Na Rahma Khamis Maelezo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar Mh; Haji Omar Kheri amewapongeza
Walimu na Wazazi wa Almadrasatul Nurul-Munawwara kwa kuonyesha
mashirikiano kati yao jambo ambalo linalopelekea kuwepo kwa ufaulu mzuri wa
wanafunzi chuoni hapo.
Pongezi hizo amezitoa huko Tumbatu Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja katika Madrasa hiyo wakati wa
mahfali ya kusheherekea maulidi ya
kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW).
Waziri huyo amemshukuru Mwalimu Mkuu wa Madrasa hiyo
kwa kuiendeleza sambamba na kumuenzi Marehemu Bakari Juma Khamis ambae ndiye muanzilishi wa Madrasa hiyo.
“Namshukuru marehemu Bakari kwa mchango wake Mungu
amlaze mahala pema Peponi na sisi tuliobaki nyuma yake atujaalie kila la kheri”,
alieleza Waziri huyo.
Aidha amesema kuwa katika kumuenzi Marehemu huyo ni vizuri watu wakatoa mali zao kwa ajili ya
Allah (SW) kwa wenye uwezo na asiye na uwezo ni vizuri akajitolea kwa hali na mawazo
mazuri ambayo yatasaidia kwa njia moja au nyengine katika kuindeleza madrasa hiyo.
“Watu wa Tumbatu watoe kwa hiari yao na waichangie madrasa hii kwani kufanya hivyo
itakua ni bora zaidi kuliko kusubiri
Wageni kutoa michango yao ’’,
alisema Waziri huyo.
Hata hivyo Waziri huyo ameahidi kuichangia Madrasa
hiyo kwa hali na mali
ili iwe katika kiwango kizuri, cha kisasa na chenye kuridhisha.
Nae Mwalimu Mkuu wa Madrasa hiyo Nd. Jecha Ali Saleh amemshukuru Waziri huyo
kwa mchango huo mkubwa alioutoa kwa
kuchangia zaidi ya asilimia 55 katika ujenzi wa Madrasa hiyo.
Akielezea baadhi ya changamoto zinazoikabili madrasa
hiyo Mwalimu huyo amesema mfumo wa kuanzishwa kwa masomo ya ziada maskulini kunapelekea
kuporomoka kwa mfumo mzima wa mwenendo wa Madrasa kwani wanafunzi huwa hawahudhurii ipasavyo masomo Chuoni hapo sambamba na ukosefu wa Banda lenye nafasi ya kutosha kwa ajili ya kusomea wanafunzi hao kwani
huchanganyika pamoja wakati wa masomo chuoni hapo.
“Tuna Madarasa matatu lakini hayatoshelezi kwani Wanafunzi wa miaka 4 hawawezi kukaa na
Wanafunzi wa miaka 20 wala miaka 14 hawawezi kukaa na wa miaka 4 hivyo
tunahitaji Darasa kubwa zaidi kwa ajili ya watoto wetu”, Mwalimu huyo alisema.
Mwalimu Jecha amewataka wafadhili
wazingatie njia za kukuza imani ya Dini kuongeza misaada yao kwa kuisaidia Tumbatu
Jongowe.
“Watu waondokane na dhana potofu kwa kuona kuwa watu
wakitoa msaada haitofanyiwa jambo lenye maana hiyo sikweli na watu waachane na
dhana hiyo”, amesema Mwalimu Jecha.
Aidha Shekh Haji Makame Mshenga amewataka watu wenye
uwezo kutoa misaada katika mambo ya kheri, ili walimu wazidi kua na moyo wa
kuwafundisha wanafunzi pamoja na kutoidharau Dini ya Kiislamu kwani ndio
muongozo wa maisha ya kila siku ya mwanadamu.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na Madrasa mbalimbali ikiwemo
Madrasatul Jauharil-Atfaal, Maamur, Nurul- Islamiyah, Tawhid Lilah, Manaqibul-Kadriya
na Madrasatul Murabiyatul- Islamiyah zote kutoka kijijini Tumbatu.
No comments:
Post a Comment