Mada: Misingi Mikuu ya Uandishi wa Habari za Uchaguzi na Utambuzi wa viashiria vya uvunjifu wa amani
Imetayarishwa na kuwasilishwa na:
Rashid Omar Kombo,
Chuo cha
UandishiwaHabari,
Zanzibar. (ZJMMC)
PGD-SW- ISW – Dar-es-Salaam
ADJ. SJMC –UDSM- Dar-es-Salaam
MISINGI MIKUU YA
UANDISHI WA HABARI ZA UCHAGUZI NA UTAMBUZI WA VIASHIRIA VYA UVUNJIFU WA AMANI
UTANGULIZI
Ujenzi wa demokrasia ya kweli kupitia
mfumo wa uchaguzi wa vyama vingi unahitaji kwa kiasi kikubwa mchango wa wadau
mbalimbali,vikiwemo vyombo vya habari makini vinavyoweza kuisaidia jamii
kuchagua viongozi wanaofaa na wanaomudu kuchapuza kasi ya maendeleo wanayoyahitaji.
Ni kwa msingi huo wa mchango na
wajibu vilionao vyombo vya habari na ndio maana hivi sasa duniani kote hasa
kwenye mfumo wa utawala bora (good governance system)hali hiyo inakubalika, na
vyombo hivi vinapewa nafasi kuwa na wajibu mkubwa katika kushajiisha kasi ya maendeleo
na vinaelezwa kwamba ni muhimili wa nne wa dola usio rasmi ukiacha ule wa Serikali,
Bunge na Mahakama.
Kidemokrasi na utawala bora,vyombo
hivi vya dola kila kimoja vinatakiwa kufanya kazi zake bila kuingiliwa na
chombo chengine, lakini chombo kimoja kinapovuka mipaka ya wajibu wake hakuna
kosa kwa chombo chengine kueleza bayana hali iliyotokea hata ikiwa ni kwa njia
ya kukosoa moja kwa moja ama vyenginevyo.
Ndio maana masuala ya uhuru wa habari
yameelezwa katika Kifungu cha 18 cha Katiba ya Zanzibar na pia kifungu cha 19
cha Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1946.
Vifungu hivi vyote vinazungumzia haki
ya kupata na kutoa habari kama ni miongoni mwa haki za binadamu ambapo
kukosekana kwake ni kuvunjwa kwa haki hizo kama sehemu binadamu anazostahiki
kuzipata wakati wote.
Hivyo basi, mada hii inalenga
kuchokoza mawazo ya washiriki na itajikita katika maeneo sita muhimu ambayo ni
maana ya vyombo vya habari kwa muhtasari, dhima na wajibu wa vyombo hivyo kwa
jamii, misingi muhimu ya vyombo vya habari katika kuandika habari za uchaguzi
na mambo muhimu kwa vyombo vya habari
kuzingatia katika masuala ya habari za uchaguzi na baadaye nitaelezea kiini cha
mada hii yaaniviashiria vya uvunjifu
wa amani wakati wa uchaguzi, na baadaye tutamalizia uchokozi huu kwa
mapendekezo na hitimisho la mada.
MAANA YA VYOMBO VYA HABARI
Vyombo vya habari vinaweza kuwa na
tafsiri tofauti, lakini msingi muhimu wa tafsiri hiyo ni uwezo wa kufanya
mawasiliano kwa kufikisha taarifa, ujumbe ama kufanya mawasiliano kati ya
mpelekaji na mpokeaji wa habari.Ujumbe utakapopelekwa na kupokelewa hapo unaweza
kuita vyombo vya habari vimetumikakwa kuwa mawasiliano ya pande mbili
yamefanyika na walengwa tena waliowengi zimewafikia kwa wakati mmoja.
Wapo pia wanaosema kwamba vyombo vya
habari ni nyenzo inayotumika kufanya mawasiliano kwa jamii ya waliowengi (umma)
kwa wakati mmoja. Vyombo hivi ni kama vile redio, televisheni na magazeti,
majarida na hata mitandao.
Lakini pia zipo aina mpya za vyombo
vya habari vya kijamii kama vile mitandao ya facebook, Twita, whatsapp na
vyengine vya aina hiyo mbalimbali vinavyotumia mawasiliano ya Itaneti, simu na
kadhalika.
Aidha, kiumiliki, vyombo vya habari
vinaweza kuwa vya Serikali. Vyombo vya habari vya Serikali huendeshwa kupitia
bajeti ya umma na vinafanya kazi zake chini ya Sera na Miongozo ya Serikali, na
moja kazi ya lengo lake kuu ni kuitetea Sera na Mipango ya Serikali
inayovimiliki.
Vyombo vya habari binafsi mara nyingi
huwa ni vya kibiashara zaidi na pia sera zake zinalenga zaidi kuongeza faida
kwa wamiliki kutokana na uzalishaji wenye tija, kwa kuzingatia sera za
kibiashara zaidi na kutimiza lengo la kuanzishwa kwake yaani kupata faida tena
ya haraka.
Na aina nyengine ni vile vya kijamii
(community media) ambavyo zaidi vinafanyakazi kwa ajili ya kutoa elimu ya jumla
katika eneo makhsusi ambapo vyombo hivyo vipo.
Bajeti ya uendeshaji wake hutegemea mchango wa wanajamii wenyewe, ruzuku
na misaada kutoka taasisi mbalimbali ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Aina zote za vyombo vya habari
tulizoeleza hapo juu zinahitaji waandishi mahiri na wenye uelewa wa malengo
halisi ya taasisi wanazozifanyia kazi ili kutimiza malengo yake. Hata hivyo,kwa vile uchaguzi ni suala la Kitaifa
linaloihusu jamii yote katika kufanikiwa kwake vyombo vyote vya habari
vinahitaji uelewa mpana wa masuala mbalimbali yanayohusu uchaguzi na taratibu
zake viwe vya Serikali, binafsi ama vya kijamii.
Kwa mfano; kuelewa sheria, maadili na
taratibu za uchaguzi, kujua manifesto na miongozo mbalimbali ya vyama vya siasa
kwenye uchaguzi, kufahamu michakato ya uchaguzi wa ndani ya vyama vya siasa,
upeo wa waandishi kutambua na kuchambua sifa za wagombea mbalimbali kwa nafasi
tofauti za uongozi na zaidi kuchambua na kutambua lipi jema na lipi baya yaani
kusoma alama za nyakati,lakini kubwa zaidi vyombo vyote lazima kuzingatia
maslahi ya waliowengi yaani umma.
Pia ni muhimu kwa wanahabari kuelewa
mazingira ya eneo wanalolifanyia kazi ikiwemo utamaduni wa jamii husika,
kusaidia jamii kwa kuielekeza katika mambo sahihi na yenye tija kwao na wala
sio kuwapotosha. Hatua hiyo itasaidia kupatikana jamii yenye uelewa mpana (informed
public) inayoweza kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi na kuondokana kuchagua
viongozi kwa kuzingatia misingi ya vyama vyao tu kama inavyofanyika hivi sasa
hapa Tanzania.
WAJIBU WA VYOMBO VYA HABARI NA MISINGI MIKUU YAUANDISHI
WA HABARI ZA UCHAGUZI
Uandishi wa habari ni taaluma iliyopo
kwa kuihudumia jamii, hivyo basi inahitaji waandishi wanaofahamu vyema wajibu,
misingi na mipaka ya majukumu yao ya kuitendaji na kitaaluma kwa kila siku. Kwa ujumla, vyombo vya habari vina wajibu wa
kuipasha habari nakuelimisha jamii juu ya masuala mbalimbali yanayotokea ndani
na nje ya nchi. Pia vijawajibika kuikosoa na kuelekeza jamii pale haja ya
kufanya hivyo inapotokea. Ni wao wanahabari wanaoweza kuisaidia jamii kwa
kuamsha ari ya mijadala yenye tija ili jamii hiyo iweze kuwa na maamuzi sahihi
pasipo kutumia tu hamasa na ushawishi wa wanasiasa hasa wanaolenga kupigania
maslahi yao binafsi ama ya vyama vyao na wakausahau umma.
Aidha,wakati Taifa la Tanzania likielea
katika uchaguzi, waandishi wa habari wanahitajika kubeba dhamana ya uwajibikaji
boratena uliotukuka kwa kutenda haki na kuwa wazi sana katika shughuli zao za
kila siku za kuipasha habari na kuelimisha jamii. Kwa ujumla, katika nyakati za
uchaguzi hasa, vyombo vya habari vina majukumu na wajibu ufuatao kwa jamii:
Ø K
uand Katika habari za uchaguzi kwa uwazi
na zilizotafitiwa kwa kina;
Ø Kuandika habari za uchaguzi kwa ukweli
na zinazoakisi matukio yakweli yaliyopo katika kila hatua ya mchakato wa
uchaguzi na athari yake katika jamii zaidi kuwepo sifa kwa waandishi ya kupima
jema na baya kwa wakati wote wanapotekeleza majukumu yao;
Ø
Kufuatilia taarifa za mara kwa mara
zinazotolewa na taasisi na mamlaka mbali mbali zinazosimamia masuala ya
uchaguzi;
Ø Kuchambua na kuaandika sifa halisi za
wagombea zinazoonsha uhalisia kwa uwezo wao;
Ø Vyombo kuwa tayari na pia kufanyakazi
ya kujitolea kwa maslahi ya umma
Ø Kupinga aina yoyote ya ubaguzi baina
ya jamii moja na nyengine ama viongozi
na wanaoongozwa.
Ø Kutumia vyanzo vya uhakika vya habari na kutoegemea upande
wowote;
Ø Kutoa nafasi sawa kwa wagombea wa
nafasi mbali mbali za uchaguzi na vyama vyao;
Ø Kuzifahamu kwa kina sheria na
taratibu zote za uchaguzi ili kuandika taarifa zisizokua na utata;
Ø Kujua dira za vyama na kwa kuaoanisha
na mambo muhimu yanayohitajika kimaendeleo katika taifa sambamba na kuifahamu Mipango
na Sera za vyama vinavyoshiriki katika uchaguzi sambamba na kupima uhalisia wa
sera hizo kimantiki kama ni kweli ama kufikirika;
Ø Kufahamu vyanzo vya mapato
yanayotumika katika shughuli za uchaguzi kwa vyama na wagombea wa nafasi mbalimbali.
VIASHIRIA VYA UVUNJIFU WA AMANI WAKATI WA UCHAGUZI
Mtakubaliana namikwamba, suala la
uchaguzi linahusisha wadau wengi na tofauti kabisa, lakini la muhimu katika
uchaguzi wowote duniani ni kuhakikisha kuwa kila upande unaohusika katika
uchaguzi hususan wananchi kupitia vyama vyao vya siasa vinapata haki yao katika
mchakato mzima wa uchaguzi huo tena bila kubaguliwa ama kudhulumiwa. Kinachohitajika
kuonekana kwa ujumla ni kuwepo kwa uchaguzi huru na wa haki (free and fair
election) unaotokana na utekelezaji wa misingi ya utawala bora na suala hili
lazima libaki kama utamaduni wa kawaida wa wanajamii yenyewe katika kuwapata
viongozi wa ngazi mbalimbali kwa njia ya kura na hata uteuzi kupitia mamlaka za
nchi.
Kuwepo dalili na viashiria vya kuleta
wasiwasi wa kutotendewa haki ama kudhulumiwa na taasisi zinazosimamia uchaguzi
ama mamlaka nyenginezo za nchiau zile zote zinazohusika kwa njia moja au
nyengine katika kufanikisha uchaguzi, mara nyingi huwa ni chanzo cha uvunjifu
wa amani. Kwa vile mchakato wa uchaguzi
unahusisha pande nyingi,viashiria vya uvunjifu wa amani unaoweza kuviona,
kuvianisha ama kusababishwa na vyanzo vifuatavyo:
(a) Wanasiasa wenyewe
Hawa ni wadau muhimu sana katika
kufanikisha uchaguzi uliohuru na wahaki. Wanapaswa kuwaelimisha kizalendo wafuasi
wao ili waelewe kwamba uchaguzi ni ushindani na kuna kushinda na kushindwa kama
ilivyo michozo mengine ya aina mbalimbali ingawa wanapaswa kuwahamasisha
wasipoteze nafasi kwa kutopuuza kushiriki katika kupiga kura lakini wanapaswa
wawaase katika mambo yote yanayoashiria uvunjifu wa amani ya nchi kwa lugha
nyengine watu wote lazima washiriki kulinda na kuhifadhi amani ya nchi .
Viashiria vya uvunjifu wa amani
kupitia kwa wanasiasa huweza kujitokeza katika mambo yafuatayo:
§ Kutoa kauli ambazo zinaweza
kuwachochea wananchi kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani (hate speech) kama
vile kuvamia maeneo au mali za serikali na watu binafsi kwa hasira;
§ Kufanya kampeni ambazo zinawapaka
matope wagombea wa nafasi za uchaguzi wa vyama vyengine;
§ Kukiukwa kwa maadili na taratibu za
uchaguzi kwa makusudi;
§ Kuandaa vikundi vya kuhamasisha fujo
kwenye masuala mbali mbali ya uchaguzi kwa njia ya dhahiri ama kwa siri;
§ Kupanga mipango na hila za wizi wa
kura na kuandaa mipango ya dhulma ya upigaji kura wa mtu mmoja zaidi ya mara
moja;
§ Kuhitaji ushindi wa lazima.
(b) Wananchi wa Kawaida
§ Uhuru wa kujieleza na haki ya
kujikusanya (freedom of expression and right to associate). Kifungu cha 18
(1-2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kinatoa haki ya mtu kutafuta,
kupokea na kutoahabari kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi. Kwa
kuzingatia msingi huo wa kisheria na kwa kuwa wananchi ni sehemu muhimu ya
kufanikisha uchaguzi huru na wa haki na kwa kuzingatia haki za msingi za
kibinadamu ni lazima haki hiyo ilindwe na wote na zaidi mamlaka za dola.Kufanya
kinyume chake ni kiashiria tosha cha uvunjifu wa amani kwani kitazuka
kisingizio cha wananchi kudai haki yao inayozuiliwa, kuporwa ama kupingwa na
watu wengine kwa sababu zao binafsi, mitazamo ya kivyama au kutokujua.
§ Haki ya kupiga kura (right to vote). Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Nam.11 ya mwaka
1984, Ibara ya 7 (1) na Katiba ya Zanzibar zinatoa haki ya kila moja
aliyetimiza miaka 18kuwa mpiga kura, lakini haki kwanza ni ya kuandikishwa kuwa
mpiga kura. Hivyo ni wazi kuwa kila raia ana haki ya kupiga kura iwapo tu
atatimiza masharti yaliyowekwa kisheria na tena sheria hizo zisiwe na mbinu za
hila za kuwakandamiza wengine. Hata
hivyo, nchi nyingi za Afrika ikiwemo hapa kwetu wakati mwengine hujitokeza
mazingira ambayo yanatia mashaka juu ya uhalali wa baadhi ya wananchi kunyimwa
haki yao ya kupiga kura. Jambo hili
ambalo wakati mwengine huanzia katika hatua ya uandikishaji wa wapiga kura hasa
kwa masheha, linazusha hasira kwa wananchi ambao wanaamini kuwa wananyimwahaki
yao wanayostahiki kuwanayo. Kuongezeka
kwa vitendo kama hivi kunaashiria kuvunjika kwa amani kama ilivyotokezea mara
kadhaa katika historia ya chaguzi za Zanzibar.
§ Haki ya kukosoa. Wananchi wanapaswa kupewa haki ya
kukosoa taasisi yoyote ma kiongozi inayoonekana kuelekea au kutokutenda
haki. Kuwabana wananchi na hivyo kukosa
sehemu ya kutolea kero na dukuduku lao na kupata suluhisho la matatizo waliyonayo
kwa njia ya mazungumzo na hatimae kutasababisha uvunjifu wa amani. Wananchi
wasiposikilizwa na kupewa nafasi ya kujieleza kwa kuwepo mijadala ya wazi
kuelezea kero na mahitaji yao kwenye mambo mbalimbali yanayowatatiza, wanaweza
kuibua mbinu ya kutumia hila na wakati mwengine hata nguvu ya kutafuta haki
wanayoamini ipo lakini inazuiwa.
(c) Taasisi Zinazosimamia Uchaguzi
ikiwemo Tume ya Uchaguzi
§ Vyombo vilivyopewa mamlaka kisheria
kusimamia suala la uchaguzi ikiwemo Tume yenyewe ya Uchaguzi na pia baadhi ya
taasisi za Serikali ambayo ndio dola inayopaswa zaidi kuchunga amani ya nchi, polisi,
mahakama na hata vyama vya siasa
vyenyewe kwa mfumo wa Tanzania zinahusika katika kusimamia uchaguzi wa huru na
wa haki. Ufanyaji kaziwa taasisi hizo unaweza kuwa ima ni sababu ya kuwepo
amani au uvunjifu wa amani. Kinachohitajika ni kufanyakazi kizalendo zaidi.
Kwa mfano Sheha ni wakala
wa Tume ya Uchaguzi katika kufanikisha zoezi zima la uandikishaji wa wapiga
kura. Sheha anapaswa kumfahamu mwananchi anaeishi katika eneo lake na ambaye
anastahiki au la kupiga kura kwa mujibu wa sheria zilizopo. Kinachojitokeza
mara nyingi ni kuwa wananchi wanawalalamikia kukosa haki yao wakiwalalamikia
masheha wao kwa kisingizio cha kutotimiza sifa za ukaazi ambapo watendaji hao wanaelezwa
hutumia madai ya kutowatambua na hivyo kuwakosesha haki yao wanayostahiki
kuwanayo. Jambo hili pia limetengeneza
mazingira ya chuki na kutoaminiana baina ya wananchi na masheha ambao wanadai
kukoseshwa haki yao kwa kudhamiria.Katika hili baadhi ya wananchi na vyama vya
siasa wanatafsiri kwamba ni hila za makusudi za upendeleo ambapo wanajenga
mazingira fulani ya kukipa ushindi chama wanachokiamini wao.
Tumeshuhudia mara kadhaa
jambo hili likizusha mizizozo na mivutano mikubwa baina ya viongozi hawa na
wananchi,na dola kuingilia kati kiasi kwamba baadhi ya maeneo wananchi
hawanaimani kabisa na masheha kwa sababu hawako wazi katika uendedaji wa
shughuli zao na pia mara nyingi wananchi wanaamini hawatendewi haki na
wanadhulumiwa na masheha hao.
Mfano mwengine ni pale
vyombo vya dola kama polisi ama taasisi nyengine za ulinzi na mahakama
vinapoonekana vinakadamiza kwa hila haki za kisiasa za wananchi kwa kutumia
isivyo halali mamlaka na madaraka ya dola waliyopewa, lakini kuonesha sura ya
utetezi wa wazi kwa chama fulani na kukandamiza chengine. Jambo hili ni wazi
huleta manung’uniko ya chini kwa chini na baadaye bayana na hivyo kuwepo chuki
baina ya pande mbili hizo jambo ambalo linapoendelea kuwepo ni kiashiria tosha
cha uvunjifu wa amani. Wananchi wanatakiwa kuamini kwamba, polisi na mahakama na
vyombo vyengine vya kiulinzi kwamba ndio kimbilio lao sahihi na la kweli la
kudai haki zao, lakini katika vyombo hivyo inapotokea zinakandamiza huwepo
uhasama mkubwa na chuki zisizo mipaka na hivyo kujenga uadui wa sio tu kwa
wananchi kuchukia mahakama na polisi na taasisi nyengine za ulinzi, lakini
huvichukia takrbani vyombo vyote vya dola na watendaji wake.
(d) Kuwepo
sheria kandamizi zinazolinda ama kuviza maslahi ya wengine
Kama tunavyojua kwamba
sheria ni utaratibu uliowekwa jamii ama dola na baadaye kukubaliwa jamii hiyo ama
dola kusimamia utekelezaji jambo makhsusi kwa maslahi ya wote. Lakini
inapotokea kuwepo sheria za uchaguzi ambazo zinakandamiza na kuviza haki za
wengine huku zikitoa upendeleo wa wazi kwa kundi fulani jambo hili bila shaka
halikubaliki na linakuwa ni chanzo kikubwa cha uvunjifu wa amani.
Sheria inayogusa
maslahi ya watu inatakiwa ichunge haki ya kila mmoja na wala sio kutoa
upendeleo kwa upande mmoja na kuukandamiza mwengine. Mifano ya jambo hili ipo
mingi katika nchi tofauti duniani ikiwemo Afrika na kwengineko duniani ambapo
athari zake zinaendelea kubakia kama ni kumbukumbu za vitabuni ambazo zimeumiza
waliowengi na kuleta machafuko ya nchi.
Dola inapotengeneza sheria za upendeleo
na ukandamizaji wa wazi na polisi na taasisi nyengine za kiulinzi kutumia nguvu
kupita kiasi za kukandamiza haki za watu wengine kwa kisingizio cha kusimamia
sheria za aina hiyo bila shaka wananchi wanaweza kuwa na kikomo cha kuvumilia kile
wanachokiita uonevu, ukandamizaji, mateso, masimango na manyanyasoya ndani ya
nchi yao kutoka kwa wasimamizi wa sheria ama wenye mamlaka. Inapotokea hali kama hiyo, baadhi ya wananchi,
wanasiasa na viongozi wanakosa uvumilivu na wanaweza kuchukua sheria mikononi
mwao wakidai wanatafuta ama kutetea haki.
(e) Vyombo vya Habari
Kama tujuavyo vyombo vya habari
vinatakiwa kuwa huru na kufanya ama kutekeleza majukumu yake bila upendeleo na
kuukandamiza ama kuumiza upande mwengine na huu ndio msingi wa maadili ya kazi
za wanahabari.
Mtakubaliana nami kwamba kutokana na
unyeti wa shughuli za uchaguzi, kipindi
cha uchaguzi waandishi wa habari wanatakiwa kuongeza umakini maradufu katika utendaji wao kazi ili kusaidia jamii na
Taifa kwa jumla kuchunga na kulinda na kuihifadhi amani ya nchi isitetereke.
Inapotokea waandishi wanaandika habari za upande mmoja kupendelea na
kuukandamiza mwengine, hawatoi nafasi kwa upande wa pili kutoa na kusikilizwa
maoni yao, jambo hili ni baya na ni kiashiria tosha cha uvunjifu wa amani ya
nchi. Wananchi wanavipenda na kuviamini sana vyombo vya habari pale
wanapojitahidi kufanya kazi zao kwa umakini, uwazi na tena bila kuegemea upande
wowote.
Mfano tunashuhudia hapa Zanzibar baadhi ya wanasiasa uchwara
wanapopanda majukwaani hawana hata neno moja lakisera ama mipango ya chama,wanapohutubia
kwenye hutuba yao ni matusi, vijembe na kejeli zinazoelekezwa kwa watu binafsi na
maneno ya namna hiyo waandishi wanapoyachukua moja kwa moja kuyaripoti kwa
wananchi kupitia vyombo vyao vya habari ni dhahiri kwamba panatengenezwa hali
tete ambayo athari zake ni kubwa kwa jamii.
Hivyo, vyombo vya habari vinatakiwa
vibebe pia wajibu wa kuunganisha jamii na wala sio kuifarakanisha kwa sababu tu
ya kutumiliwa na vyombo, vyama ama watu fulani kwa maslahi yao. Jambo la namna
hii ni bayasana na linapotokea mbali na kwamba vyombo huwa vimevunja maadili ya
taaluma yao, lakini piani chachu kubwa ya viashiria vya kuwepo amani inayoweza
kutetereka. Kama ulivyo msingi muhimu wa kisheria watu wanatakiwa watumie na
waipate haki yao ya kujieleza kwa uhuru
kabisa lakini vyombo vya habari
vinapotumika kukandamiza uhuru huo, yaani kumwita mtu mmoja akazungumza peke
yake na akaonesha watu binafsi vidole huku upande mwengine haupati nafasi kama
hiyo bila shaka hapo haki huwa haitendeki na pasipo haki sote tunajua kwamba na
amani hutoweka.
Jambo moja la hivi sasa hapa Tanzania,
tayari kuna mtindo wa kuiga nchi za magharibi katika kipindi cha uchaguzi,
kwani vipo vyombo na waandishi kuonekana wazi wazi kuwa chombo fulani kinaamua
kupigia debe chama fulani.
Jambo hili la kufuata mwelekeo wa kimagharibi ni
mapema mno kwa nchi kama Tanzania ambapo watu wake, wanasiasa, na viongozi wengine
hawajakomaa kidemokrasia kwani kwa
matamshi yao unaweza kuamini kwamba vipo vikundi kwenye nchi hii vinavyoamini
kwamba wao ndio wenye haki pekee ya kutumia rasilimali za Taifa bila kujali
wengine sasa unapoamua kumuunga mkono mtu wa namna hii ukasahau maslahi ya
waliowengi maanayake ni dhahiri unatengeneza chuki kwa wengine na ni kiashiria
tosha cha uvunjifu wa amani.
Itambulike kwamba hata utamaduni wa kuvumiliana
bado ni mdogo sana kwa siasa za Tanzania kwani matamshi yanayojitokeza ni
kwamba aliyepo madarakani hataki kuondoka na aliyenje anahisi ananyimwa haki ambayo
waandishi hawapaswi kamwe kulimwagilia maji jambo hili kwa kuwa linaweza
kuteteresha amani.
Mapendekezo
Baada ya mjadala huu uliojaribu
kuanisha mambo mbali mbali ambayo yanaweza kuashiria uvunjifu wa amani wakati
wa uchaguzi, yafuatayo yanapendekezwa yazingatiwe sana na waandishi hasa wakati
wa uchaguzi.
Ø Kwanza kufanya kazi kwa kuzingatia
utaalamu na maadili ya kazi zao;
Ø Kutokubali kutumiwa na wanasiasa na
wao kugeuzwa kama daraja la watu wengine kutafuta madaraka ya dola;
Ø Vyombo vya habari lazima visaidie
kulinda ama kutoteteresha amani sio tu wakati wa uchaguzi lakini wakati wote;
Ø Tusioneshe hisia za ufuasi wa vyama
ama kumpenda mtu moja kwa moja wakati wa kutekeleza wajibu wetu wa kazi;
Ø Tujaribu sana kuwaonesha wananchi
wagombea wanaofaa badala ya kukweza zaidi watafuta fedha kwa njia ya madaraka
ya umma;
Ø Tusiogope changamoto katika kazi la
muhimu zaidi ni kuzitambua kwa kuwa unapozitambua inaweza kuwa sababu ya
kuzitafutia ufumbuzi.
Hitimisho
Mjadala huu bila shaka umegusia mambo
mengi muhimu na zaidi kazi kubwa walionayo waandishi wa habari hasa wakati
taifa likielekea kwenye uchaguzi wa viongozi wa ngazi mbalimbali. Kwa msingi wa
kusaidia Taifa, vyombo vya habari lazima viwe chachu ya kuchapuza kasi ya
maendeleo ya Taifa kwa kutekeleza dhana ile ya kwamba wanahabari ni muhimili
wanne wa dola ijapokuwa haupo rasmi. Katika kutimiza hayo ni lazima viwajibike
kwa mujibu wa utaalamu wao, maadili ya kazi yao, lakini pia kuangalia maslahi ya
taifa lao.
Ikumbukwe kwamba waandishi makini wanaweza kusogeza mbele maendeleo
ya Taifa lao na kamwe hawatatumiliwa kama daraja la kukweza wengine katika
madaraka ya kisiasa na ama kusaka tonge kwa kuwaumiza wengine jambo hili
likifanywa na waandishi litakuwa ni dhambi kubwa itakapotokea inaweza kuleta
madhara makubwa.
Aidha, inapaswa wanahabari watambue
na waamini kwamba wao ni watu muhimu mno katika jamii na madhara ya kalamu zao kuzitumia
vibaya yanapotokea kamwe hayachagui kwamba mimi ni mwandishi, mtangazaji ama mpiga
picha niliyekuwa nikipendelea upande mmoja, lakini janga la madhara hayo yatamkumba
kila mmoja ndani ya jamii na mwanahabari ni sehemu ya jamii hiyo.
Ni kawaida taratibu za nchi nyingi
duniani hakuna mtu yoyote aliye juu ya Sheria na mara nyingi wanasheria
wanatwambia kwamba makosa ya kusababisha mtu kunyimwa au kudhulumiwa haki yake
hayana mwisho wake wa kudaiwa na unaweza kukaa miaka 50 ama 100 wajukuu wakadai
haki kwa niaba ya familia.
Hivyo ni vyema sote tuchunge haki zetu na za wengine
wala tusikubali kutumika kisiasa kwa sababu tu ya maslahi ya mtu, kundi ama
chama na tukasahau maslahi makubwa ya jamii na Taifa kwa jumla. Ni lazima
kufanya kazi za kuandika habari za uchaguzi kwa uadilifu, uweledi na umahiri
kubwa na kubwa zaidi uzalendo kuweka mbele jambo ambalolinalopaswa kuzingatiwa
na kila mmoja wetu.
Hatua hiyo itajenga Taifa la viongozi wawajibikaji
wanaotokana na jamii ya watu makini ambao huwachagua kwa njia ya kura baada ya
kuelimishwa vya kutosha na wanahabari.
Naomba kuwasilisha.
MAREJEO
·
Alexander
A.J (2003), Taking Sides Clashing Views on Controversial issues in Mass Media.
Dushikin Publishing Group, USA.
·
Ayubu
Rioba& Fiili Karashani (2002), Write or not to write Ethical concern in
Journalism.
·
John.
C. (1998), Studing Media, Problem of theory and Method, Mc. Graw Hill, USA.
·
Baraza
la Habari Tanzania, (2009), Kupasha habari za Uchaguzi, Ecoprint Ltd. Dar es
Salaam, Tanzania.
·
Katiba
ya Zanzibar (1984), Toleo la 2010.
·
Tume
ya Uchaguzi Zanzibar, (2011), Ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2010
·
Media
Council of Tanzania,(2005) professional code of Ethics
for Journalists, Ecoprint Ltd, Dar es Salaam, Tanzania.
·
UNICEF
(2003),Haki za Binadamu, Nyaraka za msingi.Runjiv Kapur
Kama kumbukumbu zangu bado ziko vizuri basi hicho kifungu cha 19 cha Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu ni la mwaka 1948 na wala sio 1946; mwaka uliotajwa hakukuwa na Azimio la aina hiyo.
ReplyDeleteVinginevyo hili ni somo zuri sana na mwandishi wake amejitahidi kuchimba kwa madhumuni ya kuisaidia jamii.
Ila kamwe tusitegemee mafanikio ya kilichowasilishwa kwa vile wengi wa waandishi wenye majina bado hawajapata skuli inayohusiana na uandishi wa habari yaani bado wengi ni makanjanja hivyo wamekosa maadili.
Kama ulivosema ndugu mwandishi, Uandishi wa habari ni fani ambayo ni lazima isomewe ili kufahamu misingi ya ufanywaji wake. Na msingi mkuu ni ukweli na tena mwandishi asiegemee upande mmoja!! Ni ajabu leo hii eti kuna waandishi wanasiasa, kuna uadilifu hapo?
Hongera kwa kazi nzuri