Habari za Punde

Balozi Seif Afanya ziara hospitali ya Mnazi Mmoja.

 Muuguzi wa Zamu katika Hopitali kuu ya Mnazi Mmoja wodi ya Watoto Bibi Mary Jadi akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif msongamano wa watoto wanaoungua moto ambao hulazimika kulazwa wagonjwa watatu kwa kitgand kimoja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpa pole Mtoto mgonjwa Nasrya Kombo aliyelazwa Hospitali kuu ya Mnazi mmoja baada ya kuungua kiwa moto.Pembeni ya Balozi Seif ni Muuguzi wa Zamu katika Hopitali kuu ya Mnazi Mmoja wodi ya Watoto Bibi Mary Jadi.
Balozi Seif akimpa pole Bibi Wanu Rajab aliyelazwa Hospital Kuu ya Mnazi mmoja yeye na Mtoto wake baada ya kibanda wanachoishi katika shughuli za Kilimo kuwaka moto katika Kijiji cha Kirombero.(Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.)

Na Othman Khamis OMPR. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikal  ya Mapinduzi ya Zanzibar ina nia ya kutaka kujenga Wodi  maalum kwa ajili ya  kulazwa watoto wadogo wanaopatwa na majanga  mbali mbali ya kuunguwa kwa moto.

Balozi seif alisema hayo wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua watoto walioungua moto ambao wamelazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar mara baada ya kumalizika kwa kilele cha maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaelewa vizuri matatizo yanayowakumba watoto wanaopatwa na majanga hayo ya moto ambao hulazimika kulazwa  zaidi ya mtoto mmoja kwenye kitanda kimoja.

Balozi Seif alisema hali hiyo mbali ya kwamba haipendezi  kuonekana lakini pia inaweza kusababisha maambukizi ya maradhi mbali mbali kwa watoto wanaolazwa pamoja.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka wazazi na walezi kuwa waangalifu na matukio ya majanga ya  moto ambayo huonekana  kushamiri zaidi katika baadhi ya vipindi na kusababisha vifo na hata vilema kwa watoto wao.

Mapema Muuguzi wa Zamu wa Wodi ya Watoto katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja Bibi Mary Jadi alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ajali za moto zinazowakumba watoto katika maeneo mbali mbali hapa nchini zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku.

Bibi Mary alisema ipo haja ya kufanywa kwa utafiti wa kina kuelewa sababu zinazopelekea kuongezeka kwa majanga hayo  na juhudi zifanywe kwa makusudi ili kupunguza au kuondosha kabisa tatizo hilo ambalo huonekana kushamiri zaidi katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani.

2 comments:

  1. Hakuna haja ya utafiti wa kuongezeka ajali za moto kwa watoto.

    Mambo makubwa yanayosababisha ni pamoja ni: 1) Umasikini wa kupindukia ambao haumpi mzazi au mlezi wa mtoto muda wa kumlinda mtoto kutokana na majanga; na la pili ni, ukosefu wa sheria ya kuwabana wazazi kwamba ni mtoto chini ya miaka 10/13 haruhusiwi kuachwa peke yake mahali popote. Au mtoto chini ya miaka 10 anapopatwa na janga lolote, basi ni lazima mzazi ajieleze au afikishwe mbele ya sheria. Nadhani kwa mkakati huo namba 2, walezi wa watoto watatia akili na kuwa hadhir na walezi.

    Hivyo, kwa yote haya mawili, bado kosa ni la serikali kutokuondoa umasikni na kutokuwalinda watoto wadogo ambao bado hawajawa na akili yeyote.

    ReplyDelete
  2. nakubaliana na mchangiaji hapo juu ingawa siwafiki kuwafikisha mbele ya sheria kwa sababu nchi yetu haina wanasheria kuna madalali tu , watawatesa hao wazazi na hakuna tija yoyote ile , hakuna sababu ya kutunga sheria kama hio , utasababisha ulaji tu kwa mapolisi na watu wa sheria, Njia ni kuwaelimisha kwa njia mbalimbali wazazi jinsi ya kuwalinda watoto wao , hakuna mzazi anayetaka mwanawe aumie , hali zetu duni za kimaisha hutufanya tuwe tumeshughulika kutafuta riziki

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.