Habari za Punde

Balozi Seif ajumuika na wananchi na wanafamilia kumzika Bi Fatma Moh'd Othman


Na Othman Khamis Ame, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  leo amejumuika pamoja na Wananchi pamoja na wana wa Familia katikia mazishi ya Mjumbe wa Bodi ya Tume ya Utumishi Serikalini  Bibi Fatma Moh’d Othman aliyezikwa kijijini kwao Jimbo la Kiwani Mkoa wa Kusini Pemba.

Marehemu Bi Fatma Moh’d  alifariki Dunia Jana katika  Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili Jijini Dar es salaam alikokuwa akipatiwa matibabu kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa Shindikizo la Damu { Blood Pressure }.

Balozi Seif katika mazishi hayo akitanguliwa na Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi  pia aliambatana na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Ali Abdulla Ali, Mwakilishi wa Jimbo la Rahaleo Mh. Nassor Jazira, Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani Mh. Ali Salim Mkuu wa
Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Omar Khamis Othman pamoja na Viongozi mbali mbali wa Serikali vyama vya siasa pamoja na Dini.

Marehemu Bibi Fatma Moh’d Othman ambae ni Mama mzazi wa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mh. Mwanajuma Majid katika uhai wake alishika nyafidha mbali mbali za Kiserikali pamoja na Kisiasa.

Katika utumishi wa Serikali Marehemu Bi Fatma aliwahi kuwa Mwalimu Mkuu wa Skuli za Ngomeni na Mkoani Pemba, Afisa wa Elimu Wilaya ya Mkoani, Mratibu wa Uendeshaji na Utumishi Elimu  Pemba  Pamoja na Mjumbe wa Bodi ya Utumishi Serikalini wadhifa alioutumikia hadi kufikwa na mauti.

Katika utumishi wa Kisiasa Mrehemu Bi Fatma alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania { UWT } Wilaya ya Mkoani, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa CCM, Mjumbe wa Baraza Kuu la Wazazi pamoja na UWT.

Pia alikuwa Mjumbe wa Kamati tekelezaji Wilaya ya Mkoani Wazazi na UWT, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mainduzi Mkoa kuanzia mwaka 21 hadi 215 pamoja na Mjumbe wa  Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.

Marehemu Bibi Fatma Moh’d Othman aliyezaliwa mwaka 1950 na kufikia umri wa miaka 65 ameacha Watoto Tisa na Wajukuu kadhaa.

Mwenyezi Muungu ailaze roho ya Marehemu Bibi Fatma Moh’d Othman mahali pema Peponi. Amin.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.