Habari za Punde

WanaCUF waaswa kutohadaiwa na kutorubuniwa kwa kuuza shahada za kura

Katibu Mkuu wa CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wanachama na wafuasi wa CUF katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kilwa Kivinje leo.

Na Khamis Haji , OMKR

Katibu Mkuu wa  Chama cha Wananchi CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amewaonya wanachama na wafuasi wa CUF na vyama vyote vinavyounda umoja wa UKAWA wasikubali kuhadaiwa na watu wanaopita kununua vipande vya kupigia kura.

Maalim Seif ametoa onyo hilo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika leo Kilwa Kivinje, jimbo la Kilwa Kusini alipokuwa katika ziara ya kichama jimboni humo.

Alisema kitendo cha kukubali kurubuniwa na kuuza shahada ya kupigia kura ni kusaliti malengo na shabaha za Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA ambao ni kuleta ukombozi wa kiuchumi na kukuza maendeleo ya Watanzania.

“Nataka muelewe 20,000 au 30,000 unayopewa leo ili upoteze haki yako ya kupiga kura itakusababishia miaka mitano ya kula msago”, alionya Katibu Mkuu wa CUF.

Alitoa kauli hiyo baada ya kuwepo malalamiko mengi kutoka kwa viongozi wa CUF na vyama vinavyounda UKAWA juu ya kuwepo watu wanaopita kwenye maeneo wanayohisi kuna wapinzani wengi na kuwarubuni wawauzie vipande vyao vya kupigia kura.

Alisema kuwa miongoni mwa mikakati ya Chama cha Mapinduzi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba ni kununua vipande vya kura kwa wanachama na wafuasi wa upinzani wakizani kwamba hatua hiyo itaweza kuwasaidia na kuwanusuru na wasikumbwe na wimbi kubwa la upinzani kuchukua nchi.

Katika hatua nyengine Maalim Seif amewakabidhi kadi wanachama wapya 619 waliojiunga na chama hicho, wakiwemo waliokihama chama cha Mapinduzi katika jimbo la Mafia.

Maalim Seif amewakabidhi kadi wanachama hao wapya katika mkutano wa hadhara uliofanyika Katika uwanja wa Mkunguni Kilindoni, ambao pia ulihudhuriwa na mgombea Ubunge wa Ukawa kupitia CUF, Omar Kimbau aliyejiunga na chama hicho wiki iliyopita akitokea CCM.

Akihutubia mkutano huo, alisema azma ya wapinzani ni kushika dola na kuhakikisha wananchi wote Tanzania wanapata haki zote za msingi kwa usawa na hakuna raia wa daraja la kwanza na daraja la pili.

Alisema hivi sasa watoto wa matajiri ndio wanaopata elimu bora kwa sababu wazazi wao wanamudu kuwapeleka shule bora nje ya nchi, lakini watoto wa maskini wanaishia kupata elimu duni katika shule za Kata na wengine kushindwa kupata elimu kabisa.

Aidha Katibu Mkuu wa CUF alisema nia ya viongozi wa Ukawa ni kupiga vita vitendo vya rushwa vilivyokithiri nchini ambavyo kwa kiasi kikubwa vinachangia wananchi walio wanyonge kushindwa kupata haki zao.

“Chini ya CCM rushwa haiwezi kuondoka Tanzania, hivi sasa ili uweze kupata nafasi ya uongozi lazima utoe rushwa na kama huna fedha huwezi kupata uongozi”, alisema Maalim Seif.

Alisema mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM uliomalizika hivi karibuni uligubikwa na vitendo vya rushwa na udanganyifu hali ambayo inathibitisha rushwa ni tatizo kubwa lililoota mizizi.

Hata hivyo, Maalim Seif alisema zama za utawala wa CCM zinakaribia kufika ukiongoni na matarajio ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi Ukawa ni kushika dola mara baada ya kufanyika uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka huu.

“Hapa Afrika vyama vilivyo pigania uhuru vimekabia vichache, Kenya na Zambia tayari vimeondoka madarakani, Tanzania mwaka huu kitaondoka madarakani na kutakuwa na Serikali inayoongozwa na wapinzani Bara na Zanzibar”, alisema.

Naye mgombea ubunge wa jimbo la Mafia kupitia CUF, Omar Kimbau alisema Mafia imekosa Mbunge jasiri na shupavu na kwamba yeye ameamua kugombea nafasi hiyo ili kuwajengea matumaini mapya wananchi wa kisiwa hicho.

Kimbau alisema iwapo atachaguliwa kuwa Mbunge atahakikisha mama lishe, wafanyabiashara wadogo wadogo na vijana wote wa jimbo hilo wanafanya shughuli zao za kujiongezea kipato bila ya hila na wala hawatasumbuliwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.