Na Abdulla Ali-Maelezo Zanzibar
Naibu
Waziri wa Mambo ya Nchi za nje wa Marekani anaeshuhulikia masuala ya Usalama wa
Raia, Demokrasia na haki za Binadam Bi. Sarah Sawell akizungumza na wandishi wa
habari (hawapo pichani) alipofika katika kituo cha Vijana muembe madema Mjini
Zanzibar.
Serikali ya Marekani imeamua kuwatembelea Vijana wa Bara la Afrika kwa
lengo la kukaa nao pamoja na kuzungumza nao juu ya Changamoto na Matatizo yanayowakabili
vijana hao.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani anaeshughulikia
masuala ya Usalama wa Raia, Demokrasia na Haki za Binadamu Bi. Sarah Sewall wakati
akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi ya Kituo cha Vijana iliyopo nyuma
ya Kituo cha Polisi Madema, Wilaya ya Mjini Unguja.
Amesema vijana wanakabiliwa na matatizo mengi kwa sasa yanayowafanya
kukata kabisa tamaa ya maisha na badala yake kujiingiza katika vitendo viovu
ikiwemo utumiaji wa madawa ya kulevya, wizi, ujambazi na wengine kuweza kutumiwa
na makundi maovu yasiyo na tija kwao.
Aidha amesema kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana ndio tatizo kubwa zaidi
duniani jambo ambalo lilimfanya Rais wa Marekani Barack Obama wiki 3 zilizopita
kuitisha mkutano wa pamoja wa Dunia ili kujadili masuala ya vijana ambapo Taasisi
Mbalimbali za Kiserikali na Binafsi Duniani zilishiriki katika mkutano huo.
Amefahamisha kuwa lengo la ziara yake barani afrika ni kuyaendeleza kwa
kuyafikisha kwa vijana yale yote yaliyojadiliwa katika mkutano huo ili kuwaonesha
njia ya mafanikio vijana hao pamoja na kuwapa msaada pindi utakapohitajika.
Akizungumzia kuhusiana na mauaji ya Watu Wenye Ulemavu wa Ngozi (Albino)
nchini Tanzania amesema Serikali
yake imeshachukua hatua mbalimbali katika kulinda haki za binadamu duniani kote
kwa kuwapatia ulinzi na usalama wakiwemo hao albino ila juhudi zaidi za
kuwalinda zinatakiwa kufanywa na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha kuwa
albino wanakuwa katika usalama zaidi.
Akigusia kuhusu mchakato wa
uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu nchini Tanzania amesema Serikali ya Marekani
imekuwa ikitoa msaada mkubwa kwa Serikali ya Tanzania wakati wa uchaguzi hivyo
itaendeleza na jitihada hizo ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa katika hali ya
usalama na amani na kuepukana na vurugu zisizo za lazima.
Nae Mwenyekiti Mtendaji wa Vituo vya Vijana Tanzania Nd. Abdalla Miraji
Othman amesema vituo vyao kwa sasa vinakabiliwa na Changamoto nyingi ikiwemo
usafiri pamoja na posho na mishahara kwa wafanyakazi wa vituo hivyo kwani huwa
havitolewi kwa wakati jambo ambalo linarejesha nyuma kwa kiasi kikubwa jitihada
zao za kuwaokoa vijana kutokana na vitendo viovu.
Akitoa wito wake Nd. Othman amesema ipo haja kwa Benki za Kitanzania kupunguza
masharti ya kutoa mikopo pamoja na Riba ili vijana wamudu kuchukua mikopo katika
Benki hizo kwa lengo la kujiajiri na hatimae kujikomboa kimaisha.
Amesema Ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani anaeshughulikia
masuala ya Usalama wa Raia, Demokrasia na Haki za Binadamu Bi. Sarah Sewall ilikua
ni ya Siku 1 Visiwani Zanzibar ambapo ziara hiyo inatrajiwa kufanyika takriban
bara lote la Afrika kwa lengo la kukutana na vijana na kuzungumza nao juu ya
masuala mbalimbali.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO- ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment