Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuanzisha Utalii wa Utamaduni wa Zanzibar ambao utakuwa ni kivutio kwa Wenyeji na Wageni mbalimbali nchini.
Hatua hiyo ni miongoni mwa jitihada mbali mbali zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha Sekta hiyo ambayo ndio tegemeo la Uchumi wa nchi.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji na Utumishi wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Joseph Kilangi wakati alipokuwa akifungua Semina ya majadiliano ya ‘Rasimu ya Sera ya Urithi wa Utamaduni’ iliyofanyika Forodhani Mjini Zanzibar.
Amesema Zanzibar ina utamaduni wake ambao unatofautiana na Nchi nyingine hivyo ipo haja ya Utamaduni huo kuenziwa na kufanywa uwe kivutio kwa Wageni ili waweze kuja nchini kwa ajili ya kujionea.
‘’Zanzibar tuna utamaduni wetu wa Asili ikiwemo Mavazi, Tabia njema, Ukarimu, kupendana,amani na utulivu,mambo ambayo tukiyaratibu vyema katika Sera hii itakuwa kivutio cha Utalii’’ Alisema Mkurugenzi Kilangi
Amewataka Washiriki wa Semina hiyo kuijadili vyema Rasimu hiyo na kutoa mapendekezo ya kuiboresha kwa lengo la kuvisaidia Vizazi vya sasa na Vijavyo.
Kwa upande wao Washiriki wa Semina hiyo wameipongeza Serikali kwa uamuzi wake na kuomba kufanyika kwa majadiliano mapana kutoka kwa Wadau mbali mbali hasa wa Vijijini ambao pia Sera hiyo inawahusu.
Awali Mwenyekiti wa Semina hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya Kale Dkt. Amina Ameir Issa amewaomba Wananchi kushirikiana na Serikali yao katika kuyahifadhi Maeneo ya Kihistoria ili kuwa chanzo cha Maendeleo kwa Taifa
Akielezea lengo la Sera hiyo amesema ni kuweka wigo wa pamoja baina ya Utamduni na Utalii ili kuona mambo hayo yanaendana bila ya kuathiriana.
Dkt Amina amefahamisha kuwa ili Sera ya Utalii wa Utamaduni itimie ni lazima Serikali kwa kushirikiana na Jamii ihakikishe inazihifadhi Mila na Silka za Zanzibar sambamba na kuhifadhi Makumbusho ambayo ni kielelezo tosha cha Utamaduni wa Zanzibar.
Dkt Amina amesema Idara yake ambayo ndio Waratibu wa Sera hiyo itashirikiana na Taasisi za Umma na Binafsi katika kuiboresha ili kutimiza lengo lililokusudiwa.
Mjadala huo utaendelea kwa siku mbili ambapo umewashirikisha Wadau kutoka Taasisi mbalimbali ikiwemo za Kibinafsi na Serikali kwa lengo la kuichangia Rasimu hiyo kabla ya kupelekwa mbele kwa hatua zaidi.
No comments:
Post a Comment