Habari za Punde

Polisi wamuhoji mtuhumiwa wa miripuko

Na Mariam Cyprian, Tanga
Mtuhumiwa Ephata Edward aliekuwa na miripuko 475 aina ya baruti iliyokamatwa na askari waliokuwa doria mkoani Tanga, anaendelea kuhojiwa na jeshi la polisi kuhusiana na tuhuma za kusafirisha miripuko hiyo bila kibali.

Mtuhumiwa ambaye ni mkazi wa jijini Arusha amekabidhiwa mikononi mwa  makashero wa polisi Januari13 siku moja baada ya miripuko hiyo kukamatwa eneo la njia kuu ya barabara ya Kilimanjaro- Tanga- Dar es Salaam.

Miripuko hiyo ilikuwa  ikisafirishwa kwa gari la abiria ikipelekwa jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga,Frasser Kashai, ameliambia gazeti hili kuwa askari wake wanaendelea kumuhoji mtuhumiwa na wakati wowote atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili baada ya upelelezi kukamilika.


"Mtuhumiwa yupo mikononi mwetu tunaendelea naye,tunataka kujua kwanini asafirishe miripukobila kibali,alikuwa anaipeleka wapi na kufanya nini,kwa kuwa miripuko yenyewe ni hatari na kibaya zaidi ilikuwa ikisafirishwa kwenye gari la abiria,"alisema.

''Mwenye mamlaka ya kusafirisha miripuko au kumiliki ni wale wenye machimbo ya madini kwa ajili ya kupasulia miamba na wenye vibali maalumu huyo hatukumuelewa kwa kuwa alikuwa hana kitu chochote cha kuufanya mzigo huo uwe halali,” alisema.

Kamanda Kashai alipiga marufuku baadhi ya watu kumiliki miripuko ya aina hiyo bila vibali kwa kuwa ni hatari na inaweza kutumiwa vibaya na watu wasiokuwa waadilifu kusababisha madhara.


Hili ni tukio la pili la miripuko ya aina hiyo kukamatwa na jeshi la polisi mkoani Tanga lakini jitihada za wananchi zinahitajika katika kutoa taarifa za watu wa namna hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.