Habari za Punde

Pemba wahofia maeneo ya kihistoria kutoweka

Na Haji Nassor, Pemba
 WANANCHI kisiwani Pemba, wamekumbwa na wasiwasi mkubwa wa kutoweka historia ya kisiwa hicho, kutokana na baadhi ya maeneo ya kihistoria, kuanza kupotea taratibu ikiwemo misikiti na nyumba za watawala, zilizojengwa miaka 600 iliopita, kwa kukosa ushughulikiaji wa kina.
Wamesema kisiwa hicho kilichojaaliwa kuwa na maeneo zaidi ya 44 ya kihistoria ambayo mengine tokea karne ya tisa, 14, 15 na hata 18, wamekuwa wakipata wasi wasi, kwamba kizazi kijacho baada ya miaka 20 watakosa kumbu kumbu hiyo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, walisema haitokuwa busara, kumbu kumbu na historia ya Zanzibar ambayo kwa sasa ipo, kubakia kwenye vitabu pekee hapo baadae.
Walieleza kuwa, maeneo hayo kama hayakuenziwa kwa juhudi za makusudi na serikali, yanaweza kutoweka wakati wowote hasa kwa vile yapo mengine yamezongwa na vichaka.
Mmoja kati ya wananchi hao, Hamad Makame wa Chambani alisema katika eneo lao, kuna msikiti na makaburi, ambayo imejengwa tokea karne ya 14, sawa na miaka 700 iliopita, mbapo hayapo katika hali ya kuridhisha.

“Makaburi yaliopo hapa na msikiti, vizazi vyetu vya sasa wanafaidi mara mbili historia ya nchi yao, lakini kwa hili ambayo hayashughukiwi ipasavyo, wanaokuja watasoma kwenye vitabu pekee’’,alifafanua.
Nae Abass Haji Omar wa kisiwa Panza, alisema tayari katika kisiwa hicho, msikiti uliokuwepo tokea karne ya 18, sawa na miaka 300 iliopita yapo mabaki pekee.
“Hakuna hasa mshughulikiaji wa eneo lililokuwa na msikiti, sasa inabidi kuwe na historia ya kuchimba mabaki, lakini kuta zilizokuwepo zimeshajifukia’’,alisema.
Kwa upande wake Hashim Saaduni Mwalimu alisema hata eneo la Mtambwe mkuu, hakuna udhibiti wa kutosha, ambapo nako kumeanza kupotea.
“Kwa mfano hapa kwetu Mtambwe mkuu pana makaburi yafika 20 na msikiti tokea karne ya 14, lakini huoni wahusika wakiyashughulikia ipasavyo’’,aliongeza.
Akizungumzia malalamiko hayo, Kaimu Mkuu wa Idara wa Mambo ya Kale na Makumbusho Pemba, Salim Seif alikiri kwamba maeneo kadhaa ya historia kisiwani Pemba, yamenza kutoweka taratibu.
Alisema hilo linasababishwa kutokana na ukosefu wa rasilima fedha na watu, ambapo kati ya maeneo 44 ya kihistoria walipohamia na kuweka wafanyakazi ni maeneo manne (4) pekee.
Aliyataja maeneo hayo ambayo kwa sasa yanausimamizi chini ya Idara yao kwa kina, ni Chwakwa Tumbe, Mkumbuu, Pujini, Kichokochwe na Ole ambapo maeneo 39 kwa sasa hakuna wafanyakazi wa kudumu.
“Tarifa rasmi serikali iko kwamba maeneo hayo kukosa wafanyakazi, ndio sababu ya kuanza kutoweka taratibu, na hasa ukosefu wa fedha ya kuyafanyia matengenezo’’,alieleza.
Aliyataja maeneo kama ya Kiwani, ambapo kwa sasa kumebakia kikuta cha kibla cha msikiti, ambapo huanguka kila muda kutokana na kukosa kufanyiwa marekebisho hasa baada ya msimu wa mvua.
Aidha alisema wastan wa miaka 15 ijayo, baadhi ya maeneo hayo ya kihistoria yatatoweka moja kwa moja, pindi juhudi za makusudi ya kuyanusuru hazikuchukuliwa, ikiwa ni pamoja na kutengewa bajeti yenye kukidhi haja.
Wilaya ya Chake chake pekee ina maeneo 10, ya kihistoria, wilaya za Mkoani na Wete13, wakati wilaya ya Micheweni 12 likiwemo la msikiti wa Mkiang’ombe uliojengwa karne ya 13 sawa na miaka 800 sasa.
Kwa mujibu wa kitabu cha bajeti cha wizara ya habari, cha mwaka 2014/2015, kilielezwa kuweko kwa mradi wa kuyafanyia ukarabati endeleveu maeneo ya kihistoria ya Zanzibar.
Aidha kwenye kitabu hicho, kileleza kuwa mradi huo ulitengewa shilingi 230,000,000 ambapo hadi kufikia Mei mwaka jana, jumla ya shilingi67,400,207 ziliingizwa sawa na asilimia 29.
Ambapo kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa choo katika chemba ya watumwa Mangapwani, utengenezaji wa kisima cha chini kwa chini Mangapwani, uungaji wa umeme katika chemba ya Watumwa Mangapwani, uwekaji wa nguzo za mipaka katika maeneo ya kihistoria ya Pete, Bungi, Unguja Ukuu, Chuini, Dunga na Shakani.

Aidha kwa upande wa Pemba maeneo ya kihistoria ya Mkamandume na Msikiti Chooko yameendelezwa ili kuyaweka katika hali nzuri na kutumika kwa miaka mingi zaidi, ingawa mengi yanaendelea kupotea taratibu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.