Habari za Punde

Jumuiya ya Blue Health Zanzibar Yatoa Taaluma kwa Wanafunzi wa Masomo ya Sayansi ya Kensa

Na Ramadhani Ali – Maelezo.
Wanafunzi  wa skuli za sekondari wanaosoma masomo ya Sayansi na walimu wao Tanzania wamesisitizwa kuongeza juhudi katika  masomo yao  na kufanya tafiti zitakazosaidia kugundua matatizo ya afya yanayoikabili nchi hivi sasa ikiwemo maradhi ya Kensa.

Rais wa Jumuiya ya wataalamu wa fani mbali mbali za Afya Zanzibar yenye lengo la kutoa taaluma ya maradhi tofauti kwa wananchi (Blue Health Organisation) Gora Faki Haji ametoa ushauri huo katika semina ya  kuelimisha tatizo la maradhi ya Kensa iliyowashirikisha baadhi ya wanafunzi wa  masomo ya Sayansi wa skuli za sekondari katika skuli ya Haillesselassie.

Amewaeleza wanafunzi hao kwamba  Kensa ni miongoni mwa maradhi hatari yanayosumbua wananchi wengi Tanzania na idadi kubwa ya watu wanaopata maradhi hayo hupoteza maisha.

“Takwimu  za maradhi ya Kensa  kutoka Hospitali ya Ocean Road, inayoshughulikia maradhi hayo, zinaonyesha kuwa  asilimia 14 tu ya watu waliopata Kensa  waliweza kupona,” alisema Gora Faki Haji.


Rais  huyo wa Blue Health Organisation omeongeza kuwa asilimia 66 ya wagonjwa wa kensa  waliofika  Ocean Road  kupatiwa matibabu ni wanawake na asilimia 24 ndio wanaume na hiyo inaonyesha wanawake  wanaosumbuliwa zaidi na maradhi hayo.

Amesema pamoja na kuwa hakuna sababu  rasmi inayopelekea  kupata kensa moja kwa moja lakini amesema matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku, utumiaji wa pombe na mpangalio usioridhisha wa chakula unachangia kupata tatizo la maradhi hayo.

Amewataka wananchi kujiepusha na viashiria  vinavyoweza kupelekea kupata kensa na kuwa na utaratibu mzuri wa chakula ikiwemo kutumia zaidi matunda na  mboga za majani.

Amewashauri watu kujenga tabia ya kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara na kuwa na  tahadhari  wanapopata tatizo la mivimbe katika miili yao.

Amewahakikishia wananchi  kuwa Blue Health Organisation itaendeleza lengo la kutoa taaluma  ya masuala ya afya kwa makundi tofauti  ili waweze kujua sababu zinazopelekea maradhi na njia za kujiepusha nayo.

Semina hiyo iliwashirikisha wanafunzi wa skuli za Sekondari Lumumba, Benbella, Hamamni na baadhi ya walimu wa skuli hizo wanaosomesha masomo ya Sayansi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.