STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 06 Juni, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema utajiri mkubwa wa historia ya uhusiano na urafiki kati ya watu wa Zanzibar na Ujerumani unawafanya watu wa nchi mbili hizo kuongeza ari ya kuuendeleza na kuuimarisha uhusiano na urafiki wao.
Katika hotuba fupi aliyoitoa kumshukuru Meya wa Jiji la Wurzburg wakati alipotemebela Ofisi za Meya wa jiji hilo jana, Dk. Shein alieleza kuwa karne nyingi za uhusiano na ushirikiano kati ya watu wa Zanzibar na Ujerumani zimeacha simulizi nyingi ambazo ni vigumu kuzielezea au kuzindika ikatosheleza msikilizaji ama msomaji.
Alilishukuru jiji la Wurzburg kwa kuwa mwenyeji wa Maonesho ya kila mwaka ya muziki na utamaduni wa Afrika na kutoa shukrani pekee kwa Waandaaji na Maonesho hayo na jiji hilo kwa kuipa Zanzibar fursa ya pekee katika Maonesho ya mwaka huu.
Katika Maonesho hayo Zanzibar imepewa fursa ya kupeleka kikundi cha Taarab ambacho kimekuwa kivutio kikubwa katika Maonesho hayo na pia kuwepo maonesho maalum kuhusu Zanzibar.
Kufuatia fursa hiyo kumekuwepo na matangazo mengi katika jiji la Wurzburg yanayosifia Zanzibar na watu wake ikiwemo vivutio vya biashara ya utalii hatua ambayo itasaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar kila mwaka kutoka Ujerumani.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi Ujerumani inashika nafasi ya pili ya nchi zinazoleta watalii wengi Zanzibar kila mwaka.
Dk. Shein aliusifu uongozi wa jiji la Wursburg kwa mafanikio makubwa katika kuhifadhi historia ya jiji hilo yakiwemo majengo miongoni wao jengo la Ofisi za Meya na kuongeza kuwa Zanzibar nayo inafanya jitihada kama hizo katika kuhifadhi historia yake kwa mfano mji mkongwe.
Akiwa katika Ofisi hizo Dk. Shein alitia saini kitabu cha wageni wa jiji hilo ambacho kinaitwa”Golden Book of Wurzburg” pamoja na kupeana zawadi na Mstahiki Meya wa jiji hilo Christian Schuchardt.
Akimkaribisha Dk. Shein katika Ofisi hizo, Mstahiki Meya wa Jiji hilo Christian Schuchardt alieleza kuwa jengo hilo lilijengwa karne ya 12 na ni miongoni mwa majengo ya zamani katika mji huo na pia ni miongoni mwa majengo mazuri ya zamani yaliyohifadhiwa nchini Ujerumani.
Alibainisha kuwa jiji wa Wurzburg ni mashuhuri kwa utalii na ni mji unaovutia sana mikutano na matamasha na kwamba wageni wote mashuhuri wa jiji hilo ni lazima wafike katika ukumbi wa jengo la Ofisi za Meya kama alivyofanya Dk. Shein.
Mstahiki Meya huyo alizidi kueleza kuwa jiji limepiga hatua kubwa katika elimu na taaluma muhimu matokeo yake karibu wafaidika wa tunzo ya Nobel 14 wamefanya tafiti zao katika chuo kikuu cha Julius Maximilians jijini humo miongoni mwao ni Wilhelm Conrad Rontgen aliyevumbia mashine ya x-ray mwaka 1895.
Mstahiki Meya alibainisha pia kuwa baadhi ya watu huliita jiji hilo kuwa jiji la mashauriano na kubadilishana mawazo kati ya Ujerumani na nchi za Afrika na kutoa mfano kuwa Chuo Kikuu cha Wurzburg kina uhusiano na vyuo vikuu 19 barani Afrika.
Zaidi jiji hilo lina uhusiano wa kindugu na jiji la Mwanza nchini Tanzania tangu mwaka 1966 na hivi sasa Hospitali ya Misionari ya Wurzburg inafanya kazi kwa pamoja na Chuo Kikuu cha Bugando na Hospitali ya Bugando huko Mwanza.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitembelea pia ofisi za Serikali ya Jimbo la Bavaria ambako mbali ya kupata maelezo kuhusu utendaji wa Bunge la Jimbo hilo lakini pia alitembelea sehemu mbali mbali za jengo hilo ambalo ni miongoni mwa majengo yaliyoharibiwa wakati wa vita kuu vya dunia.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari wa gazeti la Main Post la jiji la Wurzburg mara ya baada ya kutembelea majengo hayo, Dk. Shein alieleza kuwa kazi ya kukarabati na kuyarejesha majengo ya historia ni jukumu nzito lakini muhimu katika kuendeleza historia ya mji huo ambao ni urithi utakaodumu milele.
Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu maonesho ya muziki alibainisha kuwa amefurahishwa sana na kueleza kuwa ni jambo la kujivunia kuona Zanzibar imepewa heshma kubwa katika mji huo na anatarajia kila mtu aliyeshiriki maonesho hayo na wakaazi wote wa mji huo watafurahishwa na ushiriki wa Zanzibar katika maonesho hayo.
Dk. Shein anatarajiwa kuendelea na ziara yake nchini Ujerumani leo kwa kutembelea kiwanda cha kutengeneza magari cha Mercedes na baadae kutembelea maonesho ya Zanzibar ambayo yamepewa jina la “Zanzibar-Traditions at the gate to Africa”.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
No comments:
Post a Comment