STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Dar-es-Salaam
14.8.2015

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kutambua umuhimu wa ushiriki wa Diaspora
katika maendeleo ya Tanzania zilianzisha Idara maalum za uratibu na
kuwahamasisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi ili waweze kushiriki katika
maendeleo ya nchi yao.
Dk. Shein
aliyasema hayo leo katika hotuba iliyosomwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
Ikulu na Utawala Bora Mhe. Dk. Mwinyihaji Makame wakati wa kufunga Kongamano la
Pili la Diaspora huko katika Hoteli ya Serena, mjini Dar-es-Salaam.
Katika hotuba
hiyo, Dk. Shein alitoa wito kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuzitumia
ipasavyo Taasisi hizo kwa kutambua na kujua fursa mbali mbali zilizopo
Tanzania.
Dk. Shein
aliwaeleza Wanadiaspora popote pale walipo ni muhimu kukumbuka nyumbani kwa
lengo la kuwasaidia ndugu zao kupata ajira sambamba na kuwekeza nyumbani ili
kuwapa ajira Watanzania wenzao.
Aidha, Dk. Shein
aliwaahimiza Wanadiaspora kuendelea kutoa ushirikiano wao kwa wadau wote pale
inapohitajika sambamba na kutoa taarifa zao kwenye afisi zinazowakilisha kwa
lengo la kutoa kumbukumbu na mipango sahihi.
Alisema kuwa
ushirikiano wao ndio uliofanikisha Kongamano hilo na kuonesha imani yake kwa
kila mmoja wao na kueleza matumaini yake kuwa utaratibu huo utaendelea ili
lengo liweze kufikiwa la kuitetea nchi pamoja na kuijengea heshima.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alitumia fursa hiyo, kumshukuru Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa upendo wake na ushirikiano wake
anaouonesha katika uongozi wake.
Pia, alitoa
shukurani za dhati kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Ofisi ya Rais Ikulu Zanzibar na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendeleza juhudi za
kuwaunganisha Wanadiaspora na kuongoza timu inayoandaa Kongamano hili.
Dk. Shein
alipongeza hatua zilizofikiwa katika mijadala ya Kongamano hilo kwani imeweza
kuimarisha na kujenga daraja la mahusiano na mashirikiano ya uzalishaji na
kibiashara kati ya sekta ya biashara ndogo ndogo na za kati zilizomo ndani na
nje ya nchi.
Kongamano hilo ni
la Pili, kufuatia lile la kwanza lililofanyika mwezi Agosti mwaka jana katika
hoteli hiyo ya Serena mjiniDar-es-Salaam, ambapo Kongamano lijalo hapo mwakani
linatarajiwa kufanyika Zanzibar.
"Tutaendelea kuamini kuwa ushirikiano
mliouonyesha katika Kongamano hili utaendelea kuwepo katika Makongamano yajayo
na katika shughuli mbali mbali za kuwashirikisha Watanzania waishio nje ya
nchi",alisema Dk. Shein.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein aliwapongeza Wanadiaspora kwa kuzitumia kikamilifu siku mbili za
Kongamano hilo kwa kubadilishana mawazo, uzoefu, kupeana taarifa za fursa mbali
mbali za uwekezaji na biashara zilizopo hapa nchini na zile zinzopatikana nje
ya nchi.
Nao washiriki wa
Kongamano hilo walitoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa juhudi zao za kuhakikisha suala zima la
Diaspora linaimarika sambamba na kuwaunganisha na kuwashajiisha vilivyo
Wanadiaspora wa Tanzania waliopo nchi mbali mbali duniani.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment