Habari za Punde

RAIS WA ZANZIBAR AKUTANA NA BALOZI WA RUSSIA ANAYEMALIZA MUDA WAKE

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                       20 Januari, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ushirikiano kati ya Zanzibar na Russia ni wa miaka mingi hivyo pande hizo mbili zina kila sababu za kuuendeleza na kuuimarisha kufikia kiwango cha juu zaidi.
Dk. Shein amesema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na Balozi wa Russia anayemaliza muda wake nchini Bwana Alexander Ranikh ambaye alifika Ikulu kumuaga.
“Zanzibar na Russia ni marafiki wa miaka mingi na wananchi wa Zanzibar hawatasahau kitendo cha nchi hiyo kuwa ya kwanza kuyatambua Mapinduzi ya matukufu ya mwaka 1964” Dk. Shein alisema.
Aliongeza kuwa watanzania wengi wakiwemo kutoka Zanzibar wamepata elimu yao nchini Russia na kuishi nchini humo kwa miaka mingi hivyo imekuwa sehemu ya historia ya maisha yao ambayo kamwe hawawezi kuisahau.
Dk. Shein alimueleza Balozi Ranikh kuwa kuendeleza uhusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Russia ni jambo la lazima kwa pande zote na amefurahi kuelezwa kuwa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe aliyoifanya nchini Russia hivi karibuni imekuwa ya mafanikio makubwa.
Dk. Shein alimueleza Balozi Ranikh kuwa Utalii ni moja ya maeneo ambayo Zanzibar na Russia zinaweza kushirikiana kwa kuzingatia kuwa Zanzibar na Tanzania kwa jumla zina vivutio vingi huku wananchi wa Russia wakiwa ni miongoni watu wanaofanya safari za kitalii sana duniani.

“Tuna fursa nzuri ya kuimarisha ushirikiano wetu katika sekta ya utalii.Wananchi wa Russia wanafanya safari nyingi za kitalii nchi za nje hivyo tungependa watembelee pia Zanzibar na Tanzania kwa jumla kujionea vivutio vyetu” Dk. Shein alieleza.
Kuhusu taarifa kuwa Chuo kikuu cha Kazakh huko Kazakhstan kuwa kimeanza mafunzo ya lugha ya Kiswahili, Dk. Shein alisema kuwa “hizo ni habari njema kwa kuwa hatua hiyo itazidi kuimarisha uhusiano wetu”
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Balozi huyo kwa kuitumikia vyema nchi yake wakati wote alipokuwa nchini na kuongeza kuwa amefurahishwa na jitihada zake za kutaka kufungua tena ubalozi mdogo wa nchi hiyo hapa Zanzibar na kumhakikishia kuwa jitihada hizo zinaungwa mkono kikamilifu na serikali.
Kwa upande wake Balozi Alexander Ranikh alieleza kuwa anaondoka nchini akiwa na matumaini kuwa ametimiza wajibu wake ipasavyo wa kuitumikia nchi yake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo akamueleza Dk. Shein kuwa pamoja na matumaini hayo anaelewa fika kuwa baadhi ya mambo ambayo alitarajia kufanya hakuweza kuyakamilisha lakini ana hakika kuwa balozi ajaye ataendelea nayo hadi kukamilika kwake.
“Katika kipindi changu hapa nimejitahidi kutekeleza majukumu yangu ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi yangu na Tanzania na naamini nimefanya vizuri lakini Balozi ajaye nina imani atafanya vizuri zaidi” alieleza Balozi Ranikh.
Alisema kuwa amefurahi kuona katika kipindi hicho uhusianao kati ya Russia na Tanzania katika maeneo ya uchumi na biashara umezidi kuimarika ambapo mikataba kadhaa ya ushirikiano imeweza kutiwa saini.
Balozi Ranikh alimueleza Mhe Rais kuwa kuanzishwa kwa masomo ya lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Kazakh huko Kazakhstan ni fursa nyingine ambayo inaweza kutumiwa kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza lugha ya Kiswahili kati ya Zanzibar na Kazakhstan.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini na Mshauri wa Rais Uhusiano wa Kimataifa, Uchumi na Uwekezaji Balozi wa Mohamed Ramia Abdiwawa.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
  E-mail: saidameir@ikuluzanzibar.go.tz & sjka1960@hotmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.