa ni Ali Omar Juma (56) mkaazi wa kisiwa cha Fundo ambaye aliondoka nyumbani kwake juzi asubuhi kuelekea baharini kwa shughuli  za uvuvi .

Alisema  jeshi la polisi limechukua hatua za kitaalamu ikiwa ni pamoja na kupeleka daktari kwa ajili ya kufanyia uchunguzi ambapo uchunguzi wa daktari umebaini mtu huyo alikufa baada ya kunywa maji mengi.


Kufuatia tukio hilo, Kamanda Shekhan aliwataka wananchi hususani wavuvi kuacha tabia ya kwenda bahari mmoja mmoja bali wawe na utaratibu wa kufuatana wawili wawili ili kuweza kusaidiana panapotokea matatizo.


Aidha aliwataka watu wanaotumia bahari kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki cha upepo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.