Habari za Punde

Dk Shein Azindua Madrasa Makunduchi leo.

 Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein, akisalimiana na wananchi alipofika kuzindua madrasatul Muzdalifah Mzuri Makunduchi leo wilaya ya kusini Unguja
Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,akifungua pazia kushiria uzinduzi wa Madrasatul Muzdalifah Mzuri Makunduchi leo Wilaya ya Kusini Unguja(kulia) Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi (CCM) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  Kazi,Utumishi wa Umma Mhe,haroun Suleiman
Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,akipata maelezo kutoka kwa mwalimu Mkuu wa Madrasatul Muzdalifah Mzuri Makunduchi Habib Mohamed Mussa baada ya kuzindua  Madrasatul Muzdalifah Mzuri Makunduchi leo Wilaya ya Kusini Unguja(kushoto) Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi (CCM) na Waziri wa Kazi,Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Mhe,Haroun Suleiman
Wanafunzi wa Madrasatul Muzdalifah Mzuri Makunduchi  wakimsikiliza Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein alipokuwa kitoa nasaha zake baada ya kuzindua madrasa hiyo iliyoko Mzuri Makunduchi Wilaya ya kusini Unguja leo,[Picha na Ikulu.]


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
       Zanzibar                                                                                               21.2.2015
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein  amefungua msikiti wa Kiongoni Makunduchi na kutoa nasaha zake kwa Waumini kuwa Msikiti ni nyumba ya Mwenyezi Mungu hivyo itumike kuwaunganisha waumini na sio kuwatenganisha au kuwagombanisha.

Alhaaj Dk. Shein alisema kuwa haitokuwa vyema kusikia mizozo ikiwa ni pamoja na kugombania uongozi wa msikiti miongoni mwa viongozi au Waislamu katika misikiti kwa sababu mbali mbali kwani matokeo hayo yatakuwa ni kinyume na malengo na azma ya kuuimarisha misikiti na kutozitumia vyema neema za Mwenyezi Mungu.

Alisema kuwa licha ya kuwa baadhi ya wakati wapo wanaokhafilika na kufanya hivyo ambapo Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa imani yake ni kuwa waumini watafuata nyayo za mashehe na Maulamaa waliopita katika kufuata matendo mema

Aidha, Dk. Shein alisisitiza kuwa msikiti huo pamoja na madrasatul alizozifungua ziwe ni chemchem ya elimu mbali mbali ikiwa ni pamoja na usomaji Kuran, Fikhi na taaluma nyengine za dini, malezi na imani.

Alhaj Dk. Shein alisema kuwa Kiongoni imetoa watu mbali mbali wenye maarifa makubwa kama marehemu Mzee Sheikh Idrisa Abdul Wakil ambaye alitoa mchango mkubwa katika maendeo ya nchi na sio wananchi wa Kiongoni na Makunduchi pekee yake bali wa Taifa zima.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwasisitiza waumini kuendelea kuhimizana juu ya umuhimu wa kuendeleza amani iliyopo kwa manufaa yao na vizazi viliopo na kuwataka wazazi kutochoka kusimamia malezi ya watoto na kuwaelekeza katika maadili mema sambamba na mienendo inayozingatia utamaduni na mafundisho ya dini.

Alhaj Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa msikiti na madrasa ni masuala ya kheri na yenye umuhimu katika kuuendeleza Uislamu. Mapema kabla ya ufunguzi wa Msikiti huo, Alhaj Dk. Shein alifungua madrasatul Tawheed iliyopo hapo hapo Kiongoni Makunduchi.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini kwa niaba ya Wananchi wa Makunduchi walitoa shukurani kwa Alhaj Dk. Shein  kwa kushiriki kikamilifu katika uzinduzi wa Madrasa pamoja na msikiti kwa nyakati tofauti katika kijiji hicho cha Makunduchi na kusisitiza haja ya kuitumia vizuri misikiti hiyo pamoja kuidumisha ili iwaneemeshe waumini na Uislamu kwa jumla.


Nao wanakijiji cha Kiongoni wakisoma risala yao walieleza kuwa wazo la kujenga msikiti huo lilitolewa kiasi cha miaka 110 iliyopita kutoka kwa mababu zao na kuishukuru familia ya Bwana Ali Kitambo kwa kukubali kutoa ardhi  yao kuwa ni Wakfu.

Walieleza kuwa baada ya kijiji hicho kupanuka msikiti huo uliendelea na ujenzi kwa msaada wa mfadhili Sheikh Mwinyi Mohamed Kitovu na baadae ulifanyiwa matengenezo na marehemu Sheikh Idrisa Abdulwakil pamoja na Sheikh Ibrahim Ali Suleiman na Sheikh Mustafa Ali Suleiman.

Baada ya hapo walisema kuwa mnamo mwaka 2013, Mhe. Mwakilishi wa Jimbo hilo la Makunduchi nae aliomba kuufanyia matengenezo zaidi na ndipo wanakijiji hao wakamuomba kuuzidisha msikiti huo ili uwe mkubwa zaidi.

Nae Mkuu wa Chuo cha Kiislamu Dk. Muhidin Siasa akitoa mawaidha katika hafla hiyo ya ufunguzi wa msikiti alieleza kuwa Makunduchi ni kitovu kikubwa cha Mashehe, na Maulamaa mbali mbali hivyo ipo haja ya kuendeleza utamaduni huo.

Wakati huo huo, Alhaj Dk. Shein alizindua Madrasatul Muzdalifa Al-Qadiria Shafii, huko Mzuri Makunduchi na kueleza kuwa kuna haja ya kuimarisha mashirikiano baina ya wazazi, walimu na  na jamaii yote kwa jumla katika kuwaepusha watoto na wanawake katika vitendo vya udhalilishaji.

Alisema kuwa jukumu la kuwalinda watoto na wanawake ni la watu wote na kusisitiza kuwa vitendo vya udhalilishaji wa watoto ni kinyume na maadili  na haki za binaadamu hivyo haipaswi kufumbiwa macho kwani vinatoa taswira mbaya  kwa jamii na mustakbali wa maisha ya watoto.

Alhaj Dk. Shein alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Taasisi na Mashirika mbali mbali  imeanzisha Kampeni ya miaka miwili ya kupambana na ukatili dhidi ya akina mama na watoto.

Kutokana na elimu zote zinatokana na Mwenyezi Mungu Alhaj Dk. Shein aliwanasihi wazazi na walezi kuwahimiza vijana kufuata na masomo ya skuli kwani Serikali imekuwa ikichukua jitihada za makusudi katika kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya elimu huku pia, Serikali ikiimarisha mazingira ya skuli zote za Zanzibar.

Nae Mwakilishi wa Jimbo la Makunduchi ambaye pia, ni Waziri wa  Nchi, Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma Mhe. Haroun Ali Suleiman alisema kuwa  mafanikio ya ujenzi huo wa Madrasa ya ghorofa moja umetokana na mashirikiano mazuri ya mfadhili na wananachi wa eneo hilo kupitia Kamati yao iliyo chini ya Mwenyekiti wake Mzee Makame Mudu.

Akisoma risala kwa niaba ya wa madrasa hiyo, Ustadh Ali Habib Suleiman alisema kuwa Madrasa hiyo imeanzishwa mnamo mwaka 1940 ambapo  baadae ikaendelezwa na
Mwalimu Bi Atamani binti Ali ambaye sasa ni marehemu kwa mashirikiano na Ustadhi Ramadhan Mwinyi  hadi kupata mfadhili mnamo mwaka 2013 na 2014 ujenzi ulikamilika ambao umegharimu Shilingi za Kitanzania Milioni 37.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwataka wazazi na walezi kushirikiana na waalimu katika kufuatilia masomom ya watoto pamoja na mienendo yao ili kuwaepusha na utoro na kuacha vitendo viovu.

Nae Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji alitoa shukurani kwa niaba ya Ofisi yake kwa mfadhili wa Madrasa hiyo na kusisitiza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kuendelea na jitihada zao katika kutoa elimu bora ya dini kwa vijana.

Aidha, Dk. Shein alikubali ombi la madrasa hiyo la kuwapatia kompyuta moja pamoja na printa yake  huku akiwaahidi kuwaunga mkono pale watakapokuwa tayari kuanza ujenzi wa nyumba ya mwalimu mkuu wa Madrasa hiyo pamoja na kuanza skuli ya maandalizi ndani ya Madrasa hiyo kama walivyoomba katika risala yao.

Rajab Mkasaba, Ikulu

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.