Habari za Punde

Rais Dk Shein Amewataka Walimu wa Madrasa Kuwafundisha Dini na Malezi Bora

Na Othman Khamis OMPR
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Al-Hajj Dr. Ali Mohammed Shein alisema tatizo la baadhi ya walimu wa madrasa hapa nchini la kushindwa kutimiza wajibu kwa kuwafundisha dini na malezi bora watoto limekuwa likiondoa heshima kwa walimu hao.

Alisema vitendo vya aina hiyo havikubaliki katiba maadili ya uislamu kwani vinakwenda kinyume na mafundisho ya dini sambamba na kuwatia hofu wazazi kiasi cha kuwakataza watoto wao kushiriki darsa hali inayowakosesha haki ya msingi ya kupata elimu watoto hao.

Rais wa Zanzibar  Al- Hajj Dr. Ali Mohammed Shein alisema hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seiof Ali Iddi wakati wa hafla ya ufunguzi wa Masjid Bilal na Madrasat Taawun Chaani Mvumoni Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Al- Hajj Dr. Shein alisema katika hali isiyopendeza jamii na waumini wanaendelea kushuhudia mizozo katika baadhi ya misikiti pamoja na baadhi ya walimu kuendeleza vitendo visivyo na maadili mambo ambayo ni kinyume na mafundisho ya dini yanayosisitiza umuhimu wa kudumisha umoja na mapenzi miongoni mwa waumini hao.


Alisema kwa bahati mbaya vitendo vya walimu vilivyo nje ya maadili vimekuwa vikiripotia kuwepo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja. Hivyo waumini, walimu na wananchi wote wana wajibu wa kusimama kidete katika kuvikemea kwa kupambana navyo kwa kushirikiana na vyombo vya Dola.

Rais wa Zanzibar alisema kwamba ni jukumu la kila mtu kuhakikisha kwamba anashirikiana na mwenzake ili jamii yote irejee katika yale maadili mema yaliyozoeleka ya kupendana na kuhurumiana.

Alielezea matumaini yake kwamba Msikiti huo mpya wa Bilal na Madrasat Taawun Chaani Mvumoni  vitakuwa ni kitovu cha Elimu ya dini na maarifa mbali mbali yatakayoleta manufaa kwa jamii na hawa watoto ili kujenga jamii bora ya wacha mungu na raia wema wa baadaye.

Alisisitiza umuhimu wa mashirikiano katika kuzitunza hazina hizo mbili na kuona kuwa zinatoa matunda mazuri yatayotegemewa ya kupata vijana wenye elimu watakayochukuwa nafasi za masheikh waliopo sasa na wale waliotangulia mbele ya haki.
Dr. Shein alifahamisha kwamba ujenzi wa Msikiti na Madrasa ni kuujenga na kuuendeleza Uislamu hatua inayoashiria kuendelezwa kwa jitihada zilizoanzishwa na Kiongozi wa Umma wa Uislamu Mtume Muihammad { SAW }.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alielezea matumaini yake kwamba Waumini wa Kijiji cha Mvumoni wameridhika kwa kupata nyumba nzuri ya ibada na Madrasa zitakazokidhi kiu waliyonayo ya muda mrefu.

Aliikumbusha Kamati ya msikiti juu ya wajibu muhimu iliyonao wa kusimamia maendeleo ya msikiti huo kwa manufaa ya waumini sambamba na kuwepo kwa taratibu za kusimamia usafi na huduma zake ili nyuumba hiyo tukufu ibakie katika hali ya usafi na kupendeza wakati wote.

“ Wahenga waliosema, kitunze kidumu. Kwa hivyo kuutunza msikiti huu ni kuudumisha na ni namna ya kuonyesha shukrani kwa Mwenyezi Mungu za kupata neema hiyo “. Alisema Dr. Shein.

Rais wa Zanzibar aliishukuru na kuipongeza Kamati iliyosimamia ujenzi wa msikiti huo inayoongozwa na Rais Mstaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Al- Hajj Ali Hassan Mwinyi kwa uamuzi wake wa busara iliowapa fursa waislamu wa Chaani Mvumoni kupata pahala pazuri pa kufanyia ibada.

Alisema kujishughulisha na masuala ya ujenzi wa misikiti na madrasa ni namna bora ya kuitumia neema ya Mali na nguvu za Mwenyezi Muungu alizowaruzuku waja wake katika mambo anayoyaridhia ikiwa ni ucha mungu.

“ Aliikariri moja ya hadithi mashuhuri na Mtume Muhammad { SAW } iliyoeleza. Mkimuona mtu anajishughulisha na msikiti, basi shuhudieni kwa mtu huyo imani ya kweli “. Alifafanua Al- Hajj Dr. Ali Mohammed Shein.

Mapema akitoa maelezo mafupi ya ujenzi wa Msikiti Bilal Msimamizi wa Ujenzi katika  Kamati ya  Uendelezaji wa misikiti na Madrsa Nchini ambae pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mh. Moh’d Raza Hassanali alisema usimamizi wa msikiti na madrasa zinazojengwa kupitia Kamati hiyo unakuwa chini ya Kamati zinazoundwa na wenyeji wa maeneo husika.

Mh. Raza alisema alitahadharisha kwamba hitilafu na migogoro baina ya waumini wenyewe ndio cheche ya kuzaa uhasama baina ya waumini ambayo chanzo kikuu ni tabia ya baadhi ya waumini kung’ang’ania kusimamia kinyume na utaratibu misikiti na madrasa.

Naye  Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Mkoa wa Kaskazini Unguja Sheikh Khamis Abdulhamid alisisitiza ulazima kwa waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kutunza nyumba za Mwenyezi Muungu yaani Misikiti.
Sheikh Abdulhamid alisema nuru ya alla hupatikana katika nyumba hizo tukufu kutokana na kazi yake kubwa ya kutunza Maamrisho ya Mola yatokanayo na 
Kitabu chake kitukufu cha Quiran.

Akitoa Hotuba ya Sala ya Ijumaa mara baada ya ufunguzi wa Msikiti huo wa Ijumaa wa Kijiji cha Bandamaji Kivumoni Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Suleiman Soraga alisema sifa njema ya Zanzibar ambayo wazee wanaielewa hivi sasa imepotea.

Sheikh Soraga alisema jamii inapaswa kujikita zaidi katika kupambana na mmong’onyoko wa maadili uliozaa ufisadi  na matokeo yake maasi yameongezeka mara dufu ndani ya mitaa hapa nchini.

Alieleza na kuasa kwamba ye yote atakayemuasi muumba wa mbingu na ardhi aelewe kwamba tayari ameuvaa ufisadi unaobeba chuki, uhasama, maonevu kwa wasio na hatia na hatimae huruma inatoweka ndani ya jamii.

Alikariri Quran tukufu katika aya zake zinazofafanua kwamba Mwenyezi Muungu ameapa na kuahidi kuwa atawaonyesha adhabu kali kwa yale matendo wanayoyachuma kwa mikono yao wenyewe.

Kwa upande wake akitoa salamu kwa waumini wa Dini ya Kiislamu wa Kijiji cha Bandamaji Mvumoni Mwenyekiti wa Kamati ya uendelezaji Misikiti na Mdrasa Nchini Rais Mstaafu wa Tanzania Al-Hajj Sheikh Ali Hassan Mwinyi amewapongeza Wananchi wa Bandamaji wa kupata msikiti mpya utakaowapa utulivu wakati wa kutekeleza ibada zao za sala.

Mzee Mwinyi alisema waumini hao wanapaswa kujikita zaidi hivi sasa katika kutafuta elimu na nusra ya Mwenyezi Muungu kwa kufanya ibada kwa wingi huku wakitekjeleza wajibu wa kuwalea watoto wao katika misingi na maadili ya Dini.

Msikiti Mpya wa Ijumaa wa Kijiji cha Bandamaji Mvumoni una uwezo wa kusaliwa na waumini wasiopungua mia mbili kwa wakati mmoja wa sala.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.