Habari za Punde

Maelezo kuhusu uzinduzi wa bodi ya udhamini ya mfuko wa waasisi wa taifa

 

MAELEZO YA NAIBU KATIBU MKUU (UTUMISHI) Bw. HAB Mkwizu WAKATI WA UZINDUZI WA BODI YA UDHAMINI YA MFUKO WA WAASISI WA TAIFA LETU (MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE NA SHEIKH ABEID AMANI KARUME)

Mheshimiwa Mgeni Rasmi (Katibu Mkuu OR - MUU),

Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bodi,



Waheshimiwa Mabalozi wa Nchi mbalimbali,

Waheshimiwa Viongozi Wastaafu,

Ndugu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,

Waheshimiwa Wajumbe wa Bodi ya Udhamini ya Kuwaenzi Waasisi,

Waheshimiwa Wawakilishi wa Familia za Waasisi wetu,

Wageni Waalikwa,

Waandishi wa Habari,

Ndugu Viongozi Waandamizi wa Serikali,

Mabibi na Mabwana.
Kwanza kabisa ninapenda kuchukua fursa hii kuwakaribisheni katika Uzinduzi wa Bodi ya Udhamini ya Mfuko wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume inayozinduliwa rasmi leo.
Wageni Waalikwa, mabibi na mabwana, kama mnavyofahamu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume ni Waasisi waliotoa mchango mkubwa katika taifa hili. Hivyo, kwa kuthamini mchango wao kiuchumi, kisiasa na kijamii ndani na nje ya nchi yetu, Serikali imeamua kuunda bodi ambayo pamoja na mambo mengine itatafuta fedha za kugharamia uendeshaji wa Kituo kitakachotunza kumbukumbu, vitu na mali za Waasisi hawa zenye umuhimu wa kihistoria a katika Taifa letu.

Mheshimiwa mgeni rasmi, mbele yako ni Mwenyekiti wa Bodi Kanali Mstaafu Kabenga Nsa Kaisi aliyeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuongoza bodi ya Mfuko wa Udhamini wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, na Wajumbe sita (6) uliowateua wewe kwa mujibu wa Sheria Namba 18 ya Mwaka 2004 ya Kuwaenzi Waasisi wa Taifa letu ambao ni: Mhe. Jaji Augustino S.L. Ramadhani, Bi. Mwatumu Jasmine Malale, Dk. John M. J. Magotti, Dk. Khalid S. Mohamed, Bw. Issa I. Mohamoud na Bi. Aisha Kombo Haji. Aidha, wapo pia Wajumbe watatu(3) ambao ni wawakilishi wa familia za Waasisi wa Taifa ambao wameteuliwa na familia za Waasisi kwa mujibu wa Sheria.

Hata hivyo, uteuzi wa jina moja toka familia ya Sheikh Abeid Amani Karume bado haujakamilika. Majina ya Wawakilishi wa familia walioteuliwa ni: Mama Fatma Abeid Karume, Bi. Rosemary Julius Nyerere na Bw. Madaraka Julius Nyerere. Naomba niwapongeze wote kwa kuteuliwa kwenu kuwa wajumbe wa Bodi hii.


Mheshimiwa Mgeni Rasmi, ninaomba kutoa historia fupi ya dhana ya Kuwaenzi Waasisi wa Taifa letu. Chimbuko na azma ya kuwa na utaratibu wa kuwaenzi Waasisi wa Taifa letu (Mwalimu Julius Kambarage  Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume), ni mapendekezo mbalimbali ya Viongozi, mikutano na maandiko kadhaa ndani na nje ya nchi, na Wananchi kwa ujumla juu ya umuhimu wa kutambua na kuthamini mchango wa Waasisi hawa katika harakati za kupata uhuru wetu, kuimarisha mshikamano, umoja na kujenga uzalendo kwa wananchi wa Tanzania bara na Zanzibar. Tunawaenzi Waasisi hawa kwa kudumisha fikra zao, kwa kutunza kumbukumbu, vitu na mali zao zenye umuhimu wa kihistoria kitaifa.

Mheshimiwa mgeni rasmi, kutokana na msukumo huo mwaka 2004, Serikali ilitunga Sheria ya Kuwaenzi Waasisi wa Taifa Na. 18. Pamoja na mambo mengine, Sheria hii inaelekeza uanzishwaji wa Kituo cha kuwaenzi Waasisi wa Taifa letu. Majukumu ya kituo hicho ni kusimamia shughuli zote za kuwaenzi Waasisi ikiwa ni pamoja na kukusanya, kuhifadhi kumbukumbu, vitu na mali za Waasisi zenye umuhimu wa kihistoria kwa maslahi ya Umma.


Mheshimiwa Mgeni Rasmi, baada ya kupitishwa Sheria hii, Serikali ilichukua hatua mbalimbali za kuitekeleza ikiwa ni pamoja na:-



 Kuandaa kanuni,

 Kuandaa Muundo wa Kituo cha Kuwaenzi Waasisi,

 Kuanzisha ofisi ya muda itakayoratibu uanzishwaji wa Kituo,

 Kutafuta mtaalam Mshauri wa kuishauri Serikali namna ya kuanzisha na kuendesha, kituo.

 Kutafuta eneo la kujenga kituo cha kuhifadhi kumbukumbu, vitu na mali za Waasisi wa Taifa,


Kutambua mahali zilipo kumbukumbu, vitu na mali za Wasisi kabla ya kuanza kuzikusanya na kuzihifadhi katika Kituo, na



 Kuunda Bodi ya Udhamini ya Mfuko wa Waasisi ambayo inazinduliwa leo hii.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, kwa mujibu wa Muundo, Kituo cha Kuwaenzi Waasisi ni Sehemu (Section) ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa iliyopo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kwa upande wa Tanzania Bara. Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, shughuli za kuwaenzi Waasisi zinaratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, katika idara ya Maadhimisho na Sherehe za Kitaifa. Aidha, muundo wa kituo unatambua uwepo wa Bodi ya udhamini inayosimamia mfuko wa Waasisi (The Mwalimu Julius Kambarage Nyerere and Sheikh Abeid Amani Karume Trust Fund). Majukumu makuu ya kituo cha kuwaenzi Waasisi kama yalivyoelekezwa katika Sheria ya Kuwaenzi Waasisi wa Taifa letu kwa sasa ni yafuatayo:

Kuhakikisha kuwa Kumbukumbu na vitu vilivyohifadhiwa katika kituo cha Waasisi zinatunzwa vizuri na zinajulikana kwa umma;

Kukusanya, kuhifadhi kumbukumbu na vitu vya Waasisi vyenye umuhimu wa kihistoria kitaifa;

Kuandaa na kutekeleza taratibu za kuteketeza kumbukumbu na vitu vya Waasisi visivyo na umuhimu wa kudumu;

Page 5 of 8

Kushirikiana na Mfuko wa udhamini wa Kituo, kutafuta fedha zitakazotumika na kituo au kufanyia kazi zinazohusiana na kituo, na

Kuhamasisha, kutangaza na kusaidia kufanyika kwa tafiti na kuandaa machapisho ya vitu vinavyoonekana na visivyoonekana kuhusu Waasisi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mgeni rasmi, baadhi ya mafanikio muhimu yaliyopatikana katika uanzishwaji wa kituo cha Kuwaenzi Waasisi wa Taifa;

Kutungwa kwa Sheria Na. 18 ya mwaka 2004 ya Kuwaenzi Waasisi wa Taifa na Kanuni zake za mwaka 2005;

Muundo (organization structure) wa kituo cha Kuwaenzi Waasisi umeandaliwa na kupitishwa. Kituo cha Waasisi kimekuwa ni sehemu (section) ya Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma;

Mpango mahsusi na miongozo (Business plan and operational Mannuals) kwa ajili ya uendeshaji wa Kituo cha Kuwaenzi Waasisi imeandaliwa na Mtalaam Mshauri;

Kupatikana kwa eneo la kujenga kituo cha kuwaenzi Waasisi wa Taifa katika Wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani;

Kuanzishwa kwa ofisi ya muda ya Kituo cha Kuwaenzi Waasisi;

Kuandaliwa kwa orodha ya Kumbukumbu, vitu na Mali za Waasisi zenye umuhimu wa kihistoria;

Kuzitambua Taasisi mbalimbali zenye hifadhi ya Kumbukumbu, vitu na Mali za Waasisi wa Taifa, ambazo zimefanywa kuwa ni matawi (declared places of deposits) kwa mujibu wa Sheria;


Kuadhimisha siku za kuwaenzi Waasisi wa Taifa kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa midahalo, makongamano, maonyesho n.k.;

Kufanyika kwa upembuzi yakinifu (feasibility study) katika eneo la kujenga kituo cha Waasisi;

Kufanyika kwa tathmini ya athari za kimazingira na kijamii (Environmental and Social Impact Assessment) za mradi wa kujenga kituo cha Waasisi wa Taifa, katika eneo la kujenga Kituo lililopo katika kijiji cha Kiromo Wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani; na

Kuundwa kwa Bodi ya Udhamini ya Mfuko wa Waasisi (The Mwalimu Julius Kambarage Nyerere and Sheikh Abeid Amani Karume Trust Fund);

Mheshimiwa Mgeni rasmi, pamoja na mafanikio hayo Kituo cha Kuwaenzi Waasisi pia kina mikakati mbalimbali ya kukuza na kupanua wigo wa utoaji huduma zake kwa umma. Baadhi ya mikakati hiyo ni;

Kuanzisha Kituo Cha kuhifadhia kumbukumbu zote za Waasisi wa Taifa letu (Hayati Mwalimu J.K. Nyerere na Sheikh Abeid A. Karume) na kuzihifadhi vizuri. Kituo hiki kitajengwa Bagamoyo eneo la Kiromo;



Kuendelea kukusanya Kumbukumbu, Vitu na Mali za Waasisi zenye umuhimu wa kihistoria kutoka kwa Watu binafsi, Taasisi na Asasi mbalimbali;

Kuendelea kukusanya historia simulizi (oral documentary) kuhusu Waasisi wa Taifa toka kwa watu maarufu waliowahi kufanya kazi kwa karibu na Waasisi wa Taifa;

Kuendelea kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kuwaenzi Waasisi wa Taifa kwa kudumisha fikra zao;

Kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Waasisi wa Taifa;

Kuendelea na jitihada za kuboresha mazingira ya kazi kwa kuweka vitendea kazi vipya vinavyoendana na hali halisi ya mazingira ya kisasa.

Mheshimiwa Mgeni rasmi, kabla sijamaliza ningependa pia nitoe changamoto zinazotukabili katika uanzishwaji wa Kituo cha Kuwaenzi Waasisi wa Taifa, ambazo nadhani ni vizuri mkazijua kwani zitakuwa ni sehemu ya majukumu ambayo tutashirikiana kuyatatua kwa pamoja;

Ukosefu wa fedha za kugharamia kazi za Kituo cha Kuwaenzi Waasisi.

Uelewa mdogo wa baadhi ya watu binafsi, taasisi na asasi mbalimbali kuhusu umuhimu wa utumiaji na utunzaji bora wa kumbukumbu, hivyo, kutokutoa kipaumbele katika suala zima la utunzaji wa

Page 8 of 8



kumbukumbu na nyaraka. Hali hii inasababisha tatizo kubwa la kuharibika kwa kumbukumbu, vitu na mali za Waasisi kabla hazijakusanywa na kuhifadhiwa katika Kituo cha Kuwaenzi Waasisi wa Taifa;
Ukosefu wa vifaa vya kurekodia historia simulizi unachelewesha ukusanyaji wa taarifa toka kwa watu waliowahi kufanya kazi kwa karibu na Waasisi hasa ikizingatiwa kuwa wengi wa watu hawa ni Wazee sana;

Uwepo wa Taasisi zingine ambazo zinafanya kazi zinazofanana na za kituo cha Kuwaenzi Waasisi, uelewa mdogo kuhusu Sheria ya Kuwaenzi Waasisi wa Taifa na hivyo, uwezekano wa kuwepo mgongano wakati wa utekelezaji wa majukumu ya Kituo.

Wageni Waalikwa, mabibi na mabwana, Kwa maelezo haya mafupi, naomba nimkaribishe Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, aweze kutoa nasaha na baadae kuzindua rasmi Bodi ya Udhamini ya Mfuko wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.