Habari za Punde

DK Shein:Serikali Iko Pamoja na Wananchi Walioathirika na Mvua Zinazonyesha.

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                       05 Mei, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo ametembelea maeneo mbali mbali yaliyoathirika na mvua zinazoedelea kunyesha na kuwaahidi wananchi wa maeneo hayo kuwa Serikali itahakikisha inawapatia misaada wanayostahiki ili kuwawezesha kurejea katika maisha yao ya kawaida.
Katika ziara hiyo Dk. Shein alitembelea maeneo ya Kwahani, Mwanakwerekwe karibu na Skuli ya Mwanakwerekwe C, Bwawa la Mwanakwerekwe, Tomondo na Kisauni Mtaa wa Ziwa Maboga.
Katika maeneo yote hayo Mheshimiwa Rais Zanzibar aliwahakishia wananchi waliopatwa na maafa hayo kuwa Serikali itachukua hatua madhubuti na za haraka ili kuwapatia misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula na sehemu za kulala kwa wale watakaokuwa hawakubahatika kupata sehemu miongoni mwa ndugu na jamaa zao.
“Tumekuja kuona hali halisi ya maafa yaliyowakuta na Serikali yetu inachukua hatua madhubuti kuwasadia na kwanza kuwapatia makazi waliokosa kwa jamaa zao na pili kuwapatia msaada wa kukijikimu kipindi hiki cha shida hadi pale mtu atakapojiweza na kurudi katika maisha yake ya kawaida” Dk. Shein alieleza
Aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano walioutoa kwa wananchi wenzao waliopatwa na maafa hayo kwa kuwasaidia sehemu za kuishi kwa muda na hata misaada mingine.
Katika eneo la Kwahani ambako familia zaidi ya 200 zimeathirika huku nyumba 29 wakazi wake wakilazimika kuzihama, Dk. Shein amesema tatizo  la eneo hilo la kujaa maji ni la muda mrefu na kwa hatua za awali itabidi mtaro wa maji ya mvua wa eneo hilo upanuliwe na kuwataka wananchi kuacha kutupa uchafu katika mitaro kitendo ambacho kinasababisha mitaro kuziba na kusababisha maafa.
“Ni wajibu wetu kuangalia upya eneo hili la Kwahani na maeneo mengine kama haya ili kuyapatia ufumbuzi wa kudumu kuepuka madhara kama yaliyotokea hivi sasa” alieleza Dk. Shein
Aliongeza kuwa Serikali tayari inayo mpango maalum kuhusu eneo hilo la Kwahani ambapo alisema inafaa sasa kuja na mradi utakaolibadilisha eneo hilo kuwa kisasa.
Katika eneo la Mwanakwerekwe, Dk. Shein alishuhudia eneo lililozama ambapo shimo kubwa limetokeza na kuhatarisha usalama wa nyumba zilizojengwa katika eneo hilo pamoja na wakazi wake.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Dk. Khalid Salum Mohamed alieleza kuwa eneo hilo linahitaji kufanyiwa utafiti wa kina kwa kuwa miaka si mingi jirani na eneo hilo ardhi ilididimia na kutengeneza shimo kubwa kama ilivyotokea sasa.
Katika eneo la Tomondo Dk. Shein alitembelea wakazi wawili Bwana Ali Khamis Khamis na Bibi Mwanaisha Takrima Mohamed waliopatwa na madhara ambapo baadhi ya sehemu ya nyumba zao zimeharibiwa na mvua hizo ambako aliwataka wananchi kufanya subira kwani serikali iko pamoja nao.
Katika maelezo yake kwa Mheshimiwa Rais, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi Bwana Ayoub Mohamed Mahmoud alisema jumla ya nyumba 173 zimeathirika lakini nyumba nne zimeharibika vibaya haziwezi kukalika.
Huko Kisauni Mtaa wa Ziwa Maboga ambako sehemu ya ziwa hilo imevamiwa na wananchi maji yamejaa na kuingia katika makazi ya watu hivyo kusababisha wakazi wa nyumba 21 kuzihama.
Wakati huo huo Rais wa Zazibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezitaka mamlaka husika kuhakikisha wananchi waliovamia eneo la bwawa la Mwakwerekwe wanaondoka sehemu hiyo mara moja ili kuepusha maafa zaidi.
Alisisitiza kuwa wafanyabiashara wanaojaribu kulifukia ziwa hilo kwa kutupa taka ili kupata eneo la biashara hawana budi kuondoka kwani ujazaji huo kitaalamu haukubaliki na zaidi eneo hilo ni la kuhifadhia maji ya mvua.


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 


                                               

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.