Na Abdulla Ali-Maelezo
Mvua za masika zinazoendelea kunyesha Visiwani Zanzibar zimesababisha
hasara kubwa ikiwemo upotevu mali na mifugo, uharibifu wa miundombinu pamoja na
kusababisha vifo vya watu.
Hayo yamweelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
Zanzibar Mhe. Mohamed Aboud Mohamed wakati akitoa taarifa kwa wananchi
kuhusiana na athari za mvua hizo katika ukumbi wa Karume House, Mjini Zanzibar.
Amesema mvua hizo zimesababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali
ya Mkoa wa Mjini Magharibi na kupelekea athari kubwa katika maeneo hayo ikiwemo
vifo vya watu, uharibifu wa nyumba za makaazi na upotevu wa mali na mifugo,
ambapo hadi sasa watu wawili (2) ambao ni Nd. Juma Hamad (25) mkaazi wa Mwanakwerekwe
na mtoto mmoja (1) mkaazi wa Kinuni anaekisiwa kuwa na miaka 8 wamepoteza maisha
wakiwa wote wawili ni kutoka Wilaya ya Magharibi Unguja.
Aidha Waziri Aboud amesema kuwa maiti ya mtoto imeshapatikana na
kuzikwa jana Tarehe 3/5/2015 na maiti ya Nd. Juma Hamad bado haijapatikana na
juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Amefahamisha kuwa maeneo yaliyoathirika zaidi na mvua hizo ni pamoja
na Magomeni, Jang’ombe, Nyerere, Sebleni, Sogea, Mwanakwerekwe, Welezo, Kisauni,
Tomondo, Mombasa, Kinuni, Mtopepo, Chumbuni, Kwahani, Mpendae, Bububu na Kwaalinato,
ambapo maeneo yote hayo yanapatikana ndani ya Mkoa wa Mijini Magharibi.
Ametanabahisha kuwa, kwa vile mvua bado zinaendelea kunyesha ni
vyema wananchi wakachukua tahadhari ili kujiepusha na athari zaidi zinazoweza
kujitokeza, ikiwemo wazazi kuangalia watoto wao na kuhakikisha hawachezi karibu
na maeneo yanayotuama maji, kwa wale wanaoishi mabondeni ni vyema wakahama
sehemu hizo.
Waziri Aboud pia amewataka wananchi waliochimba mashimo katika maeneo
ya makaazi wawe waangalifu kwa kuyafunika haraka iwezekanavyo , kuchemsha maji
wanayoyatumia, kuhifadhi chakula ili kuepukana na maradhi ya miripuko pamoja na
kufuata kanuni za afya ikiwemo usafi binafsi na maeneo yanayowazunguka.
Vilevile amewataka wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki
kigumu kwani Serikali itaendelea kushirikiana nao ili kuhakikisha kuwa hali ya
maisha kwa wananchi hao inarudi kama kawaida pamoja na kuwapa pole wale wote
waliopoteza jamaa na mali zao.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment