Habari za Punde

Maalim Seif asifu mchango wa Oman kusaidia Elimu, ataka tujifunze kwa India

Na: Hassan Hamad, OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesifu mchango unaotolewa na serikali ya Oman katika kuiendeleza Zanzibar kwenye sekta mbali mbali ikiwemo sekta ya elimu.

Akizungumza na balozi mdogo wa Oman sheikh Ali Al-Rashdi ofisini kwake Migombani, Maalim Seif amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini mchango huo ambao unalenga kuwaongezea ujuzi wananchi wa Zanzibar.

Amefahamisha kuwa Serikali ya Oman imekuwa kigezo kizuri cha utoaji wa elimu kwa Zanzibar, kwani imekuwa ikitoa nafasi za masomo “scholarships’ kwa njia ya mtandao, jambo ambalo linatoa fursa sawa kwa kila mwenye sifa za kuomba nafasi hizo, na kuondokana na dhana ya kuwepo upendeleo katika upatikanaji wa fursa za elimu nchini.

Amesema nafasi za masomo zinazotolewa kupitia mfuko wa elimu wa Sultan Qaboos wa Oman, zimekuwa zikiwasaidia vijana wa Zanzibar kuongeza ujuzi katika fani mbali mbali, hatua ambayo itarahisisha maendeleo ya nchi.

Sambamba na hilo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameelezea kuridhishwa na jinsi Oman inavyofanya juhudi za kukijengea uwezo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), na kwamba itakifanya chuo kicho kiweze kutoa elimu bora zaidi.


Aidha Maalim Seif ameishukuru Oman kwa kuiendeleza na kuikuza lugha ya Kiswahili, na kuongeza kuwa Oman imekuwa miongoni mwa nchi za kigeni zinazozungumza zaidi lugha hiyo ya Taifa ya Tanzania.

Kwa upande wake balozi mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Sheikh Ali Al-Rashdi amemueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa Serikali ya Oman imekuwa ikitoa misaada hiyo kwa Zanzibar, ikielewa kwamba inatekeleza wajibu wake kwa ndugu zao wa Zanzibar wenye historia ndefu.

Amesema Oman na Zanzibar zina uhusiano  wa kindugu wa muda mrefu, jambo ambalo linaifanya nchi hiyo kuendelea kuwa karibu na Zanzibar, na kutaka uhusiano huo uimarishwe zaidi.

Ameeleza kuwa Oman inakusudia kujenga taasisi kubwa ya elimu itakayotoa taaluma mbali mbali zikiwemo za dini na sayansi katika eneo la Tunguu, baada ya kukamilika ujenzi wa msikiti mkubwa unaoendelea katika chuo cha Kiislamu Mazizini.

Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amekutana na balozi mdogo wa India aliyepo Zanzibar balozi Satendar Kumar, na kueleza kuwa Zanzibar inayo mambo mengi ya kujifunza kutokana na uzoefu wa India
.
Ametaja mambo hayo kuwa ni pamoja na mawasiliano ya habari (ICT) pamoja na maeneleo ya sekta ya afya.

Amesema India imepiga hatua kubwa katika maeneo hayo, na kwamba itashirikiana na nchi hiyo katika kuhakikisha kuwa vijana wa Zanzibar wanapata utaalamu wa kutosha na kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.

Ameishauri India ambayo imekuwa miongoni mwa nchi tatu zinazowekeza zaidi nchini, kuendelea kuweka vitega uchumi vyao ambavyo vinasaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

Aidha ameishauri nchi hiyo kuangalia uwezekano wa kushirikiana na Zanzibar katika kuvifufua viwanda vilivyopo nchini, ili viweze kufanya kazi.
Naye balozi Satendar Kumar amemuhakikishia Makamu wa Kwanza wa Rais kuwa India itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika maeneo mbali mbali ikiwa ni pamoja na kukuza biashara pamoja na kuendeleza miradi iliyoanzishwa na nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.