STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
29.8.2015
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Algeria na Tanzania ni nchi zenye
historia katika uhusiano na ushirikiano wao ulioanzishwa na waasisi wa nchi
hizo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere pamoja na Rais wa kwanza wa Algeria
Mhe. Ahmed Ben Bella.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo wakati wa mazungumzo kati yake na Balozi mpya wa Jamhuri ya Demokrasia
ya Watu wa Algeria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Belabed Saad, huko
Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo
hayo, Dk. Shein alisema kuwa uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Ageria
ni wa kihistoria hivyo kuna kila sababu ya kuuimarisha zaidi kwa kufuata nyayo
zilizowekwa na waasisi hao wa nchi hizo.
Dk.Shein alisema
kuwa kwa upande wa Zanzibar, nchi ya Algeria ina uhusiano mzuri
na wa muda mrefu tokea wakati wa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ambapo nchi hiyo ni ya kwanza katika
bara la Afrika kuyatambua Mapinduzi ya Januari 12, 1964 hatua ambayo ilipelekea
kuitwa jina la Skuli ya Ben Bella ambayo ipo Zanzibar kama alama ya uhusiano
huo.
Katika historia
ya kumbukumbu za kupigania uhuru wa Tanzania na Algeria mashirikiano makubwa
yalikuwepo kwa waaasisi wa nchi mbili hizo ambapo Dk. Shein alisisitiza kutunzwa,
kuenziwa na kuendelezwa kwa manufaa ya pande mbili hizo.
Aidha, Dk. Shein
alisema kuwa Algeria imekuwa na ushirikiano na uhusiano mzuri na Zanzibar katika uimarishaji wa sekta ya elimu kwani
imeweza kuwapatia nafasi za masomo vijana wengi wa Kitanzania wakiwemo kutoka
Zanzibar.
Hivyo kutokana na
ushirikiano huo katika sekta hiyo, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuongezwa kwa
nafasi za masomo kwa vijana wa Zanzibar nchini humo.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein alieleza kuwa mbali ya kuwepo kwa ushirkiano katika sekta hiyo ya
elimu kuwa kuna haja kuwepo kwa mashirikiano katika sekta nyenginezo za
maendeleo ikiwemo uwekezaji. huku alieleza iwapo nchi hiyo itakuwa tayari
kununua zao la karafuu kutoka Zanzibar basi Zanzibar iko tayari baada ya
kupokea maombi.
Dk. Shein pia,
alieleza kuwa mbali ya sekta hizo Zanzibar pia, ina mengi ya kujifunza kutoka
Algeria ikiwa ni pamoja na mafanikio yaliopatikana katika miundombinu, mafuta,
gasi na nguvu za umeme.
Nae Balozi mpya
wa Jamhuri ya Demokrasia ya Watu wa Algeria katika Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Belabed Saad alieleza kuwa Algeria inathamini sana uhusiano na
ushirikiano wa muda mrefu uliopo katika ya Tanzania na nchi hiyo ambao
uliasisiwa na viongozi wake wa mwanzo.
Balozi Saad
alieleza kuwa Algeria itaendeleza uhusiano huo na ushirikiano uliopo sambamba
na kuendeleza zaidi uimarishaji katika sekta za maendeleo sambamba na
kuimarisha uchumi wa kidiplomasia kati ya nchi mbili hizo.
Mapema Dk. Shein
alifanya mazungumzo na Mhe. Irene Florence Mkwawa, Balozi mpya wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania nchini Uholanzi, mazungumzo yaliofanyika Ikulu mjini
Zanzibar.
Katika Mazungumzo
hayo, Dk. Shjein alimueleza Balozi Mkwawa kuwa Tanzania na Uholanzi ina
uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ambao umeweza kusaidia uimarishaji wa
sekta mbali za maendeleo Zanzibar na Tanzania Bara zikiwemo afya, mapambano
dhini ya UKIMWI, elimu, uwekezaji na sekta nyenginezo.
Kwa upande wa
Zanzibar, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Uholanzi imeweza kutoa
ushirikiano mwema katika uimarishaji wa sekta ya afya, elimu na nyenginezo huku
akisisitiza kuwa nchi hiyo imekuwa na mashirikaino mazuri na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya.
Dk. Shein
alimueleza Balozi huyo kuwa Serikali ya Uholanzi imeweza kuiunga mkono Zanzibar
katika ujenzi wa wodi mpya ya akina mama na watoto chini ya Mradi wa ORIO na
miradi mengineyo huku Dk. Shein akimueleza Balozi Mkwawa umuhimu wa kuimarisha
uchumi wa Kidiplomasia katika ya Tanzania na nchi hiyo.
Aidha, Dk. Shein
alimueleza Balozi huyo maelewano yaliofikiwa kati ya Zanzibar na Uholanzi hasa
kupitia Kampuni yake ya mafuta ya SHELL ambapo Zanzibar ilitiliana saini
makubaliano ya ushirikiano katika kuendeleza sekta ya mafuta na gessi Agosti
2013 mjini Hague wakati wa ziara yake ya kikazi.
Alieleza kuwa
makubaliano hayo ya awali kati ya Zanzibar na Kampuni hiyo ni pamoja na kufanya
utafiti wa mafuta na gesi baada ya kumaliza taratibu za nchi ambapo tayri hivi
sasa vikao kadhaa vimeshakaa kwa lengo la kujadili suala hilo muhimu la
kimaendeleo.
Dk. Shein
alieleza kuwa mbali ya kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar katika hatua hiyo pia,
suala la ajira na elimu kwa vijana wa Kizanzibari nalo litaimarika kwani
litapewa kipaumbele zaidi mara baada ya kuanza mchakato huo.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo haja ya kuendelea kuimarisha uhusiano na
ushirikiano katika sekta ya utalii, kwani watalii wengi wamekuwa wakitokea
nchini humo.
Aidha, alimueleza
Balozi huyo azma ya kuimarishwa na kuendelezwa suala zima la Diaspora na
Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar na kumsisitiza kuwasihi wanadiaspora wa Tanzania nchini humo kuja
kuekeza na kujenga nyumbani.
Nae, Balozi Irene
Florence Mkwawa alimuahidi Dk. Shein kuwa atatumia uwezo wake wote kwa
mashirikiano ya pamoja katika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Uholanzi unaimarika
zaidi.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment