Habari za Punde

Dk Shein: 'Pimeni afya zenu mara kwa mara'

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                     01 Januari, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa pamoja na wananchi kufanya mazoezi hawana budi kuzingatia suala la kupima afya zao mara kwa mara na kufuata miongozo ya kitaalamu hasa wanapofikia umri wa maika 40 na kuendelea.
 
Akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazoezi kitaifa katika uwanja wa Amani Unguja leo, Dk. Shein aliwataka wananchi kulipa uzito suala la kupima afya na kunukuu msemo usemao usipoziba ufa utajenga ukuta.
 
Alifafanua kuwa hospitali na vituo vya afya Unguja na Pemba vina uwezo wa kupima afya za wananchi na kuwapatia ushauri unaotakiwa kuhusu afya zao na kuwataka kuacha dhana kuwa zoezi hilo linaweza kufanyika katika hospitali kubwa pekee.
 
Aliwaeleza mamia ya wanachama wa vikundi vya mazoezi kuwa takwimu zilizoelezwa katika risala yao kuhusu ongezeko la maradhi yalisiyoambukizwa yanatisha na kwamba kimsingi mazoezi yanaweza kukabiliana na tishio la maradhi hayo.
 
Katika hotuba yake fupi kwa wanamazoezi hao, Dk. Shein alitoa wito kwa vikundi vya wanamichezo kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha uchangiaji damu na kueleza kuwa wanamichezo wako katika nafasi nzuri kuchangia damu kutokana na afya zao kuwa bora wakati wote.
 
Alitumnia fursa hiyo pia kuhimiza suala la kujenga uongozi madhubuti wenye kuzingatia umoja, kutii sheria, kanuni, nidhamu na uwajibikaji katika michezo kwa kuwa ndio msingi mkubwa wa mafanikio.
 
Dk. Shein aliupongeza uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo pamoja na vikundi vya mazoezi kwa kutekeleza agizo lake alilolitoa mwaka jana la kuifanya tarehe 01 Januari ya kila mwaka kuwa siku ya bonanza la mazoezi ya mwili.
 
Katika hafla hiyo, Dk. Shein alikabidhiwa cheti cha heshima kwa uamuzi wake wa kuitangaza siku ya tarehe 01 Januari ya kila mwaka kuwa siku ya Bonanza la Michezo ya mazoezi ya mwili.
 
Akizungunza awali kumkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk alieleza kuwa pamoja na kuongezeka vuguvugu la vikundi vya mazoezi katika kila wilaya Unguja na Pemba bado zipo changamoto za hapa na pale ikiwemo tatizo la baadhi ya watu kuwa na mtazamo tofauti kuhusu ufanyaji mazoezi hasa kwa wanawake.
 
Waziri Mbarouk alieleza pia kuwa suala la mafunzo kwa walimu wa mazoezi linafanyiwa kazi na serikali na  pamoja na suala msaada wa kidaktari kwa wanamichezo hao.
 
Waziri huyo aliongeza kuwa uwekaji wa zulia la kukimbilia (tartan) katika uwanja wa Gombani unatarajiwa kukamilika katika wiki mbili za mwanzo wa mwezi Machi na utafunguliwa kwa kufanyika mashindano makubwa ya riadha.
 
Katika risala yao iliyosomwa na Amina Kassim Abdalla, wanamazoezi hao walieleza kuwa kumekuwepo kwa ongezeko kubwa la wananchi kujiunga katika klabu za mazoezi kutoka klabu 10 mwaka 2010 chama hicho kilipoanzishwa hadi klabu 33 zilizoandikishwa hivi sasa.
 
Alifafanua kuwa wananchi wamekuwa wakiitikia wito wa kufanya mazoezi ambapo mwaka jana katika siku kama hiyo vikundi vya mazoezi 60 kutoka Unguja na Pemba na vingine 5 kutoka Tanzania Bara vilishiriki wakati mwaka huu vikundi 75 vimeshiriki kutoka Unguja na Pemba pamoja  na vikundi kutoka mikoa ya Dar Es Salaam na Dodoma.
 
Hata hivyo risala hiyo ilieleza kuwa pamoja na mwitikio huo kuna haja kuongeza kasi ya uhamasishaji ili wananchi wengi zaidi washiriki mazoezi kutokana na tafiti zilizofanywa mwaka 2010 hapa Zanzibar kuonesha kuwa kuna ongezeko kubwa la maradhi yasiyoambukizwa ambayo chanzo chake ni mabadiliko ya mtindo maisha.
 
“Utafiti uliofanywa mwaka 2010 kwa watu wenye umri wa kati ya miaka 25 na 64 hapa Zanzibar ulionesha kuwa kuna ongezeko la maradhi kama ya shinikizo la damu, kisukari na saratani” Ilieleza risala hiyo.
 
Alifafanua kuwa katika utafiti huo watu asilimia 3.7 waligundulika kuwa na maradhi ya kisukri wakati watu asilimia 30 walikutwa na maradhi ya shinikizo la damu.
 
Kwa hivyo walitoa wito kwa serikali kuangalia uwezekano wa kuingiza vipindi vya mazoezi katika skuli za Serikali na chama hicho kiko tayari kusaidia kufundisha mazoezi kwa wanafunzi kazi ambayo tayari inaofanya katika baadhi ya skuli za binafsi.
 
Katika maadhimisho hayo wanamichezo na vikundi mbali mbali vilipewa zawadi pamoja vyeti ambapo Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alikabidhi vyeti kwa klabu za mazoezi.
 
Naye Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad alitoa vyeti kwa waanzilishi wa Klabu za mazoezi na kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi alitoa vyeti kwa Benki ya Watu wa Zanzibar na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kwa kusaidia kufanikisha maadhimisho hayo.
 
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
                                               

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.