Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua rasmi mradi wa Maji safi na salama wa Wananchi wa Shehia ya Jongwe iliyomo ndani ya Jimbo la Kiwani, Wilaya ya Mkoni, Mkoa wa Kusini Pemba.
Balozi Seif Ali Iddi akiutembelea mradi wa ujenzi wa Skuli ya Sekondari ya Wkilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba iliyopo katika Kijiji cha Mkanyageni kuona harakati za maendeleo ya ujenzi wake unaofanywa na Kampuni ya Ruuns.
Mhandisi wa Ujenzi wa Kampuni ya Runs Bwana Mohammed Hamad aliyevaa nguo nyeupe akimpatia maelezo Balozi Seif hatua iliyofikia ya ujenzi wa majengo ya Skuli ya Sekondari ya Wilaya ya Mkoani iliyopo katika Kijiji cha Mkanyageni.Nyuma ya Mhandisi Mohammed Hamad ni Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mh. Mwanajuma Majid.
Balozi Seif akizungumza na Walimu, Wazazi na Wanafunzi wa Madrasat Jahidu Fiiy - sabilillah ya Kijiji cha Mwambe Wilaya ya Mkoani baada ya kukagua ujenzi wa jengo la Madrasa hiyo na kujionea changamoto zinazowakabili.
Mwalimu Mkuu wa Madrasat Nur Minal Quran ya Kijiji cha Mwambe Wilaya ya Mkoani akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hatua waliyofikia ya ujenzi wa jengo lao ambapo wanahitaji kuungwa mkono na wadau wa elimu ya Dini. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mheshimiwa Mwanajuma Majid.
Picha na – OMR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi amewapongeza Wananchi
wa Shehia ya Jongwe kwa uamuzi wao wa kujitafutia mbinu za kupambana
na changamoto zinazowakabili katika Shehia yao hasa lile la
huduma za
maji safi na salama.
Alisema
uamuzi wao huo ndio uliopelekea washirika wa
maendeleo,Viongozi
pamoja na wahisani kuamua kuwaunga mkono katika kukabiliana
na tatizo la huduma za maji safi na salama baada ya kuona juhudi
walizozionyesha.
Balozi
Seif Ali Iddi alitoa pongezi hizo wakati akiuzindua rasmi mradi wa Maji
safi na salama wa Wananchi wa Shehia ya Jongwe iliyomo ndani ya Jimbo
la Kiwani Wilaya ya Mkoni Mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema
Serikali inaelewa changamoto mbali mbali zinazowakabili Wananchi
katika maeneo yao tofauti Nchini na ndio maana ikatoa kipaumbele
katika kuwasaidia nguvu za uwezeshaji na hata taaluma katika
kupambana nazo.
Balozi
Seif aliwashauri Wananchi wa Shehia ya Jongwe kuhakikisha kwamba
jukumu la kulinda mazingira yanayolizunguuka eneo la Kisima cha maji liko
mikononi mwao.
Alisema
ipo tabia kwa wananchi walio wengi kuona tatizo na kuliachia bila ya
kuchukuwa hatua yo yote na matokeo yake kulalamikia changamoto za tatizo
hilo linalochukuwa muda mrefu kulipatia ufumbuzi.
Akigusia
suala la amani ya Nchi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba
Wananchi hao wakiendelea kujiandaa na maandalizi ya uchaguzi
Mkuu wa Mwezi wa Oktoba mwaka huu waelewe kwamba suala la utulivu
wa amani wanalisimamia kwa nguvu zao zote.
Alitahadharisha
kwamba Serikali itaendelea kulinda amani iliyopo na kamwe
haitamvumilia mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuvuruga hazina na
lulu hiyo inayoringiwa naTanzania katika nyanja ya Kimataifa.
Balozi
Seif alifahamisha kwamba hakuna Mtu mwenye akili timamu akajaribu
kuwa na mawazo au kauli za kuitakia mabaya nchi yake ilhali na yeye
anaendelea kuishi ndani ya nchi hiyo.
Katika
kuunga mkono juhudi za Wananchi hao wa Shehia ya Jongwe Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar alichangia shilingi Milioni 1,000,000/- na
kuahidi i kukamilisha nyengine iliyobaki ili kulipa Deni la vifaa walivyokopa
Wananchi hao katika kukamilisha mradi huo wa maji safi na salama.
Akisoma
Risala Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Shehia ya Jongwe Ndugu Mussa
Juma alisema mradi wa maji safi na salama ulibuniwa mnamo Tarehe19 Machi
mwaka 2014 kufuatia usumbufu mkubwa uliokuwa ukiwapata Wananchi
hao wa kupata maji safi na salama.
Ndugu
Mussa alisema Wananchi hao walikuwa wakitumia maji yasiyo safi na
kupelekea kukumbwa na maradhi ya miripuko yaliyosabisha madhara kwa wananchi
walio wengi wa Kijiji hicho.
Alisema
juhudi za pamoja za Wananchi kupitia Kamati yao ya Maendeleo ndio
iliyofanikisha mradi huo ulioungwa mkono na Viongozi mbali mbali,wahisani,
mfuko wa Jimbo, Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA }pamoja na shirika
la Umeme Zanzibar {ZECO }.
Naye
Afisa Mdhamini Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Pemba Ndugu
Hemed Salum alisema mradi mkubwa wa maji safi na salama katika ukanda
huo ulibuniwa na kuanza rasmi mwaka 2006 baada ya mripuko wa maradhi
ya matumbo katika Jimbo la Kiwani.
Nd. Hemed
alisema hatua za uchimbaji kisima zilianza mwaka 2007 kwa ufadhili
ya Jumuiya ya Misaada ya Maendeleo ya Al – Yousuf Charitable Society
ya Nchini Saudi Arabia na kufaidisha takriban Vijiji vya Mwambe na
Shamiani.
Afisa
mdhamini huyo wa Wizara ya Ardhi, makazi, Maji na Nishati aliwahakikishia
Wananchi hao wa Jongwe kwamba Mamlaka ya Maji Zanzibar
{ ZAWA } itaandaa utaratibu maalum wa kukifanyia utafiti Kisima
hicho ili kuelewa mienendo ya maji yake kwa vile kiko karibu na Bahari.
Akijibu
changamoto inayowakabili Wananchi hao ya kufungwa kwa Mashine ya Tukuza
kwenye kisima hicho Nd. Hemed aliwaahidi Wananchi hao kwamba jukumu
hilo litabebwa na Wizara hiyo ili kuwaondoshea usumbufu
Wananchi
hao wa kukatika katika kwa huduma za Umeme kwenye kisima hicho.
Kisima
hicho cha maji safi na salama kilichopo Jongwe Mwambe chenye uwezo wa
kuzalisha Lita Tani Elfu 10,000 kwa saa moja kikiwa na mifereji
89 iliyosambazwa kuhudumia wananchi wa Vijiji vitatu vya Jongwe,
Mwambe na Shamiani kimegharimu zaidi ya shilingi Milioni 44,755,000/-.
Wakati
huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alizitembelea
Madrasat Jahidu Fiiy - sabilillah na Madrasat Nur Minal Quran za
Kijiji cha Mwambe Wilaya ya Mkoani.
Akizungumza
na Walimu, Wazazi pamoja na Wanafunzi wa Madrasa hizo baada ya
kuona changamoto zinazowakabili Balozi Seif alisema uamuzi wa wazee hao
kuwatengenezea mazingira mazuri ya kupata elimu watoto wao ni jambo
zuri na la msingi.
Aliwatahadharisha
walimu wa madrasa hizo kujiepusha na tabia ya baadhi ya walimu
nchini wenye hulka ya kuwapotosha wanafunzi na kusahau wajibu
wao wa kuwapatia watoto elimu ya dini kama ilivyoagizwa katika
vitabu
vya Muumba wa ulimwengu.
Katika
kuunga mkono jitihada za walimu na wazazi wa Kijiji hicho Balozi
Seif alichangia shilingi Milioni 1,000,000/- kwa madrasat ahidu
Fiiy - sabililah na kuahidi kusaidia shilingi Milioni 5,000,000/-
kwa kila madrasa zote mbili katika kipindi kifupi kijacho.
Hatua ya
Balozi Seif pia ilimuhamasisha Mbunge wa Viti Maalum CCM Mkoa
Kusini Pemba Mh. Faida Moh’d Bakari ambaye naye aliahidi kuchangia
shilingi 2,000,000/- kwa madrasat Jahidu Fiiy - sabilillah na
shilingi Milioni 5,000,000/- kwa Madrasat Nur Minal Quran.
Mapema
asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alipata fursa ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Skuli ya Sekondari
ya Wilaya ya Mkoani iliyopo katika Kijiji cha Mkanyageni.
Ujenzi wa
Skuli hiyo unaenda sambamba na ule wa Skuli ya Sekondari ya Wilaya ya
Kusini Unguja iliyopo Kibuteni aliyoitembelea hivi karibuni ambazo
zote zinafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA }.
Mhandisi
Mkuu wa Ujenzi wa Skuli hiyo kutoka Kamuni ya Ujenzi ya Runs Bwana
Mohammed Hamad alimueleza Balozi Seif kwamba Kampuni yake inatarajia
kukabidhi Skuli hiyo mwishoni mwa Mwezi Disemba mwaka huu ili iwahi
kuanza kuchukuwa wanafunzi mapema mwezi Januari mwaka 2016.
Bwana Mohammed
alisema wafanyakazi wa kampuni hiyo hivi sasa wanaendelea
na hatua za mwisho za ujenzi wa nyumba za walimu, mabweni ya
wanafunzi, kupaka rangi madarasa pamoja na kukamilisha sehemu za michezo
mbali mbali ndani ya eneo la skuli hiyo.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar alionyesha kuridhika kwake na ujenzi
huo unaokwenda kwa kasi zaidi kuliko ule ya majengo ya Skuli ya Sekondari
ya Kibuteni licha ya kuanza mwanzo kwa zaidi ya miezi mitatu nyuma ya
Skuli ya Mkanyageni.
No comments:
Post a Comment