Katika michuano iliyoshirikisha timu kubwa za Simba, Yanga, Azam, Mtibwa na mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi KCCA ya Uganda, usingetarajia kuziona timu za Zanzibar zikifurukuta.
Ni kwa sababu ya rekodi zilizopo na hata matokeo ya mwanzoni mwa michuano hiyo ya mwaka huu kwenye Uwanja wa Amaan.
Yanga ilishinda mechi zake mbili za kwanza za michuano hiyo mwaka huu kwa kutoa vipigo vikubwa zaidi vya 4-0 kwa timu za Zanzibar za Polisi na Taifa ya Jang’ombe katika hatua ya makundi.
Simba pia iliifunga Taifa ya Jang’ombe 4-0 katika hatua ya robo fainali.
Vipigo hivyo vikubwa ndivyo vilivyomfanya kocha wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm kutoa wazo zuri la kimaendeleo kwamba mamlaka za soka za bara na Zanzibar, TFF na ZFA, zikae pamoja na kuangalia uwezekano ili timu za Zanzibar na Bara zishiriki ligi moja.
Ni wazo lenye ‘akili’ sana kwa kuzingatia namna ambavyo timu za Zanzibar zimekuwa zikionekana ‘vibonde’ kila zinapokutana dhidi ya timu za Bara – na ushahidi wa matokeo pia unaonyesha.
Hata rais wa TFF, Jamal Malinzi aliyekuwapo Zanzibar alikubaliana na maoni ya Pluijm, lakini kwa kufahamu ugumu unaoweza kuwapo katika kuunganisha ligi hizo hasa kutokana na sababu za kisiasa, akatoa pendekezo linaloweza kuafikiwa kirahisi la kuwa na ligi ya ‘Super 8’ itakayounganisha timu nne za Zanzibar na nne za Bara.
Lakini wakati hayo yakiendelea, Pluijm na Yanga yake walishangazwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu ya Shaba katika mechi yao ya mwisho ya Kundi A.
Licha ya kushinda 1-0 kupitia ‘goli la usiku’ la kiungo Mbrazil Andrey Coutinho, Yanga iliyojaa wachezaji wa pesa nyingi siku hiyo walikiona chamoto kutoka kwa vijana wadogowadogo wa Shaba.
Walilazimika kupambana hadi dakika ya mwisho ili kupata ushindi huo ugumu.
Pluijm na Watanzania kwa ujumla walishangaa zaidi siku miamba hao wa soka nchini walipokumbana na kichapo cha 1-0 kilichowafanya waage mashindano hayo mikononi mwa vinara wa ligi kuu ya Zanzibar, JKU katika hatua ya robo fainali.
Mabingwa watetezi KCCA walijikuta wakiaga mashindano hayo katika hatua ya robo fainali pia dhidi ya Wazanzibar wengine, timu ya Polisi.
Miamba wengine wa soka nchini, Simba licha ya kufika fainali walikumbana na wakati mgumu kuzibwaga timu za Zanzibar.
Licha ya kushinda mechi zao zote dhidi ya timu za Zanzibar, Simba ni mara moja iliweza kufunga goli zaidi ya moja, tena ilifanya hivyo dhidi ya timu ya daraja la pili ya Taifa ya Jang’ombe ambayo haikupewa muda wa kupumzika kwa kuwekewa ratiba mbaya ya kucheza mechi mbili ndani ya 27.
Licha ya kushinda kwa magoli 4-0 katika mechi hiyo, Simba hawakupata bao katika kipindi cha kwanza kabla ya kuja kufungua mvua hiyo ya mabao katika kipindi cha pili ambacho wapinzani wao hao waliocheza mechi mfululizo wakionekana tayari walishachoka kabisa.
Mifano ya matokeo hayo ndiyo iliyompa nguvu Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, aliyekuwa mgeni rasmi katika mechi ya robo fainali baina ya Simba na Polisi ambayo Wekundu wa Msimbazi walishinda kwa tabu goli 1-0, kuthubutu kusema kwamba Zanzibar kuna vipaji sana vinavyohitaji kuendelezwa.
Kiongozi huyo wa kisiasa alisifu michuano hiyo maalum ya kusherehekea Mapinduzi ya Zanzibar na kusema kwamba kilichoonekana uwanjani kimethibitisha kwamba Zanzibar kuna vipaji vingi lakini vinahitaji kuendelezwa ili kuiletea sifa nchi.
Na hakika NIPASHE hicho ndicho tulichokiona katika mashindano ya mwaka huu.
Kitendo cha timu mbili za Zanzibar, Polisi na JKU, kufika hatua ya nusu fainali na kuziacha nje timu za Yanga, mabingwa wa Tanzania Bara Azam na waliokuwa mabingwa watetezi wa Mapinduzi, KCCA, kilikuwa ni kitu ambacho hakikuja mawazoni mwa wengi wakati michuano hiyo ikianza.
Kama hakuna aliyetarajia hayo na yakatokea, ni uthibitisho kwamba soka la Zanzibar ambalo limekuwa likidharauliwa, lina kitu. Tena kitu kikubwa.
Na kitu hiki ndicho ambacho leo hii Watanzania na mamlaka za kusimamia mchezo huu nchini zinapaswa kukisimamia ili soka letu lipige hatua kutokea hapa lilipodumaa kwa miaka mingi sasa.
Lakini mafanikio ya kwenye soka hayaji kwa miujiza. Ni kwa mipango sahihi, mipango ya kupika vipaji vipya kila uchao.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment