Habari za Punde

Dk Shein: Kuna umuhimu mkubwa kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na Zimbabwe

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Balozi mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Zimbabwe Lt.Gen.Mstaafu Charles Makakala alipofika Ikulu Mjini Zanzibar kujitambulisha leo,[Picha na Ikulu.]

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na Balozi mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Zimbabwe Lt.Gen.Mstaafu Charles Makakala alipofika kujitambulisha Ikulu Mjini Zanzibar  leo,[Picha na Ikulu.]


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) akifuatana  na Balozi mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Zimbabwe Lt.Gen.Mstaafu Charles Makakala baada ya mazungumzo yao leo alipofika  Ikulu Mjini Zanzibar kujitambulisha   ,[Picha na Ikulu.]


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Zanzibar                                                                         21.08.2015
---
RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha uchumi wa kidiplomasia kati ya Zimbabwe na Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa nchi hizo zina uhusiano wa kihistoria.

Dk. Shein aliyasema hayo leo, huko Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zimbabwe Mhe. Luteni Jenerali Mstaafu Charles  Laurence Makakala, ambaye alifika Ikulu kwa ajili ya kuaga na kupata baraka za Rais.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Makakala  kuwa tayari Tanzania na Zimbabwe zimekuwa na uhusiano wa kindugu na wa kihistoria hivyo mkakati zaidi unahitajika katika kuimarisha uchumi wa kidiplomasia kati ya nchi hizo ili zizidi kupata mafanikio.

Dk. Shein alisema kuwa katika hatua za kuimarisha sekta za maendeleo sambamba na kukuza mashirikiano kati ya Tanzania na Zimbabwe uimarishwaji wa sekta ya uchumi ina umuhimu wa pekee hivi sasa hasa ikizingatiwa mafanikio yaliopatikana katika nchi mbili hizo
.

Alisema kuwa uimarishwaji wa mashirikiano katika sekta ya biashara nayo yanahitajika kwa kiasi kikubwa kati ya nchi mbili hizo kutokana na kuwa mazuri tokea siku za nyuma.

Aidha, alisema  kuwa uhusiano na ushirikiano katika sekta ya utalii nalo ni jambo muhimu hasa ikizingatiwa kuwa nchi ya Zimbabwe imekuwa ni miongoni mwa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika ambayo imekuwa ikipata watalii kutokana na kivutio chake kikubwa cha maporomoko ya maji Victoria ‘ Victoria waterfalls’.

Dk. Shein alisema kuwa sekta hiyo ya utalii pia, ni sehemu ya uimarishaji wa uchumi wa Kidiplomasia hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania nayo ina vivutio vingi vya kitalii vikiwemo vivutio vilivyopo katika visiwa vya Zanzibar na maeneo mengine yakiwemo mbuga za wanyama.

Alisema kuwa ipo haja ya kuendelea kuimarishwa uhusiano kati ya nchi mbili hizo kwa kuwepo programu maalum za ubadilishanaji wa utaalamu na wataalamu kati ya vyuo vya Tanzania na Zimbabwe ambapo hapo awali ulikuwepo kupitia Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaa na vyuo vya Zimbabwe.

Hivyo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kusisitiza haja ya  vyuo vikuu vya Zimbabwe kuimarisha uhusiano na vyuo vikuu vya Zanzibar kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) hasa ikizingatiwa kuwa chuo hicho tayari kimeshaanza kusomesha Shahada ya Uzamifu ‘PhD’ katika lugha ya kiswahili.

Alisema kuwa kutokana na hatua kubwa iliyofikiwa hivi sasa katika kuikuza lugha ya Kiswahili kwa nchi za Afrika, lugha hiyo ni moja kati ya lugha rasmin za Umoja wa Afrika (AU) inayozungumzwa katika mikutano yake.

Hivyo, Dk. Shein alisema kuwa,  ipo haja kwa Zimbwabwe kuitumia fursa hiyo kuleta vijana wake kuja kujivunza lugha ya Kiswahili hapa Zanzibar kwani pia, wapo baadhi ya wananchi wa Zimbabwe wanaozungumza Kiswahili.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano kwa Taasisi za utafiti wa mazao ya kilimo kati ya nchi mbili hizo kutokana na mafanikio yaliopatikana sambamba na mikakati iliyowekwa katika kuikuza sekta hiyo katika nchi hizo.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aligusia umuhimu wa kuendeleza suala zima la Diaspora kwa kuwaunganisha na kuwaweka pamoja Watanzania wanaoishi nchini humo na kuwaeleza fursa zilizopo nchini mwao, ikiwa ni pamoja na kuwasisitiza kuekeza nyumbani.

Nae Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zimbwabwe  Mhe. Luteni Jenerali Mstaafu Charles Laurence Makakala alitoa shukurani zake kwa uteuzi huo alioupata na kumuahidi Dk. Shein kuwa atazidi kujenga uhusiano na kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Zimbabwe ambao una historia tokea wakati wa kudai uhuru.

Balozi Makakala alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa kuendeleza uhusiano na ushirikiano kati ya nchi mbili hizo kati nyanja mbali mbali za kimaendeleo hasa katika uchumi wa Kidiplomasia ambao unaweza kuleta mafanikio kwa pande zote mbili.

Aidha, Balozi huyo alieleza kuwa Zimbabwe kuna vitu vingi ambavyo Tanzania inaweza ikajifunza na hatimae kuleta mafanikio hivyo, atatumia fursa hiyo kuhakikisha mafanikio yanapatikana sambamba na kuhakikisha uhusiano na ushirikiano uliopo unaimarika.


Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.