STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
19.02.2015

Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesisitiza umuhimu wa
wafanyabiashara na wananchi wote kwa jumla kuendelea kulipa kodi kwa mujibu wa
sheria za nchi ili kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake ipasavyo
ikiwemo kutekeleza miradi ya maendeleo na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza na uongozi wa Wizara ya Fedha Zanzibar katika mkutano wa
kutathmini utekelezaji wa mpango kazi na bajeti ya Wizara ya Fedha Zanzibar
huko Ikulu leo, Dk. Shein amesema hakuna namna ambayo itaiwezesha Serikali
kufanya kazi zake kwa ufanisi bila ya kuwa na nyenzo ya fedha ambazo
upatikanaji wake unatokana na makusanyo ya kodi.
“hakuna namna ya kuendesha serikali bila ya mapato yanayotokana na kodi, na
suala hili ni la kihistoria halikuanza leo, kila mtu ni lazima alipe kodi kwa
mujibu wa sheria”, alisisitiza.
Rais wa Zanzibar ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara ya Fedha kwa kusimamia
vyema ukusanyaji wa mapato ya ndani katika kipindi cha miezi sita Julai –
Disemba 2014, ambapo jumla ya Shilingi 175,659 milioni sawa na asilimia 91 ya
makadirio ya miezi sita zilikusanywa.
Fedha hizo zinajumuisha mapato ya kodi ya TZS 86,185 milioni yaliyokusanywa
na Bodi ya Mapato ya Zanzibar ZRB ambayo ni sawa na asilimia 96 ya makadirio
na TZS 70.402 yaliyokusanywa na Mamlaka
ya Kodi Tanzania TRA kwa upande wa
Zanzibar ambayo ni sawa na asilimia 86 ya makadirio.
Makusanyo hayo pamoja na makusanyo mengine yasiyokuwa ya kodi katika
kipindi cha miezi sita iliyopita yameonesha ongezeko la asilimia 12
ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Vile vile Rais wa Zanzibar ameipongeza Wizara hiyo kwa kuweza kusimamia
vyema ugawaji na matumizi ya fedha hizo ambazo kwa mujibu wa taarifa za Wizara
zote zilizowasilisha taarifa zake kwenye vikao hivyo zimeonesha mafanikio
makubwa ya utekelezaji kifedha.
Akizungumzia maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa huduma za jamii Zanzibar
(ZUSP), Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ameelezea
kuridhishwa kwake na hatua ya utekelezaji wa mradi huo, ambao unajumuisha kazi
kadhaa ikiwemo kazi za ujenzi wa njia za kupitishia maji ya mvua, taa za mjini
na ukarabati wa ofisi ya Baraza la Manispaa.
Hata hivyo, ametoa wito wa kuandaliwa utaratibu maalum wa kuwasilisha
taarifa hizo kwa wananchi, kwani alisema bado baadhi ya wananchi hawana taarifa
za kutosha juu ya maendeleo ya mradi huo.
Amefahamisha kuwa wananchi wamekuwa wakisubiri kwa hamu kukamilika kwa
mradi huo kutokana na ahadi walizoahidiwa na viongozi mbali mbali, hivyo ni
vyema wakaarifiwa ipasavyo kuhusiana na maendeleo yake.
Akiwasilisha taarifa ya Wizara yake, Waziri wa Fedha Mheshimiwa Omar Yussuf
Mzee amesema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana na Wizara yake, bado
wanakabiliwa na changamoto ya kutotabirika kwa mapato yasiyokuwa ya kodi na
mapato yatokanayo na misaada na hivyo kupelekea ugumu wa kujua muda na kiasi
cha fedha ambacho kitapatikana kila mwezi.
Changamoto nyengine ni kwa baadhi ya walipa kodi kushindwa kuwajibika
kulipa kodi ipasavyo na kuongezeka matumizi ya dharura yasiyokuwemo katika
bajeti ya Serikali ya mwaka 2014/2015.
Hata hivyo amesemam changamoto hizo zote zimo ndani ya uwezo wa Wizara na
zinaendelea kupatiwa ufumbuzi.
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment