Habari za Punde

Uchunguzi: Walimu kwenda masomoni kwa wakati mmoja kumechangia uhaba wa Walimu Pemba

Na Haji Nassor, PEMBA
TATIZO la uhaba wa waalimu kisiwani Pemba, limeripotiwa kusababishwa na kadhia mbali mbali, moja wapo ni ile ya waalimu 510 kuweko masomoni kwenye vyuo tofauti, kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka huu, huku wilaya ya Wete ikiongoza kwa kuwaruhusu waalimu 155.
Hali hiyo imebainika kuwa, sasa kisiwa cha Pemba chenye wilaya nne, kimebakiwa na waalimu 3,014 walioko madarasani, kati ya idadi ya waalimu wote 3, 524 ambapo kati ya hao, walimu wanawake ni 1,839 na wanaume 1,685.
Wilaya nyengine inayoongoza kwa kukumbwa na uhaba wa waalimu kwa kuweko masomoni, ni wilaya ya Chake Chake ambayo imeruhusu waalimu 129, ikifuatiwa na wilaya ya Mkoani 121, ambayo ilishika nafasi ya mwisho kitaifa, kwenye mitihani ya darasa la kumi na darasa kumi na mbili mwaka 2014/2015.
Wilaya ya Micheweni mkoa wa kaskazini Pemba, yenyewe imeruhusu waalimu 105 kwenda masomoni, ambapo kati ya hao waalimu wanawake ni 58 na waalimu wanaume 47.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi, umebaini kuwa, waalimu wanawake walio mosomoni kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka huu wa 2015, ni 285, ambapo wilaya ya Wete pekee inawalimu 84, ikifuatiwa na wilaya ya Chake chake yenye waalimu wa kike 76.
Wilaya ya Mkoani walimu wanawake walioko masomoni ni 67, Micheweni 58, ambapo waalimu wanaume ambao hawako madarasani kwa kuweko masomoni ni 225, huku wilaya ya Wete ikiwa na waalimu 71, ikifuatiwa na Mkoani 54, Chake chake 53 na wilaya ya Micheweni 47.

Hivi karibuni afisa elimu na mafunzo ya amali wilaya ya Mkoani Seif Mohamed Seif, alipotakiwa kujibu shutuma za wizara hiyo kuwa na uhaba wa waalimu na kusababisha wilaya ya mkoani kufanya vibaya kwenye mitihani ya taifa, alisema hilo limesababishwa na waalimu wengi kwenda masomoni kwa wakati mmoja.
Alisema wamekuwa wakizuia ruhusa za waalimu wengi kwenda masomoni kwa wakati mmoja, ingawa hata baadhi ya wazazi na walezi, wamekuwa wakishilikilia kumuombea ruhusa mwanawe ili aende kuongeza elimu.
“Mzazi anakujia kwamba lazima mwanawe umsaidie aende chuoni, maana amepata ufadhili na akihoji kwamba mbona wengine wameruhusiwa na kisha kunapelekea uhaba wa waalimu’’,alisema.
Afisa mdhamini wa wizara hiyo Pemba, mwalimu Salim Kitwana Sururu, alikiri kwamba kuna kundi kubwa la waalimu walioko masomoni, ingawa wamekuwa wakishindwa kuwazuia kutokana na wengi wao wamekuwa wajikisomesha wenyewe.
“Wanaokwenda masomoni baada ya muda wanarudi, lakini mimi nasumbuliwa na wale wanaochukua uhamisho kwa kudumu, baada ya kuolewa, na wengi wao wapo mkoa wa mjini Magharibi Unguja’’, alifafanua.
Hivyo amewataka wazazi na walezi waelewe hasara iliopo kisiwani Pemba, licha ya wizara kujitahidi kuajiri waalimu kila muda, ingawa tatizo ni wale wanaomba uhamisho muda mfupi baada ya kuolewa kisiwani Unguja.
Afisa elimu wilaya ya Micheweni Mbwana Shaame Hamad, alisema kama wengeamua kuwazuia waalimu hao kwenda masomoni, ni dhahiri kwamba dunia ingewaacha nyuma kielimu.
‘’Sasa mwalimu ameshapata fursa ya kwenda kuongeza elimu na tayari anamfadhili wake umzuie, ni bora akaongeze elimu maana dunia inakwenda mbio kitaaluma’’, alifafanua.
Kwa upande wake Afisa elimu wilaya ya Wete Khamis Hamad Said alisema, kila mwalimu anaekwenda masomoni, analewa kwa kina kwamba, amewaacha wanafunzi wakiwa na uhaba wa waalimu.
Akijibu suali na mwakilishi wa Jimbo Wawi katika ukumbi wa baraza la wawakilishi hivi karibuni, Naibu waziri wa elimu na mafunzo ya amali Zanzibar Mhe: Zahra Ali Hamad, alikiri kuwa skuli nyingi kadhaa,  zinaupungufu mkubwa wa walimu na hasa kwa masomo sayansi.

Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imekuwa ikitumia mbinu mbali mbali katika kuongeza idadi ya walimu wa masomo ya Sayansi na Hesabati, ikiwemo kuomba msaada wa walimu wa kujitolea kutoka mataifa na mashirika ya kujitolea kutoka mataifa mbali mbali.

Baadhi ya nchi na mashirika yaliyojitokeza kusaidia ni pamoja na Shirika la VSO la Uingereza, Peace Corps la Marekeni, JICA la Japani, Koica la Korea na Serikali ya Nigeria kupitia “Technical Aids Corps” ambalo lilikubali kuleta walimu 14  kufundisha masomo hayo.

Hata hivyo Naibu waziri huyo wa elimu, alieleza kuwa wizara inakusudia kutumia huduma za mtandao wa mawasiliano katika kusomeshea na kufundishia masomo mbalimbali, kwa kutumia  uwezo mkubwa wa mkongo wa taifa wa mawasiliano wa simu uliopo hapa Zanzibar.

Aidha alisema hadi hivi sasa, ni taasisi chache tu za elimu ndizo zilizounganishwa na mkongo wa taifa, ikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Chuo cha Kiislamu Mazizini, Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia na Skuli ya Sekondari ya Kiembe Samaki.

Baadhi ya wanafunzi wameishauri wizara ya elimu, kuwa na mpango maalumu wa kuwaruhusu waalimu kwenda masomoni, ili tatizo la uhaba wa waalimu lisiathiri mtiririko wa usomeshaji.

Hata hivyo wananfunzi hao, wametaka kuwepo kwa mkakati maalumu kwa waalimu wenye ajira mpya, wasikubaliwe uhamisho wao kutoka skuli moja kwenda nyengine, alau baada ya kutimiza miaka mitatu.

Mwalimu Ame Shaali wa skuli ya Michakaini, alisema waalimu kwenda wengi masomoni kwa wakati mmoja, hakusababishi tu uhaba wa waalimu, bali ni kuwapa mzigo mkubwa wa vipindi waliopo.

“Unajua suala la waalimu kuongeza elimu ni zuri, lakini wanapokwenda kwa kundi, hutubebesha mzigo wa vipindi sisi tuliopo madarasani, lazima kuwe na mpangilio mzuri ili pande zote zisiathirike’’,alifafanua.

Mzazi Asha Ali Makame wa Wete, alisema lazima wizara ya elimu, iwe na mipango mahasusi ya kuwaruhusu watendaji wake kwenda masomoni ili kusiathiri ufundishaji kwa wanafunzi.

Nae mdau wa elimu Khatib Juma, alisema lazima wizara ya elimu ijipange vyema, maana hata hao wanaokwenda masomoni wengi wao wanapomaliza hawarejei tena katika skuli walizoondokea.


Kwa mujibu wa hutuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya  fedha ya wizara ya elimu ya mwaka 2014/2015, mwaka 2013/2014 wizara  iliajiri walimu 235, ambapo kisiwa cha Pemba kilipata waalimu 125 na Unguja 110, huku ikitimiza idadi ya waalimu 12,756 wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.