Habari za Punde

Kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Na Ali Issa na Rahma Hamiss Maelezo –Zanzibar.    
Wizara ya Mawasliano na Miundombinu Zanzibar imedhamiria kununua vifaa vya upekuzi wa mizigo na abiria katika Bandari ya Zanziabr katika  mwaka ujao wa fedha.

Hayo yamesemwa  huko Baraza la Wakilishi nje ya Mji wa Zanzibar na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Issa Haji Ussi (Gavu) wakati akijibu suali la Mwakilishi Jaku Hashim Ayuob alietaka kujua sababu ya Serikali kushindwa kuweka vifaa vya ukaguzi kama ilivyo katika  bandari ya Tanazania bara ili kuepusha vitendo vya uvunjifu wa haki za binaadamu ikiwemo kuwapapasa abiria katika Sehemu zao za siri.

Amesema Wizara yake imeamua  kununua vifaa hivyo ili kuweka usalama zaidi kwa kugundua vitu hatarishi kufuatia  ongezeko kubwa la abiria na mizigo wanao ingia na kutoka katika bandari hiyo.

Amesema mashine hizo zitanunuliwa mwaka ujao wa fedha ambapo mradi huo tayari umeshaingizwa katika bajeti ijayo ya Shirika la Bandari Zanzibar ili kuondoa kasoro ziliopo za kiusalama na haki za kibinaadam.

Aidha alifahamisha kuwa kwa sasa njia inayotumika kuwachunguza abiria na mizigo ni kuwapekuwa kwa mikono jambo ambalo limepitwa na wakati na linapelekea  abiria  kukosa huduma kwa haraka.

Hata hivyo alieleza kuwa katika upekuzi huo wanawake hupekuliwa na wanawake weziwao na wanume hupekuliwa na wanaume weziwao kwa mpangilio maalumu.


“Kwaza naomba kufahamisha kuwa Wizara yangu kupitia Shirika la Bandari tumeweka utaratibu kwa wasafiri wanawake kupekuliwa na Maafisa wanawake na wanaume kupekuliwa na maafisa wanaume wezao pale inapo bidi msafiri kupekuliwa mwilini,” alisema Gavu.

Aidha alieleza kwa upande wa mizigo Shirika halibagui mzigo wa mwanamke au mwaname kwani mizigo hiyo hupekuliwa na afisa  aliepo wakati huo na  ndio utaratibu wa kawaida katika bandari zote. 

Na Ali Issa na Rahma Khamis Maelezo Zanziabr.
Shirika la umeme  Zanzibar (ZECO) linadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 50.8 na Shirika la umeme  Tanzania (TANESCO)  ambazo ni malimbikizo ya madeni ya miezi ya nyuma hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu.

 Naibu waziri wa Wizara ya Ardhi, Maji,Makazi na Nishati   Haji Mwadini Makame ameeleza hayo  katika Baraza la Wawakilishi wakati akijibu swali la Salim Abdalla Hamadi alietaka kujua kiasi cha fedha ambacho ZECO inakusanya na inachodai kutoka kwa  wateja wake na kiasi cha fedha wanachodaiwa na TANESCO.

Amesema Shirika la umeme la Zanzibar limekuwa likipata hasara kutokana na kupanda kwa gharama za ununuzi wa umeme kutoka TANESCO na bei ya chini wanayowauzia wateja wao.

Alieleza kuwa sababu  nyengine ya  kushindwa kulipa TANESCO ni makusanyo kidogo  kutoka Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma.

Amewaeleza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa hadi kufikia mwezi Machi 2015  ZECO linawadai wateja wake zaidi ya shilingi Bilioni 33.02.

Akitoa ufafanuzi wa deni hilo alisema wateja wa kawaida wanadaiwa shilingi Bilioni 9.01, Taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar shilingi Bilioni 22,52 na shilingi Bilioni 1,45 wanadai Taasisi za  Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema hasara hiyo imeonekana katika mahesabu ya Shirika hilo ya mwaka ulioishia tarehe 30 juni 2014.

Ameongeza kusema kuwa pamoja na madeni na hasara wanayoipata Shirika limeweza kutekeleza majukumu yake ya msingi ikiwemo kupeleka umeme vijijini.

“ZECO limeweza kujiendesha pamoja na  kupata hasara kwani  imeweza kulipa robo tatu ya ankara yake kwa TANESCO na robo inayobakia hutumia kwa shughuli zake za kawaida,” alieleza Naibu Waziri.

Alisema katika kuhakikisha ZECO inapunguza  deni hilo wamekubaliana na TANESCO kulipa ada ya mwezi  na kutoa shilingi Bilioni moja kila mwezi.
Aidha alisema ZECO imeweza kulipa  ada kwa miezi minne na kulipa ziada ya milioni 500 kwa TANESCO
                          IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO ZANZIBAR



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.