Habari za Punde

Balozi Seif Ajumuika na Wafanyakazi wa Ofisi Yake katika Chakula cha Usiku

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kuzungumza na Viongozi na watendaji wa Ofisi yake.
Balozi Seif akitoa nasaha zake mara baada ya kuwaandalia chakula cha usiku Viongozi na Watenmdaji wa Taasisi zilizochini ya Ofisi yake kufuatia kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara hiyo pamoja na kuagana baada ya kufanyakazi pamoja katika kipindi ya miaka mitano iliyopita.
Balozi Seif Ali wapili kutoka kushoto akijumuika pamoja na Viongozi na watendaji wa Ofisi yake kwenye tafrija aliyowaandalia baada ya kupita kwa Bajeti ya Wizara hiyo katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea.Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wqa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed, Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi Mh. Ali Mzee Ali, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mh. Hamza Hassan Juma, Mh. Makame Mshimba Mbarouk pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mh. Saleh Nassor Juma.
Baadhi ya Watendaji wa Taasisi zilizochini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wakijipatia mlo kwenye tafrija hiyo iliyofanyika katika Makazi ya Balozi Seif yaliyopo Mazizini nje kidogo ya M,ji wa Zanzibar.
Kikundi cha Muziki wa Morden Taarab cha Big Staa chenye mastakimu yake Ofisi ya Mkoa Mjini Amani kikitoa burdani kwenye tafrija ya kuwapongeza Viongozi na watendaji wa Taasisi zilizochini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar baada ya kupita kwa Bajeti ya Wizara hiyo pamoja na kuagana kwa kukaribia kukamilika kwa kipindi cha miaka mitano.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif Ali Iddi  aliyepo mwanzo kushoto akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Serikali Kushoto yake Mh. Hamza Hassan Juma na Mjumbe wa Kamati hiyo Mh. Makame  Mshimba Mabrouk  kwenye tafrija ya kuwapongeza watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.


Na Othman Khamis OMPR. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Watendaji wa Taasisi za Serikali wana wajibu wa kutumia vipaji walivyojaaliwa kuwa navyo katika kubuni mbinu na mikakati watakayohisi kwamba inaweza kutaleta faida na ufanisi katika maeneo yao ya kazi sambamba na Serikali  Kuu kwa jumla.

Alisema faida ya ubunifu watakaoutumia watendaji hao utaongeza kasi ya uwajibikaji endapo wataendelea kushikamana baina yao katika kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na nidhamu kwa kutumia vipaji hivyo.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa hafla maalum ya chakula cha usiku alichowaandalia watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi yake kufuatia kukamilisha  na hatimae kupita kwa Bajeti ya Wizara hiyo pamoja na kuagana baada ya kufanya kazi pamoja katika kipindi chote cha miaka mitano tokea mwaka 2010.

Hafla hiyo ya chakula cha usiku iliyofanyika katika Makaazi ya Balozi Seif Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ilijumuisha pia baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa Serikali, wafanyakazi wa Baraza hilo wakiwemo wawakilishi wa taasisi tofauti za ndani na nje ya nchi wanaofanya kazi pamoja na watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Balozi Seif aliwapongeza watendaji wa taasisi zote zilizo chini ya Ofisi yake kwa kufanya kazi nzuri katika utekelezaji wa majukumu yao likiwemo pia suala  la kutengeneza Bajeti na hatimae kupita bila ya vikwazo katika Kikao cha Bajeti cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea.

Alisema hatua hiyo imempa moyo na faraja kubwa iliyosababisha ndani ya kipindi cha miaka mitano cha uwepo wake katika Wizara hiyo kutokwaruzana au kumgomba Mfanyakazi ye yote kwa vile kila mmoja likuwa akijuwa wajibu wake.

“ Miaka mitano ya uwepo wangu ndani ya Ofisi hii sijawahi kumgomba Mfanyakazi hata mmoja ukiachia zile kasoro ndogo ndogo za kibinaadamu zisizoepukika. Hii inatokana na kila mtendaji kuelewa wajibu wake ipasavyo “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae ndie Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliwaasa Viongozi wa Taasisi hizo pamoja na nyengine  za umma kuwa na tahadhari wakati wanaposimamia haki za watendaji wao na kuepuka fitna na majungu ambazo hatimae huzaa chuki kati yao na watendaji hao.

Balozi Seif alisema wapo baadhi ya viongozi wanaokumbwa na kashfa na matatizo kutokana na vitendo wanavyowafanyia  watendaji  wa ngazi ya chini ambapo hutoa mwanya kwa  wafanyakazi wanaowaongoza  kufurahia wakati wanapohamishwa au kustaafu kazi.

“ Tumekuwa tukishuhudia mara kwa mara mikasa inayowakumba baadhi ya Viongozi wa Taasisi ambapo watendaji wao hufikia maamuzi ya kupika pilau au biriani wanapopata taarifa kwamba Bosi wao kastaafu au kuhamishwa na kupelekwa katika sehemu nyengine ya kazi “.Alitahadharisha Balozi Seif.

Aliuwakumbusha Viongozi hao kwa kushirikiana na watendaji wao kuendelea kupendana ili inapotokea kukutana tena baada ya kumaliza utumishi wao wakumbatiane kwa kuonyeshana upendo wao wa dhati.

Mapema Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohammed kwa niaba ya Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo amemshukuru na kumpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa kuwaongoza vyema watendaji hao katika utekelezaji wa majukumu yao.

Dr. Khalid alisema Uongozi  huo wa busara wa Balozi Seif Ali Iddi umesaidia kuleta ufanisi na kuiwezesha Ofisi hiyo inayoratibu shughuli  nzima za Serikali kufikia malengo iliyojipangia ya zaidi ya asilimia 90% katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Alifahamisha kwamba Watendaji wa Taasisi zote zinazofanyakazi chini  ya Ofisi hiyo wamefarajika na utendaji wa Kiongozi huyo pamoja na wale waliochini yake ulioonyesha upendo na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi wote.

Dr. Khalid alisema mshikamano huo wa pamoja kati ya viongozi na watendaji hao ndiyo chachu ya mafanikio yaliopelekea kuibua wafanyakazi bora wapatao 11 ndani ya Taasisi zilizo chini ya Ofisi hiyo jambo ambalo linastahiki kupongezwa na kuigwa na Taasisi nyengine za Umma hapa Nchini.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Serikali Mh. Hamza Hassan Juma alisema Utamaduni  wa kupongezana ulioanzishwa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar baada ya kazi ngumu wanazozifanya unafaa kuigwa na Taasisi nyengine hasa wakati watendaji wanapopata mafanikio makubwa.

Mh. Hamza alisema uratibu makini  uliokuwa ukisimmamiwa na watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar umesaidia kuleta mafanikio makubwa katika utendaji mzima wa Serikali.  

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Serikali ameipongeza Idara ya Maafa Zanzibar chini ya Mkurugenzi wake kwa juhudi zake za kutoa elimu kwa Umma iliyosaidia kupunguza majanga ya maafa wakati wa  mvua za masika zilizopita hivi karibuni.

Akimkaribisha Balozi  Balozi Seif kuzungumza na hadhara hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed amewashukuru na kuwapongeza Wajumbe wa Kamati  ya Kudumu ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Serikali kwa kusimamia vyema na uadilifu utendaji Mzima wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Waziri Aboud alisema usimamizi wa Kamti hiyo umeiwezesha Ofisi hiyo kuratibu vyema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 kwa zaidi ya asilimia 95% chini ya rasilmali iliyopo ya Taifa ya amani na utulivu inaoendelea kupatikana kutokana na umoja na mshikamano miongoni mwa Wananchi wote.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.