Habari za Punde

Dk.Shein: Kuimarisha Ustawi wa Watoto ni Moja ya Vipaumbele Vyetu.

                                                    STATE HOUSE ZANZIBAR

                                            OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
                                                                                  PRESS RELEASE                                                                     
   Pemba                                                                                                                            27.8.2015
---

RAIS wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekizindua Kiwanja cha kufurahishia watoto cha ZSSF Umoja Tibirinzi Pemba na kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Saba imeweka kipaumbele katika kuimarisha hali na ustawi wa watoto kwa njia zote.

atika hotuba yake aliyoitoa mara baada ya uzinduzi huo Dk. Shein alisema kuwa tayari Serikali anayoiongoza imetekeleza mipango mingi ya maendeleo yenye lengo la kuimarisha elimu, afya na usalama wa watoto na kutoa shukurani kwa wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao katika utekelezaji wa mipango hiyo.

"Napenda niyakariri tena maneno ya Rais wetu wa Kwanza wa Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pale aliposema 'Furaha ya watoto ni neema kwa wazee'... imani yangu ni kwamba kumalizika kwa kiwanja hiki na kile cha Kariakoo Unguja kutamaliza kilio na kiu ya muda mrefu ya watoto wetu",alisema Dk. Shein.

Aidha,  alieleza kuwa uzinduzi huo ni jumla ya utekelezaji kwa vitendo wa mipango na maelekezo yaliyoagizwa kwenye Ilani ya CCM iliyoeleza kuwa chama hicho kitaielekeza Serikali kuendeleza malezi ya watoto kwa kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuimarisha viwanja vya kuchezea watoto katika ngazi za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.

Dk. Shein alieleza kufurahishwa kwake na ZSSF kutokana na ujenzi huo ambapo Mfuko huo umejenga kiwanja hicho kwa fedha zake wenyewe bila ya msaada wala kukopa huku akisisitiza kuwa kushiriki kwa kampuni za kizalendo katika miradi mikubwa kama huo ni ishara ya kukua na kuimarika kwa kampuni za hapa nchini.

Alisisitiza kuwa kunahitajika kuzipa fursa kubwa zaidi kampuni za hapa nchini zinazoonesha kuwa na uwezo na utaalamu katika sekta zinazojishughulisha nazo na kusisitiza kujenga utamaduni wa kujiamini, kuachana na dhana ya kuwa kila kizuri katika nchi hii kinajengwa na kampuni kutoka nje.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa viwanja vyote viwili  vya watoto ni maendeleo ya kujivunia katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Saba, hasa ikizingatiwa wapo waliowahi kukejeli, kubeza na kudhihaki kwenye mitandao ya kijamii kuwa viwanja hivyo ni magofu ya viwanja vya watoto.

"Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni Serikali inayoongozwa na misingi ya utawala bora na demokrasia na pale penye ukweli na khitilafu tunakiri, lakini hatulumbani, kwani tunatambua kuwa 'Ada ya mja ni kunena, muungwana ni vitendo' na wahenga wamesema 'Mwenye macho haambiwi tizama",alisema Dk. Shein.

Aliongeza kuwa Zanzibar imepiga hatua kubwa sana katika kuwawekea watoto mazingira mazuri ya kuchezea na kujifurahisha vikiwemo viwanja hivyo kwani kuna nchi nyingi za Afrika hazina mambo hayo licha ya gharama kubwa lakini Zanzibar imeweza.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alisema kuwa kwa kuiga mfano wa ZSSF,  alizihimiza taasisi za fedha ziimarishe mashirikiano na ubunifu ili ziweze kutumia amana na mitaji waliyonayo kwa kuweza katika miradi mbali mbali.

Vile vile alizihimiza taasisi zote za Serikali kuimarisha utaratibu wa kubadilishana taarifa za uendeshaji ambazo ni muhimu kwa maendeleo na Serikali kwa jumla akitolea mfano katika jitihada za kupambana na utoaji wa mishahara na mafao hewa ambapo panahitajika mashirikiano baina ya Benki, ZSSF, na taasisi za Serikali.

Dk. Shein alitoa shukurani kwa taasisi zilizoshirikiana na ZSSF katika ujenzi huo, na kutoa pongezi kwa Mkandarasi wa Kiwanaja hicho Kampuni ya Kizalendo ya Mazrui Building Contractors pamoja na Kampuni ya Golden Horse kutoka China kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kufunga mitambo na vifaa mbali mbali kiwanjani hapo.

Aidha, alitoa pongezi kwa Mshauri wa ujenzi huo Kampuni ya Covell Mathews and Partnership, Msambazaji wa Umeme na Miundombinu ya CCTV, Kampuni ya Mollel Electrical Contractor na wengineo.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kukubali ombi lililotolewa la kupunguza kodi ya VAT kwenye kiingilio cha kiwanja hicho ambayo itakuwa ni asilimia 18.

Nae Waziri wa Fedha Mhe. Omar Yussuf Mzee, alieleza kuwa kila Wizara ina jukumu la watoto na kutoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuitaka Wizara hiyo kutenga kodi kwa ajili ya ununuzi wa madawati ya watoto ambapo asilimia 50 ya kodi ya Bandari inakwenda katika utekelezaji huo.

Aidha, aliendelea kutoa shukurani na kumpongeza Dk. Shein kwa hatua zake za kupandisha mishahara katika mwaka 2011 na mwaka 2013 hatua ambayo imepelekea mfuko wa ZSSF nao uimarike na kuweza kufanya shughuli zake huku makushanyo ya yakiimarika kutoka chini ya shilingi Bilioni 12 alipoingia madarakani hadi Bilioni 23 hivi sasa.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya 6 ya Wadhamini wa Mfuko wa ZSSF Dk. Suleiman Rashid alieleza kuwa ujenzi wa kiwanja hicho ni matunda ya uongozi wa Dk. Shein ndani ya miaka yake mitano sambamba na matunda ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Mapema, Mkurugenzi Mwendeshaji  wa ZSSF Abdulwakil Haji Khafidh alieleza kuwa ujenzi wa Kiwanja hicho una awamu tatu ambapo ujenzi wa kiwanja cha kufurahishia watoto cha Umoja ni awamu ya kwanza ambapo awamu ya pili ni ujenzi wa ofisi mpya ya ZSSF itakayokuwa na ghorofa tatu ili kuweza kuwahudumia wanachama wa ZSSF.Na
Awamu ya tatu ni ujenzi wa hoteli ya kisasa ambayo itakuwa ni ya ghorofa tano yenye vyumba 70.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa kwa awamu ya kwanza, mradi huo unatarajiwa kutumia TSh. Bilioni 7 hadi kukamilika kwake ikiwa ni pamoja na pembea tano mpya na za kisasa, jengo la michezo ya ndani, jukwaa la maonesho ya wazi, vibanda 8 vya biashara, sehemu 4 za kuuzia vyakula na jengo la utawala.

Vyengine ni majengo mawili ya vyoo ambayo yana jumla ya vyoo 20, sehemu ya kusalia, chumba cha matengenezo na kuhifadhi vifaa, uwekaji wa mifumo ya usalama wa kiwanja kama kamera za ulinzi(CCTV camera), uwekaji wa majenereta na ujenzi wa kituo cha Polisi.

Aidha, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa ZSSF inatarajia mradi huo utajilipa ndani ya kipindi cha miaka kumi ijayo, kutoa ajira zaidi ya 50 kwa wananchi na kueleza kuwa kwa wakati mmoja uwanja unatarajiwa kupokea watu wasiopungua 10,000.


Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.