Habari za Punde

Dk Shein: Kuwapatia wananchi huduma ya maji ni miongoni mnwa vipaumbele vya serikali

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                 18 Agosti, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa huduma ya maji ni moja ya vipaumbele vya Serikali na ndio maana utekelezaji wa malengo ya kusambaza huduma hiyo kwa wananchi umekuwa wa mafanikio makubwa.

Alifafanua kuwa kuongezeka kwa mahitaji makubwa ya huduma ya maji nchini ni miongoni mwa changamoto zinazotokana na mafanikio makubwa ya utekelezaji wa malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964 ambayo yalilenga katika kuimarisha kiwango cha maisha ya wananchi kwa kuhakikisha kuwa huduma za jamii zinapatikana ikiwemo maji safi na salama.

Akizungumza mara baada ya kuzindua mradi wa maji katika jimbo la Kikwajuni mjini Unguja leo pamoja na Kituo cha Maendeleo ya Vijana cha Jimbo hilo, Dk. Shein alisifu ubunifu wa uongozi wa jimbo hilo chini ya Mbunge wake Hamad Masauni Yusuf kwa kuweza kushirikiana na wananchi pamoja na washirika wa maendeleo kubuni na kufanikisha miradi hiyo miwili muhimu katika jimbo hilo.


Aliongeza kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu nchini ambako kumeambatana na ongezeko kubwa la mahitaji ya maji kwa shughuli mbali mbali za maendeleo, kuchakaa kwa miundombinu ya maji pamoja na kupungua kiwango cha maji katika vyanzo vya maji kunachangia kuwepo kwa tatizo la uhaba huduma hiyo.

Hata hivyo alibainisha kuwa kiwango cha upatikanaji wa maji katika maeneo ya mijini umeongezeka kutoka asilimia 75 mwaka 2010 hadi asilimia 87 hadi sasa  ambapo kwa upande wa mkoa wa mjini Magharibi kiwango kimefikia asilimia 87.7. Kwa upande wa vijijini alieleza kuwa hali ya upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka asilimia 60 mwaka 2010 hadi 70 mwaka huu.

Dk. Shein alieleza matumaini yake kuwa katika kipindi kilichobaki huduma hiyo itaendelea kuongezeka kwa kuwa kazi ya kuimarisha huduma hiyo inaendelea ili kufikia malengo yaliwekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010-2015 ambayo yanaelekeza maji mijini yafikie kiwango cha asilimia 95 na vijijini asilimia 80.  

Mradi huo wa maji ambao ni wa awamu mbili umejumuisha kuchimba kisima kilichochimbwa katika eneo la kambi ya jeshi Migombani, kuweka tangi pamoja na kusambaza maji katika maeneo ya Kilimani na maeneo ya karibu.
Dk. Shein aliipongeza Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kwa kuongeza jitihada za kuimarisha huduma ya maji ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma hiyo.

Aliwashukuru washirika mbalimbali wakiwemo Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kuchangia mradi wa maji pamoja na Kituo cha Maendeleo ya Vijana na kuelezea matarajio yake ya kuona mashirika zaidi wanashirikiana na kituo hicho kusaidia maendeleo ya vijana.

Dk. Shein alieleza kufurahishwa na taarifa za matokeo ya kituo hicho za kubadili tabia za baadhi ya vijana ikiwemo ‘kikundi cha Ubaya Ubaya’ ambacho huko nyuma kilivuma kwa vitendo visivyopendeza kwa jamii lakini leo kimekuwa kikundi cha mfano wa tabia na kujitegemea.

Katika hotuba yake hiyo fupi Dk. Shein alikubaliana na ombi la uongozi wa Kituo cha Vijana kuwa mlezi wa kituo hicho na kuahidi kushirikiana nao kufikia malengo ya kituo kwa faida ya vijana nchini.    
                                       
Akiwa katika kituo hicho ambacho kinajulikana kama Tanznia Youth Icon-TAYI aliangalia shughuli mbalimbali vijana ambazo zimelenga kuwawezesha vijana kukabiliana na changamoto za maisha ikiwemo ukosefu wa ajira.
Kabla ya kufikia kituoni hapo alikagua kisima huko katika kambi ya jeshi ya Migombani pamoja na kuzindua mradi wa maji huko eneo la Mnara wa Mbao Kilimani.

Katika maelezo yake mafupi kumkaribisha Mhe Rais, Waziri wa Ardhi,Makaazi, Maji na Nishati Ramadhani  Abdalla Shaaban aliushukuru uongozi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania-JWTZ kwa kuiruhusu serikali kuchimba kisima katika eneo lake.

Aidha aliwashukuru na kuwapongeza wananchi wa jimbo la Kikwajuni kwa kuweza kufanikisha mradi huo kitendo ambacho kimechangia utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuwapatia wananchi wake maji safi na salama.
   
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni Hamad Masauni Yusuf aliwaeleza wageni na wananchi waliohudhuria hafla hiyo jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na wananchi kulitafutia ufumbuzi tatizo la maji ikiwemo kuchimba visima vidogo vidogo katika jimbo hilo.

Hata hivyo alieleza lengo la mradi huu awamu ya kwanza na awamu ya pili umelenga kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo la maji katika jimbo hilo.

Masauni alifafanua kuwa wananchi wa jimbo hilo kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo waliweza kutekeleza awamu ya kwanza ya mradi huo kwa gharama ya shilingi milioni 344 kati ya hizo shilingi milioni 200 zilitolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa-UNDP.

Aliongeza kuwa kwa awamu ya pili ya mradi tayari Kituo cha Maendeleo ya Vijana tayari kimeshapatiwa fedha nyingine milioni 320 kwa kazi hiyo.


Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

                                               

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.