Habari za Punde

Hotuba ya Rais, Dk Shein kuadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi

HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHE. DK. ALI MOHAMED SHEIN, KATIKA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 51 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR, AMAAN STADIUM TAREHE 12 JANUARI, 2015
 
Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
 
Mheshimiwa Dk. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
 
Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
 
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar;
 
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar;
 
Mheshimiwa Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
 
Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
 
Mheshimiwa Dk. Salmin Amour Juma,  Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
 
Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
 
Viongozi Wakuu Wastaafu Mliohudhuria;
 
Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar;
 
Mheshimiwa Mama Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
 
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar;
 
Mheshimiwa Othman Chande Mohamed, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
 
Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
 
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
 
Mheshimiwa Abdalla Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi;
 
Waheshimiwa Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa;
 
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
 
Assalaam Alaikum,
 
Namshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa Mbingu na Ardhi na Mwenye uwezo wa kila kitu kwa kutujaalia uhai na uzima wa afya, tukaweza kukusanyika hapa leo kwa kusherehekea miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ya tarehe 12 Januari, 1964.  Namuomba Mwenyezi Mungu aibariki shughuli yetu hii iwe ya mafanikio.

Pili, natoa shukurani zangu na za wananchi wa Zanzibar kwako Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuja kuungana nasi katika sherehe zetu hizi adhimu na muhimu.
 
Shukurani zetu vile vile zije kwenu viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, mliopo madarakani na mliostaafu, Mabalozi wa nchi mbali mbali, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa dini na vyama vya siasa na wananchi wote, kwa kuhudhuria kwa wingi kwenye sherehe hizi.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Mwaka jana, katika tarehe kama ya leo tuliadhimisha sherehe za kutimiza miaka 50 tangu tulipojikomboa, tarehe 12 Januari, 1964.  Nawapongeza wale waliozifanikisha sherehe hizo pamoja na wananchi wote kwa mahudhurio yenu katika hatua zote za maadhimisho hayo.
 
Leo tunaadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi na tumefurahi sana kwa mafanikio tuliyoyapata katika kutekeleza dhamira za Mapinduzi hayo Matukufu.  Ni dhahiri kwetu sote kwamba Mapinduzi ndiyo yaliyotukomboa wanyonge na kusimamisha utawala wa haki na usawa. Tutaendelea kuwakumbuka wazee wetu Waasisi wa Chama cha Afro Shirazi walioongozwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, kwa ushujaa wao na jitihada zao za kupigania haki, kuleta usawa na maelewano na kuondoa kila pingamizi walizokuwa wakizipata wananchi wa Unguja na Pemba.   

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Pamoja na ufanisi wa utekelezaji wa dhamira ya Mapinduzi, ambayo nitaielezea baadae, tunaona fahari kubwa kwamba mwaka uliopita, tulisherehekea kutimia miaka 50 ya Muungano wa nchi zetu mbili zilizokuwa huru na kuanzishwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Tutaendelea kuutunza, kuuheshimu na kuuenzi Muungano huu ambao ndio chombo kikubwa cha amani; umoja na mshikamano wa wananchi na maendeleo yetu.Vile vile, sherehe zetu za leo zinajumuisha kumalizika miaka minne ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa. Kwa hakika, tumefanikiwa kufanya mengi katika miaka minne hiyo, yakiwemo maendeleo ya uchumi wetu na maendeleo ya jamii, pamoja na kudumisha amani, utulivu na mshikamano. Nawapongeza viongozi na wananchi wote walioshiriki katika kuleta mafanikio haya.


Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Sasa nitaelezea baadhi ya mafanikio yaliyopatikana baada ya Utekelezaji wa Dira 2020, MKUZA II, Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010-2015 na Malengo ya Milenia. Miongoni mwa mafanikio muhimu yaliyopatikana ni kuwepo kwa amani, umoja na mshikamano wa Wazanzibari na Watanzania wote kwa jumla, mambo ambayo yamechangia sana kuongeza kasi yetu ya maendeleo.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Katika kutekeleza matakwa ya Katiba, Serikali imeifanyia marekebisho Sheria Nam. 5 ya Tume ya Mipango na kutunga Sheria Nam. 3 ya mwaka 2012. Tume ya Mipango ni chombo cha juu cha kupanga, kuratibu na kusimamia mipango ya kiuchumi na ya kijamii.Katika kipindi hiki cha miaka minne, Tume imesimamia utekelezaji wa miaka mitano ya MKUZA na imesimamia utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa kwa ajili ya utekelezaji wa “Matokeo kwa Ustawi” (Results for Prosperity) katika Utalii, Mazingira na Utafutaji wa Fedha.  Vile vile, Tume imekamilisha vipaumbele vya utafiti kwa Zanzibar, imefanya uchambuzi wa uchumi na jamii na kutoa muelekeo.  Kadhalika imetoa vipaumbele vya Zanzibar katika matayarisho ya Bajeti na Mpango wa Maendeleo, imesimamia tafiti za Utumishi na imeandaa vipaumbele vya mafunzo kwa ajili ya mahitaji ya wataalamu mbali mbali.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Uchumi wetu umekuwa ukikua mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2010 hadi 2014. Pato la Taifa limeongezeka kutoka TZS bilioni 942.3 mwaka 2010 hadi kufikia TZS bilioni 1,442.8 katika mwaka 2013, sawa na ongezeko la asilimia 53.  Uchumi wetu umekua kutoka asilimia 6.4 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.4 mwaka 2013.  Pato la Mtu Binafsi limeongezeka kwa wastani wa asilimia 38, kutoka TZS 778,000 (USD 558) mwaka 2010 na kufikia TZS milioni 1.077 (USD 667) mwaka 2013.Kwa mwaka 2014, kasi ya kupanda kwa bei za bidhaa na huduma (mfumko wa bei) ilibaki katika wastani wa tarakimu moja, asilimia 5.6, ikilinganishwa na asilimia 6.1 kwa mwaka 2010.  Katika mwaka 2015 uchumi wetu unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 7.8 na Pato la Taifa litaongezeka hadi kufikia TZS bilioni 1,555.1.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Kufuatia utaratibu unaokubalika duniani kote wa kubadilisha mwaka wa kuanzia hesabu za makadirio ya takwimu za Pato la Taifa kwa lengo la kuziimarisha takwimu ili zilingane na mabadiliko ya kiuchumi yanayotokea,  mwaka 2014, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mapitio hayo.  Ofisi hio imerekebisha mwaka wa kuanzia hesabu za Pato la Taifa kutoka bei za mwaka 2001 na sasa zitatumiwa takwimu za bei za mwaka 2007.  Kwa msingi huo, thamani ya Pato la Taifa imeongezeka kutoka TZS bilioni 1,442.8 mwaka 2013 kwa bei za mwaka 2001 mpaka TZS bilioni 1,859 kwa bei za mwaka 2007. Kadhalika, ongezeko hilo la thamani la Pato la Taifa limeongeza wastani wa Pato la kila Mzanzibari kutoka TZS Milioni 1.077 (US$656) kwa bei za mwaka 2001 hadi kufikia TZS Milioni 1.39 (US$ 870) kwa bei za mwaka 2007.
 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeongeza juhudi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato pamoja na kupanua wigo wa vianzio vya mapato hayo.  Katika kipindi cha miaka minne, 2006/2007 hadi 2009/2010 Serikali ilikusanya mapato ya TZS bilioni 484; ikilinganishwa na TZS. bilioni 997 zilizokusanywa katika kipindi cha 2010/2011 mpaka 2013/2014.  Takwimu hizi zinaonesha ongezeko la asilimia 106.  Natoa pongezi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania na Bodi ya Mapato Zanzibar kwa kazi nzuri waliyoifanya.

Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuimarisha mazingira ya biashara kwa kushirikiana na sekta binafsi.  Juhudi hizo zimeiwezesha Zanzibar kusafirisha bidhaa zenye thamani ya TZS milioni 94,235.8 kwa mwaka 2014 kutoka bidhaa zenye thamani ya TZS milioni 87,799.6 kwa mwaka 2013, sawa na ongezeko la asilimia 7.3. Usafirishaji wa bidhaa kwenda Tanzania Bara umeongezeka kutoka TZS milioni 71,396.8 mwaka 2011 hadi kufikia TZS milioni 642,110.3 mwaka 2014. Ongezeko hilo ambalo ni sawa na mara tisa, limechangia katika kuongeza mapato ya Serikali na ajira.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Kwa upande wa zao la karafuu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua juhudi za kulifufua zao hilo, ambapo mpango wa miaka kumi umeandaliwa na umeanza kutekelezwa.  Katika kipindi cha miaka mitatu ya kwanza ya mpango huo; 2011/12 - 2013/2014, jumla ya tani 11,477 za karafuu zenye thamani ya US$ milioni 130.82 zilisafirishwa na kuuzwa nje ya nchi. Kiwango hicho ni sawa na ongezeko la tani 2,792 ambalo ni sawa na asilimia 32.1 ikilinganishwa na mwaka 2008/09 - 2010/2011.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Serikali imetimiza ahadi yake iliyoitoa mwaka 2011 ya kuwalipa wakulima wa zao la karafuu asilimia 80 ya bei ya karafuu ya soko la dunia. Karafuu za daraja la kwanza zinanunuliwa kwa bei ya TZS 14,000 kwa kilo badala ya TZS 5,000 kwa kilo, bei iliyokuwepo mwaka 2010.  Ongezeko hili ni sawa na asilimia 180.  Kadhalika, vituo vipya vya ununuzi na uuzaji wa karafuu vimejengwa, vituo vya zamani vimekarabatiwa na huduma zote muhimu zinapatikana kwenye vituo hivyo. Tumefanikiwa sana katika kupambana na magendo ya karafuu na wananchi wanauza karafuu zao katika vituo vya ZSTC. Tunawashukuru Wananchi na Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kazi nzuri walioifanya ya kushirikiana na Serikali katika kupambana na magendo ya karafuu.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Kuhusu uwekezaji, katika kipindi cha 2010-2014 jumla ya miradi 141 imeidhinishwa na kuwekezwa nchini kupitia Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA). Miradi hiyo itakapomalizika itaingiza jumla ya mtaji wa US$ milioni 1,469 na kutoa nafasi za ajira 5,969.Kupitia ZIPA, Serikali imo katika hatua ya utekelezaji wa Mpango wa uendelezaji wa mji mpya wa kisasa katika Maeneo Huru ya Uchumi ya Fumba ili kuvutia wawekezaji.  Mji huu utakuwa na mitaa ya biashara na eneo la viwanda lenye ukubwa wa kiasi cha hekta 100. Mipango yetu imejumuisha kujenga kituo cha kisasa cha mikutano cha kimataifa na maeneo ya kupumzikia wananchi na wageni.  Tayari shughuli za uwekezaji wa miundombinu ya barabara, maji na umeme zimeanza. Natoa wito wananchi washirikiane na Serikali katika kuziunga mkono jitihada hizi.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Serikali imeweka mkazo maalum wa kuiendeleza sekta ya utalii ikiwa ni sekta kiongozi katika kukuza uchumi wetu. Katika kutekeleza Mpango wa Utalii kwa Wote, idadi ya watalii wanaokuja kutembelea Zanzibar imeongezeka kutoka watalii 132,836 mwaka 2010 na kufikia watalii 274,619 mwaka 2014.  Hili ni ongezeko la asilimia 107.Hivi sasa, inaandaliwa Sera ya Urithi wa Utamaduni itakayotoa muongozo wa matumizi bora ya maeneo ya urithi ili kuimarisha shughuli za utalii.  Aidha, maeneo ya historia, mambo ya kale na urithi wa utamaduni yaliyopo Mangapwani, Kuumbi Jambiani na Kwa Bi. Khole kwa upande wa Unguja na Chwaka - Tumbe kwa Pemba yanaendelea kuimarishwa.  Wito wangu kwa wananchi wote wazitumie fursa hizo kujifunza masuala mbali mbali yanayohusu utamaduni na urithi wetu wa kimaumbile.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kuhusu sekta ya elimu, Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuiimarisha na kuiiendeleza elimu. Katika kipindi hiki cha miaka minne, tumepata mafanikio makubwa kuanzia kwenye skuli za maandalizi, msingi, sekondari hadi elimu ya juu.  Tumeweza kupunguza tatizo la upungufu wa walimu, maabara, vitabu vya kusomea na uhaba wa madarasa na samani.Aidha,  tumeweza kuajiri walimu 1,781 wa ngazi mbali mbali. Idadi hii ni sawa na asilimia 74 ya mahitaji.  Hata hivyo, bado walimu 627 wanahitajika, sawa na asilimia 26.  Aidha, idadi ya skuli za maandalizi imeongezeka kutoka skuli 238 mwaka 2010 hadi 279 mwaka 2014,  ongezeko hili ni sawa na asilimia 17.  Skuli za msingi zimeongezeka kutoka 299 mwaka 2010 hadi skuli 359 mwaka 2014.  Ongezeko hili ni sawa na asilimia 20.  Ingawa skuli za msingi zimeongezeka katika mwaka 2014, lakini bado kuna upungufu wa skuli hizo.  Kwa hivyo, Serikali ina mpango wa kujenga skuli za msingi 10, katika Wilaya zenye upungufu wa skuli za msingi. Jumla ya US$ milioni kumi zimepatikana kutoka Shirika la Mafuta Duniani (OPEC) kwa ajili ya ujenzi wa skuli hizo.
 
Kuhusu skuli za sekondari kuanzia Kidatu cha Kwanza hadi cha Sita nazo zimeongezeka kutoka 194 mwaka 2010 hadi skuli 210 mwaka 2014.  Ongezeko hili ni sawa na asilimia 8.Kwa lengo la kukabiliana na tatizo la uhaba wa madarasa Serikali imekamilisha ujenzi wa madarasa 513 kati ya madarasa 600 kwa mujibu wa lengo la mpango mkuu wa elimu, ifikapo mwaka 2016.  Idadi hii ni sawa na asilimia 85.5 ya malengo.  Serikali itafanya kila jitihada ili tuweze kulifikia lengo hili.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Katika kipindi chote cha miaka minne, Serikali imefanikiwa kuwaandikisha wanafunzi wote waliotarajiwa kuanza darasa la kwanza.  Jumla ya watoto 35,535 wameanza darasa la kwanza mwaka 2014, ikiwa ni sawa na asilimia 100 ya uandikishaji. Idadi hii ni sawa na ongezeko la asilimia nane ikilinganishwa na wanafunzi 32,983 walioandikishwa mwaka 2010.  Jitihada hizo zinakwenda sambamba na utekelezaji wa MKUZA II na Malengo ya Milenia.Kuhusu mafunzo ya elimu ya amali, idadi ya vijana wanaojiunga na vituo vya mafunzo hayo yanayotolewa katika kituo kilichopo Mkokotoni Unguja na Vitongoji Pemba, imeongezeka kutoka wanafunzi 449 mwaka 2010 hadi kufikia wanafunzi 580 mwaka 2014.  Ongezeko hili ni sawa na asilimia 29.  Hivi sasa Serikali inatayarisha ujenzi wa skuli nyengine ya mafunzo ya amali huko Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja na Mtambwe katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Vile vile, Serikali imechukua hatua ya kuimarisha fursa za elimu ya juu.  Idadi ya wanafunzi katika vyuo vikuu vitatu vya Zanzibar imeongezeka kutoka 3,624 mwaka 2010 hadi 6,038 mwaka 2014.  Ongezeko hili ni sawa na asilimia 67.  Sambamba na ongezeko la wanafunzi, idadi ya masomo katika viwango vya shahada mbali mbali katika vyuo vikuu vyote vitatu imeongezeka.  Aidha, masomo ya udaktari (Doctor of Medicine), yaliyoanzishwa mwaka 2013 yanaendelea vizuri na wanafunzi 99 wanaendelea na masomo yao ya mwaka wa kwanza na wa pili.  Kadhalika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kutoa mikopo na hadi kufikia Disemba, 2014 imetoa mkopo kwa wanafunzi 4,678 yenye jumla ya TZS bilioni 19.4.kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Huduma katika Hospitali ya Mnazi mmoja zimeimarishwa, ili ifikie lengo la kuwa Hospitali ya Rufaa. Vifaa vya kisasa vipya vimewekwa kwenye chumba cha upasuaji, maabara ya uchunguzi wa maradhi, wodi mpya ya wagonjwa mahututi, wodi ya wazazi na chumba cha wagonjwa wa dharura.  Kadhalika, kituo cha meno cha tabasam, (smiling centre) kinachowahudumia watu wenye matatizo ya midomo kimeanzishwa.Jengo jipya la utoaji wa huduma za upasuaji wa kichwa na uti wa mgongo, limezinduliwa rasmi tarehe 9 Januari mwaka huu.  Huduma zinazotolewa kwenye kitengo hiki, ambacho kimeanzishwa kwa msaada wa NED ya Hispania ni cha kwanza kuwepo katika eneo la Afrika ya Mashariki na Kati. Mradi wa huduma za mama na watoto, ujenzi wa jengo jipya la watoto na huduma za wagonjwa wa maradhi ya figo, imeanza kutekelezwa.  Vile vile, kitengo cha uchunguzi wa maradhi ya mfumo wa chakula kimeanzishwa na wodi mpya ya wagonjwa mahututi imefunguliwa rasmi tarehe 10 Januari, 2015.
 
Huduma kwenye hospitali ya Wete zimeimarishwa ambapo wodi mpya ya wazazi, wodi ya wagonjwa wa akili na chumba cha upasuaji vimejengwa.  Vile vile, huduma katika hospitali ya Chake Chake zimeimarishwa baada ya kuzipanua huduma za uchunguzi wa maradhi kwa kuifanyia matengenezo makubwa maabara yake na kuwa maabara ya kisasa, mashine mpya ya x-ray kufungwa, wagonjwa kupatiwa huduma za damu salama na kitengo cha mazoezi ya viungo kufanyiwa matengenezo.Katika kuziimarisha huduma za afya katika hospitali ya Abdalla Mzee, ili ifikie daraja la hospitali ya Mkoa, hospitali ya Abdalla Mzee ya Mkoani imeanza kujengwa upya kwa msaada wa Jamhuri ya Watu wa China. Hospitali hii inatarajiwa kumalizika katika kipindi cha miaka miwili ijayo.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, idadi ya madaktari na wataalamu mbali mbali wa afya imeongezeka kutoka 3,634 mwaka 2010 hadi kufikia 4,618 mwaka 2014.  Ongezeko hili ni sawa na asilimia 26.Idadi ya madaktari wazalendo walioajiriwa sasa imefikia 102. Idadi hii imefikiwa baada ya kuajiriwa madaktari wazalendo 37 katika mwezi wa Novemba, 2014.  Hivi sasa Zanzibar wapo madaktari 40 wa kigeni. Kwa hivyo, idadi ya madaktari wote wanaotoa huduma Zanzibar, sasa imefikia 142.  Kwa idadi hii ya madaktari na idadi ya watu wa Zanzibar, kwa mujibu wa sensa ya 2012, daktari mmoja anatoa huduma kwa watu 9,708 hivi sasa.  Kiwango hiki cha madaktari kimesaidia sana katika kutoa huduma za afya kwa Unguja na Pemba.  Hata hivyo, jitihada za kuwasomesha madaktari na watalaamu wengine wa afya zinaendelezwa.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Elimu ya Afya kwa umma inaendelea kutolewa kwa njia mbali mbali ikiwemo Radio, TV, kupitia ZBC na vipeperushi. Mkazo zaidi umewekwa kuwaelimisha wananchi kuhusu maradhi ya kuambukiza na yasio ya kuambukiza. Serikali ilifanya jitihada maalum juu ya kinga na tahadhari kuhusu maradhi ya Ebola.  Mafanikio ya kutia moyo yamepatikana kwenye huduma za mama na mtoto pamoja na chanjo zinazotolewa dhidi ya maradhi mbali mbali na kwenye kampeni ya kitaifa ya chanjo, ambapo asilimia 96.75 ya watoto walichanjwa Unguja na Pemba. 
 
Kwa lengo la kupunguza vifo vya mama wajawazito, Serikali inahimiza utekelezaji wa uamuzi wake uliotolewa mwezi wa Mei, 2012 kwamba kinamama wajawazito wakajifungue kwenye vituo vya afya na hospitali za Serikali bila ya malipo yo yote.  Kwa hivyo, nawataka wafanyakazi wa vituo vya afya na wodi za wazazi za Serikali, wasiwatoze wazazi fedha zozote wanapokwenda kujifungua kwa njia ya kawaida au ya upasuaji.  Huduma hizi zinapaswa zitolewe bure.Kuhusu UKIMWI, kiwango cha maambukizo kinaendelea kubakia kuwa asilimia 0.6 na idadi ya wagonjwa wanaopata huduma ya ARVs imeongezeka kutoka wagonjwa 2,341 mwaka 2010 hadi 4,669 mwaka 2014.  Ongezeko la idadi hii ni sawa na asilimia 99.  Jitihada zetu za kupambana na UKIMWI zimepata mafanikio ya kuridhisha na wanaoishi na virusi vya UKIMWI ambao wanatumia ARVs afya zao zimeimarika.
 
Naendelea kuwanasihi wananchi waendelee kupima afya zao, kwani tatizo la UKIMWI bado lipo.
 
Serikali inaendelea kuwahamasisha wananchi kuchangia damu ili kuimarisha upatikanaji wa damu salama kwa mahitaji ya wagonjwa wetu kupitia kitengo cha damu salama. Katika mwaka 2010/2011, kitengo hiki kililenga kukusanya “units”  6,000 za damu na kufanikiwa kukusanya “units” 7,965. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 33. Katika mwaka 2013/2014, mahitaji yaliongezeka na kufikia units 10,000 kwa mwaka ambapo makusanyo yalifikia asilimia 95 ya lengo. Kutokana na mafanikio haya yaliyopatikana, nawapongeza wale wote wanaochangia damu kwa imani yao ya kuwasaidia wagonjwa wote. Ili kuhakikisha upatikanaji wa damu salama ya kutosha, natoa wito kwa wananchi wote wajitokeze kuchangia damu ambayo inahitajika katika hospitali zetu za Unguja na Pemba katika wodi ya wazazi, watoto upasuaji na wodi za dharura.
 
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Kuhusu malaria, baada ya kasi ya malaria kupungua, baada ya jitihada zilizochukuliwa na Serikali, mikakati mbali mbali ya ziada ya kupambana na malaria imeongezwa.  Hivi sasa, bado kiwango cha malaria kipo chini ya asilimia 1. Katika mwaka 2013, shehia 71 hazikuwa na mgonjwa hata mmoja wa malaria, lakini wagonjwa wachache wamebainika katika Wilaya ya Magharibi, Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja na Wilaya ya Micheweni kwa Pemba. 
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa Awamu zote za uongozi ndani ya kipindi cha miaka 51, imetekeleza mipango mbali mbali ya kuwapatia wananchi huduma ya maji safi na salama kwa kuamini kuwa maji ni uhai.  Vile vile,  suala hili limepewa kipaumbele katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010 - 2015, ambapo Serikali imetakiwa kusambaza huduma ya maji safi na salama kutoka asilimia 75 hadi asilimia 95 kwa mijini na kutoka asilimia 60 hadi asilimia 80 kwa vijijini ifikapo mwaka 2015. Ili kufikia lengo hilo, Serikali kwa kushirikiana na Washirika mbali mbali wa Maendeleo imetekeleza miradi kumi, program mbili na mpango wa kulinda vyanzo vya maji. 
 
Katika kipindi cha miaka minne, jumla ya visima 106 vimechimbwa, matangi 31 yenye viwango tofauti yamejengwa na mabomba yenye urefu wa km. 371.65 yamelazwa katika maeneo mbali mbali ya Mikoa yote ya Unguja na Pemba.  Katika jitihada hizi, uzalishaji maji wa jumla ya lita milioni 17.6 umefikiwa na idadi ya watu 175,873 wameongezeka katika kupatiwa huduma za maji katika kipindi hiki.  Hadi kufikia Disemba, 2014, mahitaji halisi ya maji kwa Unguja na Pemba, ni lita milioni 214.6 na uzalishaji uliofanyika katika kipindi hiki ni lita milioni 163.  Kiwango hiki ni sawa na asilimia 76 ya mahitaji na kiwango cha upungufu ni asilimia 24.
 
Katika takwimu hizi Mkoa wa Mjini Magharibi, kiwango cha upatikanaji wa maji kimefikia asilimia 87.7 ya mahitaji halisi, Mkoa wa Kaskazini Unguja asilimia 71.68, Mkoa wa Kusini Unguja asilimia 76.45, Mkoa wa Kaskazini Pemba asilimia 56.42 na Mkoa wa Kusini Pemba asilimia 74.08.Juhudi hizi, ni kielelezo cha jinsi Serikali inavyozingatia umuhimu wa kuwapatia wananchi huduma ya maji safi na salama kulingana na MKUZA II na Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya mwaka 2010-2015.  Natoa wito kwenu wananchi muendelee kuwa na subira na mshirikiane na Serikali katika kuvitunza vianzo vyote vya maji.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Katika kipindi hiki cha miaka minne, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, ilikamilisha kazi za ujenzi wa barabara 11 zenye urefu wa km 102 za mikoa miwili ya Pemba na barabara nne zenye urefu wa km. 34.85 za mikoa mitatu ya Unguja zilizoanzwa kujengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Sita.  Barabara zote hizo zilizinduliwa katika sherehe za Mapinduzi za mwaka 2014 na 2015. Kukamilika kwa barabara hizi kumerahisisha usafiri wa abiria, usafirishaji wa mazao ya wakulima, shughuli za kijamii, kukuza uchumi na kuimarisha mtandao wa barabara zetu.Ujenzi wa barabara mpya ya Jendele-Cheju hadi Kaebona yenye urefu wa km 11.7 na barabara ya Koani hadi Jumbi yenye urefu wa km 6.3 umeanza na kazi inaendelea vizuri.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Ujenzi wa barabara ya Wete hadi Gando (km 15) na barabara ya Wete hadi Konde (km 15) umefikia hatua ya utiaji lami na kukabidhiwa katika kipindi kifupi kijacho.  Aidha, maandalizi ya ujenzi wa barabara kutoka Ole hadi Kengeja yenye urefu wa km 35 yameanza. Ujenzi wa barabara ya Chake Chake hadi Wete yenye urefu wa km 22.1 utaanza baada ya kukamilika kwa barabara ya Wete hadi Gando na Wete hadi Konde.  Ujenzi wa barabara hizo unafadhiliwa kwa pamoja kati ya Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kiarabu (BADEA) na Serikali ya Saudi Arabia (SAUDI FUND) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Natoa shukurani kwa Shirika la MCC la Marekani, Benki ya BADEA na Serikali ya Saud Arabia kwa kushirikiana nasi katika ujenzi wa barabara saba za Mkoa wa Kaskazini Pemba na kwa Serikali ya Norway kwa msaada wao katika ujenzi wa barabara za Mkoa wa Kusini Pemba.Natoa wito wangu kwa wananchi wazitunze barabara hizi ili zidumu kwa muda mrefu kwa madhumuni ya kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi yetu. 
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika uimarishaji wa miundombinu ya bandari, Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Azam Marine imejenga majengo mapya ya kupumzikia abiria katika Bandari ya Malindi. Aidha, Serikali imenunua mashine na vifaa mbali mbali kwa ajili ya kuimarisha shughuli za kazi bandarini. Jitihada zinafanywa ili kuziongeza mashine na vifaa vyengine.  Katika jitihada za kuziimarisha huduma za bandari kutokana na shughuli nyingi ziliopo katika bandari ya Malindi, na uchache wa nafasi, Serikali imeamua kujenga bandari mpya huko Mpigaduri.  Upembuzi yakinifu umekamilika na jitihada za kuanza ujenzi zinafanywa. 
 
Kadhalika, Mamlaka ya Usafiri Baharini imeimarisha ukaguzi wa vyombo vya baharini kwa kushirikiana na SUMATRA, hatua ambayo imepelekea kupungua kwa ajali za vyombo vya baharini kwa kiasi kikubwa. Katika kuimarisha usafiri wa abiria baharini, Serikali iliamua kununua meli mpya kwa ajili ya kupunguza tatizo la usafiri wa abiria na mizigo yao.  Meli hiyo yenye uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na mizigo tani 200 inatarajiwa kufika nchini mwezi wa Juni, 2015.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa usafiri wa anga, ujenzi wa maegesho ya ndege na njia ya kupitia ndege unaojengwa kwa ajili ya kukiimarisha kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume umekamilika na tarehe 3 Januari, 2015 umezinduliwa. Ujenzi wa jengo jipya la abiria bado unaendelea na unatarajiwa kumalizika mwezi Oktoba 2015. Kazi ya kuweka taa katika Kiwanja cha Ndege cha Pemba inatarajiwa kuanza hivi karibuni na kumalizika mnamo mwezi wa Juni mwaka huu.  Kumalizika kwa kazi hizo, kutaimarisha usafiri wa ndege na kuimarisha utalii na biashara.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imesimamia na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi.  Serikali imetayarisha sera mpya ya ardhi ambayo imezingatia mabadiliko na maendeleo ya kijamii na kiuchumi tuliyofikia hivi sasa pamoja na mwelekeo wetu wa miaka ijayo.  
Vile vile, kazi ya usajili na utambuzi wa ardhi inaendelea.  Hadi hivi sasa, shehia 20 za Unguja na Pemba zishasajiliwa na 13 nyengine zinaendelea na zoezi la utambuzi.  Zoezi la utoaji wa Hati za Matumizi ya Ardhi mpya pamoja na kuzibadilisha hati za zamani, linaendelea. Napenda niwahimize wananchi, wauitikie wito wa usajili wa ardhi, ili zoezi hili liweze kufanyika kwa haraka kama ilivyopangwa kwenye MKUZA II la kusajili asilimia 50 ya ardhi mwaka huu wa 2015.
 
Katika kipindi hiki cha miaka minne, katika sekta ya ardhi jumla ya mikataba 223 imesainiwa na kukabidhiwa wawekezaji sambamba na utoaji wa hati 1,310 za matumizi mbali mbali ya ardhi.  Vile vile, jumla ya viwanja 1,691 vimepimwa Unguja na Pemba kwa matumizi mbali mbali ikiwemo nyumba za makaazi za wananchi. 
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Hivi sasa wakati tunasherehekea miaka 51 ya Mapinduzi ya 12 Januari, 1964, mafanikio makubwa yamepatikana ya kuwa na umeme wa MW 100 kwa Unguja na MW 20 kwa Kisiwa cha Pemba.Kazi kubwa imefanyika katika kuusambaza umeme huu kwa Unguja na Pemba, kwa mijini na vijijini.  Hivi sasa huduma za umeme zinapatikana katika miji yote na huduma hizi zimefikishwa katika vijiji 129 badala ya 123 vilivyokisiwa awali.  Hili ni ongezeko la asilimia 4.9. Ahadi ya Serikali ya kupeleka umeme kwenye visiwa vidogo vidogo imeanza kutekelezwa.  Tayari kazi ya kupeleka umeme Kisiwa Panza,  Makoongwe na Shamiani huko Pemba, imeanza na inatarajiwa kukamilika mwaka huu, 2015. Nawanasihi wananchi wa Kisiwa Panza, Makoongwe na Shamiani, waendelee kuwa na subira huku Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) likifanya bidii kubwa ya kuikamilisha kazi hiyo.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Serikali inafanya jitihada mbali mbali katika kuendeleza Mapinduzi ya Kilimo ili kuongeza uzalishaji, kuwa na uhakika wa chakula na lishe. Kwa lengo la kuwasaidia wakulima hasa wa mpunga, Serikali inaendeleza programu iliyoanzishwa mwaka 2011 ya kuwapa ruzuku wakulima ya asilimia 75 ya gharama za bei ya mbolea, mbegu, dawa ya kuulia magugu na huduma za matrekta. Katika kipindi hiki, zana, vifaa na nyenzo mbali mbali zilinunuliwa.  Jumla ya wakulima 61,500 wa kilimo cha kutegemea mvua na kilimo cha umwagiliaji maji walifaidika.
 
Vile vile, mavuno ya zao la mpunga kwa jumla, yaliongezeka kutoka tani 21,014 mwaka 2010 hadi tani 33,655 mwaka 2013.  Ongezeko hili ni sawa na asilimia 60.  Juhudi za Serikali za kutoa ruzuku zimesaidia sana kupatikana mafanikio haya na juhudi hizi zitaendelezwa katika miaka ijayo. 
Kadhalika, jitihada za kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji maji wa hekta 2,200 katika mabonde ya Cheju, Kibokwa na Kilombero kwa Unguja na Mlemele na Makwararani kwa Pemba zinaendelea.  Kazi iliopo hivi sasa ni kuanza ujenzi wa miundombinu hio baada ya kazi ya usanifu (design) kukamilika.  Fedha za miradi hii tayari zimepatikana kutoka Exim Bank ya Jamhuri ya Korea na Benki ya Dunia.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Katika kuendeleza utafiti, kwa lengo la kuimarisha kilimo Serikali imeanzisha Taasisi ya Utafiti ya Kizimbani na inashirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (COSTECH) katika kuendeleza utafiti. Jumla ya mbegu 43 zimefanyiwa utafiti kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa zao la mpunga wa kimataifa (IRRI). Kwa upande wa utafiti wa mbegu za mazao ya mizizi, Taasisi ya Utafiti imeweza kutoa mbegu zinazostahamili maradhi na kunawiri katika mazingira ya Zanzibar.
 
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, mwaka 2014 ulikuwa ni mwaka wa mafanikio kwa watu wa Zanzibar ambapo uzalishaji wa mazao muhimu ya chakula ulifikia tani 674,334.  Kiwango hiki ni ongezeko la asilimia 95 la tani 346,535 zilizovunwa mwaka 2013.Aidha, katika kipindi cha miaka minne, jitihada za kuotesha na kupanda miti zilichukuliwa ambapo jumla ya miti milioni 5 ya misitu ilioteshwa katika vitalu vya Serikali na miche milioni 8 katika vitalu vya watu binafsi. 
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Kuhusu sekta ya mifugo, Serikali imefanya juhudi kubwa ya kuwaendeleza wafugaji kupitia programu ya Uimarishaji wa Huduma za Mifugo (ASDP-L) yenye kutoa taaluma ya ufugaji bora.  Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, wafugaji 54,567 wametembelewa na kupewa ushauri wa kitaalamu.Vituo vya kutolea huduma za utibabu na uzalishaji wa mifugo pamoja na huduma za utafiti na utibabu wa wanyama ziliimarishwa. Vile vile, matengenezo makubwa ya maabara ya Maruhubi, Unguja na ya Chake Chake, Pemba yamefanywa.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Katika kipindi hiki cha miaka minne sekta ya uvuvi imeimarika ambapo mchango wa sekta hii katika Pato la Taifa umefikia asilimia 7.2.  Tani 148,535 za samaki walivuliwa wenye thamani ya TZS bilioni 527.5.  Jumla ya wavuvi 2,320, walifundishwa taaluma na mbinu bora za uvuvi na ufugaji wa samaki unaozingatia hifadhi ya mazingira.  Vikundi 100 vya ufugaji samaki vimeundwa na mabwawa sita ya kufugia samaki yameanzishwa Unguja na Pemba. 
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Ukulima wa zao la mwani umeimarishwa, ambapo wananchi wengi, hasa wanawake, wanajishughulisha na uzalishaji wa zao hili hivi sasa. Kiasi cha tani 51,687 za mwani mkavu zenye thamani ya TZS bilioni 18.7 zilisafirishwa kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.Nawasisitiza sana wananchi waendelee kupinga vitendo vya uvuvi haramu ili kazi ya uvuvi iwe endelevu na yenye tija.  Aidha, Serikali itaendelea kuwahamasisha wawekezaji wawekeze kwenye uvuvi wa bahari kuu ili kuongeza mchango wa sekta hii katika uchumi na kutoa fursa za ajira kwa vijana.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Zanzibar kama ilivyo nchi nyingi duniani, inakabiliwa na changamoto za kimazingira ikiwa ni pamoja na uharibifu wa misitu, utupaji mbaya wa taka na umwagaji wa maji machafu, uchimbaji wa mawe, mchanga na kifusi.Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali inaitumia Sera mpya ya Mazingira ya mwaka 2013 kwa ajili ya kuzishughulikia changamoto za kimazingira pamoja na kutayarisha mpango wa usimamizi wa mazingira.  Kadhalika, Serikali imeandaa na kuzindua Mkakati wa Zanzibar wa Mabadiliko ya Tabianchi ambao una shabaha ya kuihami Zanzibar dhidi ya athari hizo. Vile vile, sheria mpya ya mazingira yenye lengo la kulinda na kusimamia mazingira imeandaliwa na inatarajiwa kupelekwa katika Baraza la Wawakilishi kwenye vikao vijavyo.
 
Hadi kufikia mwezi wa Septemba, 2014, jumla ya tani 4.0 za mifuko ya plastiki zimekamatwa mafanikio haya yamepatikana kutokana na utekelezaji na usimamizi wa kanuni za mwaka 2011.  Natoa wito kwa kila mmoja wetu ashiriki katika kuyalinda na kuyahifadhi mazingira yetu, ambayo ni muhimu katika maendeleo yetu.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali imeendelea kufanya jitihada mbali mbali za kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutekeleza mipango yenye lengo la kuinua kipato cha wananchi na kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa kinamama na vijana.Tarehe 21 Disemba, 2013, Serikali ilizindua Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili kukabiliana na tatizo la ajira na kuinua uchumi wa wananchi. 
 
Mfuko huu hivi sasa una jumla ya TZS bilioni 2.313.Hadi tarehe 31 Disemba, jumla ya mikopo 706 imeidhinishwa kwa Unguja na Pemba na jumla ya TZS milioni 795.55 zimekopeshwa kwa wananchi.  Katika mikopo iliyotolewa, ajira za moja kwa moja 1,384 na ajira zisizo za moja kwa moja 4,000 zimepatikana.  Jumla ya TZS milioni 146.95 tayari zimerejeshwa kuanzia Julai hadi Novemba, 2014.  Mfuko huu umetoa mikopo katika sekta muhimu za kiuchumi.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza vyema wajibu wake wa kuielimisha jamii na kuipa habari za ndani na nje ya nchi. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) limesimamia mfumo wa utangazaji, kutoka “Analogue” kwenda “Digital”  kwa mafanikio makubwa.  Matangazo ya Radio na TV yanaendelea kwa saa 24 tangu yalipoanzishwa pamoja na chaneli ya pili ya ZBC (ZBC2) imeanzishwa ili kuimarisha huduma zake. Vifaa vipya kwa ajili ya studio ya Karume House na studio ya Pemba vimenunuliwa na wafanyakazi wa ZBC wamepewa mafunzo kwa ajili ya kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
 
Aidha, Serikali imetekeleza ahadi yake ya kuwajengea wasanii Studio ya kisasa ya kurekodia nyimbo na michezo ya kuigiza kwenye jengo la zamani la Utangazaji la Sauti ya Tanzania Zanzibar, baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa. Vifaa vipya kwa ajili ya Studio vinatarajiwa kununuliwa hivi karibuni.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Utamaduni ni kielelezo cha utambulisho wa jamii. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali imeendelea kusimamia na kuuendeleza utamaduni wetu, silka na desturi zetu.  Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Zanzibar imeendelea kuandaa matamasha mbali mbali ambayo yamesaidia sana kuendeleza na kuhifadhi utamaduni wa mambo ya asili, kuchangia uchumi wetu na kutoa ajira kwa vijana. Nawanasihi wananchi wote tuendeleze utamaduni wetu na mila zetu kwa manufaa yetu na kizazi kijacho.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali imetekeleza mambo mbali mbali katika kuimarisha sekta ya michezo.  Miongoni mwa mambo hayo ni kuandaliwa kwa sera mpya ya michezo ya Zanzibar itakayoimarisha na kuiendeleza michezo yote.  Serikali imeanzisha mashindano ya riadha ya Wilaya, kwa Wilaya zote kumi za Zanzibar na ilitoa vifaa vya michezo kwa wanariadha 250 ili kurejesha vugu vugu la michezo ya riadha. Utaratibu wa kutoa vifaa kwa wanamichezo utaendelezwa. Vile vile, Serikali imewahamasisha wananchi waendeleze michezo ili wajenge afya zao kwa kufanya mazoezi ya viungo kila siku na washiriki kwenye tamasha la mazoezi ya viungo linalofanyika litakalofanyika tarehe 1 Januari ya kila mwaka.
 
Kadhalika, katika kuhakikisha watoto wetu wanapata maeneo ya kucheza na kufurahi, Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii imekijenga upya Kiwanja cha Kufurahishia Watoto cha Uhuru kiliopo Kariakoo kwa TZS bilioni 15. Kiwanja hicho kimefunguliwa tarehe 8 Januari, 2015 katika shamrashamra za miaka 51 ya Mapinduzi na kina aina nyingi ya michezo ambayo watoto wataifurahia sana.  Ujenzi wa Kiwanja cha Kufurahishia Watoto cha Tibirinzi Pemba, utakamilika hivi karibuni.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Kwa lengo la kutekeleza azma ya Serikali ya kukifufua Kiwanda cha Upigaji Chapa na Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali ili kurudisha hadhi yake na kuinua kiwango cha uzalishaji, jumla ya TZS milioni 5,532.40 zimetumika kwa matengenezo ya majengo yaliyokuwa kiwanda cha sigara Maruhubi pamoja na ununuzi wa mashine mpya za kisasa za uchapishaji za kiwanda hicho.

Hivi sasa kiwanda hiki kina uwezo wa kuchapisha vitabu na nyaraka za aina mbali mbali. Serikali ina lengo la kukiimarisha zaidi ili kiweze kuchapisha magazeti, vitabu vikubwa na kadhalika. Ni dhahiri kukamilika kwa kiwanda hiki kumeipunguzia mzigo Serikali na kitaiwezesha kutoa huduma zenye ubora wa kiwango kikubwa zaidi.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Miongoni mwa malengo ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 ni kuwahudhumia na kuwatunza wazee. Katika kutekeleza azma hii Serikali imeendelea kuwatunza na kuwahudumia ambapo huduma zote muhimu zimeimarishwa na zinapatikana kwa ajili ya maisha yao ya kila siku.
 
Kadhalika, Serikali imefanya jitihada mbali mbali ili kuwasaidia watu wenye ulemavu.  Mfuko Maalum wa Watu Wenye Ulemavu umeanzishwa na uliozinduliwa mwaka 2012.  Mfuko huu una jumla ya TZS milioni 167.6 ambazo zitatumika kwa mahitaji mbali mbali ya watu wenye ulemavu. Vile vile usajili wa watu wenye ulemavu uliofanywa kwenye Wilaya zote za Unguja na Pemba sasa umekamilika, na umesaidia sana kuwatambua ili kurahisisha upangaji na utekelezaji wa mipango yao ya maendeleo.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Vitendo vya unyanyasaji wa wanawake na watoto bado vinaendelea kuwepo. Tarehe 6 Disemba 2014, Serikali ilizindua rasmi Kampeni ya kupinga vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto. Mpango wa miaka miwili tayari umeandaliwa na utatekelezwa na taasisi zote za Serikali na za kiraia kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo. Sote tuseme kwa kauli moja na tuoneshe kwa vitendo, kwamba udhalilishaji wa wanawake na watoto sasa basi. Hii ni imani yangu na bila ya shaka hii itakuwa ni imani ya wananchi wote wa Zanzibar.  Tunapaswa tuchukue hatua sasa, kwa pamoja tutafanikiwa.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Serikali inaendeleza jitihada za kuhakikisha kwamba watumishi wa umma wanatekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kuwatumikia wananchi bila ya ubaguzi wowote. Katika kipindi hiki, viwango vya utendaji kazi vimeongezeka na haya yamedhihirika kutokana na mafanikio yaliyopatikana.  Ingawa bado zipo changamoto zinazotukabili, lakini jitihada zinaendelea kuchukuliwa ili kuziondoa changamoto hizo hatua kwa hatua.
 
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, jumla ya wananchi 19,758 walipatiwa ajira.  Watumishi walioajiriwa Serikalini na kwenye mashirika ya umma ni 5,667. Wananchi 7,256 walipatiwa ajira katika sekta binafsi na wananchi 6,835 walipatiwa ajira katika vyama vya ushirika.  Vile vile, wapo wananchi waliojiajiri wenyewe baada ya kupata mikopo ambao ni 3,400 na wananchi 4,000 wamepata ajira zisizokuwa za moja kwa moja.
 
Kwa upande wa maslahi ya wafanyakazi, Serikali ililishughulikia suala hili kwa kuwaongezea mishahara na posho wafanyakazi wote wa Serikali katika mwaka wa fedha 2011/2012 na 2013/2014. Marekebisho hayo, yalizingatia mambo mbali mbali ya sheria ya Utumishi wa Umma na Kanuni zake.Serikali itahakikisha kuwa maslahi ya watumishi wa umma yanaimarishwa kutokana na utendaji wao wa kazi, ili yawe bora zaidi, kwa kuwaongezea mishahara na stahili nyengine kadri hali ya uchumi wetu inavyoimarika na kwa kuzingatia miundo ya utumishi mipya ambayo sasa iko tayari kutumika.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kwa lengo la kuziimarisha huduma za mawasiliano Serikalini, Serikali ilianzisha mradi wa “e-government” uliozinduliwa mwaka 2013. Hadi hivi sasa, jumla ya majengo 86 ya Serikali yameunganishwa katika mtandao wa Serikali (e-government) na tayari yameanza kupata huduma ya intaneti bila ya malipo.  Awamu ya kwanza ya mradi huu inaendelea vizuri na maandalizi ya awamu ya pili yamekamilika.Kupitia mradi wa “e-government”, maeneo yote ya visiwa vya Zanzibar yanaunganishwa na baadae Zanzibar itaunganishwa na Tanzania Bara kupitia mkonga wa Taifa na itaunganishwa na mkonga wa mawasiliano wa Kimataifa wa “EASSy” na “SEACOM”.
 
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Katika utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuimarisha Utawala Bora, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi imeanzishwa baada ya kutungwa Sheria Namba 1 ya mwaka 2012.  Taasisi hii imeanza kazi zake baada ya kupatiwa nyenzo, vifaa vya kazi na wafanyakazi na inaendelea vizuri.  Vile vile, sheria ya maadili ya viongozi tayari imeandaliwa na inatarajiwa kupelekwa kwenye Baraza la Wawakilishi kwenye kikao kijacho.Aidha, katika kipindi hiki, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amewasilisha Serikalini Ripoti ya Ukaguzi ya mwaka 2010/2011 hadi 2012/2013 na Serikali iliziwasilisha kwenye Baraza la Wawakilishi, kama Katiba ya Zanzibar ya 1984 inavyoelekeza na baadae Serikali ilizifanyia kazi.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Baraza la Wawakilishi la Zanzibar la Nane lililoanza kazi zake mwezi Novemba 2010, limetekeleza shughuli zake kwa ufanisi mkubwa. Hadi kufikia Disemba, 2014 jumla ya mikutano 17 imefanywa na Baraza hilo.  Aidha, jumla ya miswada 53 imepitishwa kuwa sheria na hoja binafsi tatu za wajumbe zilipokelewa na kufanyiwa kazi. Kadhalika, wajumbe na watumishi wa Baraza walipatiwa mafunzo ndani na nje ya nchi ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.
 
Katika kipindi hiki cha miaka minne, Serikali imechukua juhudi mbali mbali za kuziimarisha mahakama ili ziweze kutekeleza kazi zake kwa ufanisi.  Idadi ya majaji imeongezeka kutoka majaji wawili mwaka 2011 hadi sita mwaka 2014; wakiwemo wanawake wawili.  Kadhalika, idadi ya mahakimu katika ngazi mbali mbali imeongezeka kutoka 43 mwaka 2010 hadi 69 mwaka 2014.  Ongezeko hili ni sawa na asilimia 60. Jumla ya kesi 29,786 zilifunguliwa katika mahakama zote za Unguja na Pemba ambapo kesi 19,952 ziliweza kutolewa maamuzi, sawa na asilimia 51.7.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Katika hotuba yangu niliyoitoa katika Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 49 ya Mapinduzi, nilielezea uamuzi wa Serikali wa kuleta mageuzi kwenye mfumo wetu wa kiutawala kwa kuzipa uwezo zaidi Serikali za Mitaa.  Nilielezea kuwa Serikali iliandaa Sera ya Serikali za Mitaa pamoja na Mpango wa Utekelezaji.  Ili kuipa nguvu Sera hio na Mpango wake, Serikali imefanyia marekebisho Sheria Namba 3 na 4 ya mwaka 1995 na Sheria Namba 1 ya mwaka 1998 na tayari imeandaa sheria mpya ya Tawala za Mikoa na Sheria mpya ya Serikali za Mitaa za mwaka 2014.  Ninatarajia kwamba wananchi wataendelea kutuunga mkono katika mabadiliko haya tunayokusudia kuyatekeleza.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Katika kukabiliana na changamoto mbali mbali za kimazingira zinazoikabili Manispaa ya Zanzibar pamoja na miji ya Chake Chake, Wete na Mkoani, Serikali ilianzisha Mradi wa Huduma za Jamii (ZUSP) mwaka 2011.  Lengo kuu la mradi huu ni kuimarisha upatikanaji wa huduma za mji Unguja na miji ya Pemba na kuhifadhi eneo la urithi wa Mji Mkongwe.Katika kipindi hiki cha miaka minne, gari 19 zimenunuliwa,  vizimba vinaendelea kujengwa,  jengo la Manispaa linafanyiwa ukarabati,  taa za barabarani zimeanza kuwekwa na ujenzi unaendelea katika maeneo mbali mbali ya miradi.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Kama nilivyosema hapo awali, maelezo niliyoyatoa yalikuwa ni muhtasari tu wa mafanikio ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, tuliyoyapata wakati tunapoadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964.  Ni wajibu wetu tuyaendeleze mafanikio haya na tufanye kila jitihada, ili nchi yetu iweze kupata mafanikio zaidi.  Jukumu kubwa tulilonalo ni lazima tuhakikishe kwamba amani na utulivu inatunzwa, inaimarishwa na inaendelezwa wakati wote.  Bila ya shaka yoyote, hali hio tutaifikia tu, ikiwa tutaendeleza umoja, mshikamano wetu na mapenzi baina yetu. 
 
Sote tuna wajibu wa kuzitii sheria ikiwa ni hatua moja muhimu katika kuitekeleza mipango yetu ya maendeleo na kuzitatua changamoto mbali mbali zilizotukabili.  Ni wajibu wa viongozi wote wa Serikali, wanasiasa, viongozi wa dini na viongozi wengine katika jami, sote kwa pamoja tutekeleze wajibu wetu huo kwa kuhakikisha kuwa amani na utulivu inadumishwa, inaendelezwa na sheria za nchi zinafuatwa.  Mapinduzi yetu na Muungano wetu ndizo nguzo zetu kubwa za maendeleo yetu na ndivyo vilivyotufikisha hapa tulipo hivi leo na ndivyo vitakavyotufikisha kule dira zetu za maendeleo zinavyotuelekeza tufike hapo baadae.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Kwa kuzingatia umuhimu wa Muungano wetu, katika kipindi cha miaka minne hii, nchi yetu ilikabiliwa na mambo kadhaa muhimu ya kuuimarisha Muungano wetu.  Miongoni mwa mambo hayo ni kuanza kwa mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulioanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, na kupelekea kutungwa kwa Sheria ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba Namba 8 ya Mwaka 2011.Bunge Maalum la Katiba la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilikamilisha kazi yake muhimu ya kutunga Katiba Mpya na kuikabidhi Katiba inayopendekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na kwangu, tarehe 8 Oktoba, 2014 huko Dodoma.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Mwaka huu tumekabiliwa na kuipigia kura ya maoni Katiba inayopendekezwa, ifikapo tarehe 30 Aprili, 2015 kama ilivyotangazwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.  Vile vile, kama nyote mjuavyo, mwaka huu tunakabiliwa na Uchaguzi Mkuu wa nchi yetu ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano.Chaguzi hizi mbili tutakazozifanya ni kielelezo cha kukua kwa demokrasia nchini na ni wajibu wetu tuendelee kuzitii sheria zetu katika kusimamia maslahi ya nchi yetu na tufanye jitihada za pamoja za kulinda amani na utulivu nchini.  Serikali zetu mbili zitaendelea kutimiza wajibu wake wa kuilinda nchi yetu na zitahakikisha kuwa wakati wote zinakabiliana na vitendo vyo vyote vya uvunjaji wa amani na sheria.  Nchi yetu iko salama na Mwenyezi Mungu ataijaalia kuwa salama wakati wote.  Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama viko imara katika kuilinda nchi yetu na mipaka yake.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Katika hotuba zangu za Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi ya miaka 47 mwaka 2011 na miaka 48 mwaka 2012, nilielezea jinsi Serikali ya Mapinduzi ya Awamu ya Saba yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa ilivyoanza kazi zake na ilivyokuwa ikiendelea kuwatumikia wananchi.Leo baada ya kukamilisha miaka minne na kuuanza mwaka wa tano wa kuiongoza Serikali hii, napenda nielezee furaha kubwa niliyonayo kutokana na mafanikio tuliyoyapata.  Maelezo niliyoyatoa ya kila sekta na mengine ambayo sikuweza kuyaelezea kwa sababu ya muda, tunayatekeleza kwa ufanisi kwa kuzingatia mpango wetu wa Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2020, MKUZA II, Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010/2015 na Malengo ya Milenia.
 
Napenda niitumie nafasi hii niwashukuru na niwapongeze Makamu wa Rais wote wawili, ambao ndio Wasaidizi na Washauri wangu wakuu; Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais.  Ninakushukuruni sana kwa ushauri wenu mnaonipa na mnavyonisaidia.
 
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
 
Namalizia hotuba yangu kwa kutoa shukurani zangu tena kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, viongozi mbali mbali mliohudhuria,  wageni wetu wote na Mabalozi wa Nchi za Nje.  Vile vile, natoa shukurani zetu za dhati kwa Washirika wetu wa Maendeleo wa ndani na nje ya nchi wakiwemo nchi rafiki, jumuiya za kimataifa, Asasi za kiraia na sekta binafsi kwa michango yao muhimu katika maendeleo yetu.  Kwa hakika michango yenu ni kichocheo kikubwa cha utekelezaji wa mipango yetu ya maendeleo.
 
Kadhalika, natoa shukurani zangu kwa wananchi wote kwa mahudhurio makubwa katika Sherehe za Miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu zilizofana sana.  Shukurani zangu vile vile, nazitoa kwa kwa vikosi vyote vilivyoshiriki kuandaa gwaride la kuvutia, wanafunzi waliofanya halaiki ya kupendeza, waandishi wa habari walivyofanya kazi kubwa ya kuzitangaza sherehe hizi.  Vile vile, shukrani zangu nazito kwa vikundi vya utamaduni vilivyotuburudisha na wananchi wote walioshiriki kuzifanikisha sherehe zetu za kuadhimisha Miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964. 
 
Aidha, natoa pongezi kwa Kamati ya Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa inayoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi kwa kazi nzuri ya walioifanya ya kuandaa na hatimae kuzifanikisha sherehe za leo na zile zilizotangulia kwa mafanikio makubwa.  Hongereni Sana.
 
Ndugu wananchi
 
Leo nataka kutangaza rasmi kwamba kuanzia mwaka ujao wa fedha 2015-2016 unaoanza Julai mwaka huu uchangiaji katika elimu ya msingi utaondoshwa wazee na wazazi hawatatakiwa tena watoe mchango wowote. Fedha hizo sasa zitachangiwa na kutolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa hivyo elimu ya msingi itakuwa bila ya malipo. Uwamuzi huu una lengo la uwamuzi wa Serikali wa kutoa elimu bure kama ilivyotangazwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume mnamo tarehe 23 Septemba mwaka 1964. Kuhusu elimu ya Sekondari, Serikali itaendelea kugharamia mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne pamoja na mitihani ya Kidato cha Sita, wazee hamtatakiwa kugharamia hata senti moja. Mambo mengine yanayohusu gharama za elimu ya Sekondari tutayatangaza hapo baadae
 
Nakutakieni viongozi, wageni waalikwa na wananchi nyote kheri na baraka ya mwaka mpya wa 2015.  Namuomba Mwenyezi Mungu aturudishe sote nyumbani salama.
 
MAPINDUZI DAIMA
MUNGU IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA
 
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.