Na Miza Othman / Rahma Khamis- Maelezo
Serikali imesema kupanda na kushuka kwa bei ya mafuta haiathiri usafiri wa Daladala wala vyombo vya Baharini na huduma za umeme pia imeathiri kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania kwa sarafu za kigeni.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee leo huko Chukwani katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akijibu suali la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Jaku Hashim Ayoub alipotaka kujuwa Serikali inatowa kauli gani kwa wananchi wake katika kupunguwa kwa bei za vitu kutokana na kupunguwa kwa bei ya mafuta Nchini.
Amesema kwamba bei ya mafuta duniani imepungua sambamba na thamani ya shilingi ya Tanzania kushuka bei jambo ambalo linapelekea hali duni ya mauzo ya soko la ndani na kutoleta tija kwa wananchi wa kawaida.
“Napenda pia kuliarifu Baraza lako tukufu kwa bei zilizopo sasa hasa za usafiri wa daladala zimekuwepo kwa muda mrefu hali hii inatokana na makubaliano kuwa bei zisipande kiholela kutokana na hali za watu”,alisema Waziri wa Fedha Omar Yussuf Mzee.
Ameeleza kuwa bei ya Umeme iliyopo hivi sasa ni chini ya gharama halisi ya uzalishaji, hivyo isingeweza kupunguza kwani hali hii ndio iliyopelekea isishuke wala isipande bei za huduma hizo kwa wakati huu.
Aidha amesema kuwa ipo haja kubwa kwa wananchi kuongeza uzalishaji hasa mazo ya chakula kwa ajili ya soko la Ndani na nje ya Nchi.
Hata hivyo Serikali itahakikisha kuendelea kutoa ruzuku kwa wakulima pamoja na pembejeo za kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa ndani sambamba na kutoa unafuu wa kodi hasa kwa bidhaa za vyakula vinavyoingiza kutoka nje ya Nchi ili wananchi waweze kupata bei mbalimbali za bidhaa hizo.
No comments:
Post a Comment