Habari za Punde

NEC yasogeza mbele uandikishaji

Na Mwandishi Wetu
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesogeza mbele tarehe ya kuanza kuandikisha wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura.
 
Zoezi hilo lililokuwa lianze Februari 19 mwaka huu sasa litaanza kufanyika Februari 23 katika mkoa wa Njombe.
 
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu, Damian Lubuva, alisema sababu ya kusogeza mbele ni kuchelewa kufika vifaa vya kuandikisha.
 
Alisema vifaa vilivyopo kwa sasa ni 250 tu ambavyo vilitumika katika uandikishaji wa majiribio na vifaa vyengine 7750, vinasubiriwa kufika nchini hivi karubuni.
 
Aidha alisema sababu nyengine ya kuahirisha ni kuitikia wito wa wadau hasa vyama vya siasa vilivyoomba zoezi hilo lisogezwe mbele ili kupata muda wa kujiandaa.

Alisema vyama vya siasa vitatumia muda uliobakia kuwaandaa mawakala wao kwa ajili ya kushiriki zoezi hilo.
Uandikishaji wa wapiga kura wapya utafanywa kwa kutumia Teknolojia mpya ya Biometric Vote Regstration ( BVR).

Mfumo huo mpya ni wa kuchukua au kupima taarifa za mtu za kibaiolojia au tabia ya mwanadamu na kuhifadhi katika kanzi data kwa ajili ya utambuzi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.