Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Amefungua Maonesho ya Mei Mosi Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja

Serikali ya Awamu ya Nane(8) inayoongozwa na Dkt Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025, sheria za kazi na miongozo ya Kazi imekuwa ikiendelea kuchukua hatua mbali mbali katika kuweka mazingira bora kwa wafanyakazi ikiwemo kuboresha maslahi ya wafanyakazi na usalama kazini.


Hayo yamesemwa na  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati wa  ufunguzi wa maonesho ya MEI MOSI mwaka 2025 yanayofanyika katika Kijiji cha Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema Serikali itahakikisha kuwa  wafanyakazi wote  wanapata haki zao kwa kujibu wa sheria za utumishi nchini na kuhakikisha wanakuwa na Mazingira bora ya kufanyia kazi zao ikiwemo kujenga majengo mapya na ofisi za kisasa, kupatiwa vifaa vya kisasa na mafunzo kazini ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wafanyakazi kutambua kuwepo kwa haki na wajibu katika utekelezaji wa majukumu yao na  kuwakumbusha kufanya kazi kwa kufuata sheria na miongozo ya kazi ili kupunguza malamiko kwa waajiri na waajiriwa.

Aidha, Mhe. Hemed amewasisitiza Viongozi wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) kuendelea kuwasimamia wafanyakazi kutimiza wajibu wao ili kuweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi ikiwa ndio lengo kuu la Serikali zilizopo madarakani.

Sambamba na hayo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali itaendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi ili kwa pamoja kuweza  kuijenga nchi na kuweka mazingira bora kwa wafanyakazi.

Hata hivyo Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amewakumbusha wananchi juu ya umuhimu wa kuitunza amani ambayo ndio kipaombele cha Taifa na kuwataka kutokubali kufarakanishwa na kupandikizwa chuki baina yao na Serikali kwa maslahi ya watu wachache wasio na malengo ya kujenga ustawi mwema wa Taifa la Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Mhe.Ali Suleiman Ameir amesema Wizara ya Kazi itaendelea kutekeleza Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo mbali mbali inayohusu stahiki za wafanyakazi jambo ambalo linasaidia kupunguza changamoto nyingi kwa wafanyakazi wa Serikali na wasekta binafsi.

Mhe. Ameir amesema Serikali imekuwa ikitoa fursa mbali mbali kwa wafanyakazi ikiwemo  kuwapatia mafunzo, ujuzi na nyenzo za kufanyia kazi ili kuweza  kufanya kazi zao kwa ufanisi na ustadi wa hali ya juu.

Amefahamisha kuwa kipaombele cha Serikali ya Awamu ya Nane (8) ni kuhakikisha wafanyakazi wanapatiwa kila aina ya stahiki zao na kuwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata miongozo yao ya kazi na kutoa huduma bora wa wananchi wanaofuata huduma katika maeneo yao ya kazi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) ndugu Seif Moh'd Seif amesema ZATUC imekuwa ikikaa pamoja na Wizara ya Kazi katika kuajadili mambo mbali mbali yanayohusu wafanyakazi ikowemo fursa, stahiki, changamoto na mambo ya kufanya katika kuhakikisha ustawi mzuri wa wafanyakazi nchini.

Aidha Mwenyekiti Seif amesema atahakikisha kuwa  wafanyakazi wa Taasisi za Serikali na Taasisi binafsi nchini wataendelea kufanya kazi kwa bidiii na ubunifu mkubwa ili kufikia malengo ya kuwa na Taifa lenye wafanyakazi weledi na wenye kutambua haki na wajio wawapo makazini.

Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Hufanyika kila ifikapo tarehe 01 Mei ya kila mwaka ambapo kwa mwaka 2025 yanatarajiwa kufanyika katika Kijiji cha Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja.








Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 29.04.2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.