Pemba
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, kimelaani vitendo vinavyofanywa na wafuasi
wa chama cha CUF cha kuwapiga wafusi wa CCM wanaobandika picha za wagombea wao
pamoja na kuzichana picha za wagombea wa CCM zinazobandikwa sehemu mbali mbali
kwa ajili ya Kampeni.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai
Ali Vuai alilaani vitendo hivyo katika mkutano wa Kampeni ya uchaguzi wa CCM
uliofanyika Konde, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba uliohudhuriwa
na maelfu ya wanaCCM na wananchi ambapo mgeni rasmi alikuwa mgombea Urais wa Zanzibar
kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.
Vuai alisema kuwa Chama cha CUF ndio
kilichoanza kuzindua Kampeni zake za uchaguzi mapema kabla ya CCM, pia ndicho
kilichoanza kubandika picha za wagombea wao Unguja na Pemba bila ya kufanyiwa
fujo wala vurugu zozote lakini anashangazwa na vitendo vya wafuasi wa CUF
kuwapiga vijana wa CCM wanaobandika picha pamoja na kuzichana picha za wagombea
wa CCM.
Katika maelezo yake, Vuai alisema Chama
cha CUF ndio cha mwanzo kuanza fujo na vurugu lakini pia ndio cha mwanzo kupita
kwenye vyombo vya habari, Tume ya Uchaguzi na kusema uongo kuwa wao ndio
wanaofanyiwa fujo.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM alisema kuwa chama hicho kimesaini
kanuni za maadili ya uchaguzi na kuahidi kuendesha kampeni za kistaarabu bila
ya kuwepo vitisho, kutukanana, kupigana na hata kuchana picha za wagombea iweje
leo CUF tayari wameshaanza kufanya vitendo hivyo ambavyo alisema ni vya
kusikitisha.
Aidha, alisema kuwa makubaliano
yalifanyika kwa vyama vya CUF na CCM baada ya kuwepo siasa chafu kwa muda mrefu
makubaliano ambayo yalifanyika mara tatu na hatimae kupatikana muwafaka
uliopelekea kuundwa Serikali ya Mapoinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa
Kitaifa chini ya uongozi wa Dk. Shein lakini alionesha kushangwazwa na CUF
kuanza dalili za kuvunja makubaliano hayo.
Mapema Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar,
Mhe. Pandu Ameir Kificho alisema kuwa
kuna haja ya kumchagua Dk, Shein kwani anaijua siasa sambamba na kutekeleza
suala zima la amani na utulivu kwa vitendo.
Alisema kuwa mara zote wanapofika wageni
kutoka sehemu mbali mbali duniani afisini kwake huwaeleza namna Dk. Shein
alivyodhamiria kuhakikisha uchagauzi mkuu wa mwaka huu unakuwa huru na haki
pamoja na juhudi zake za kuhakikisha amani na utulivu uliopo vinaendelea.
Aidha, alieleza kuwa amekuwa akitumia
nafasi kuwaeleza wageni hao jinsi Dk. Shein anavyofuata sheria pamoja na
kuitekeleza na kuilinda Katiba ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Kutokana na juhudi hizo Spika Kificho
alisema kuwa hiyo ndio sababu ya kutosha kwa Dk. Shein kupewa nafasi ya
kuongoza kwa mara ya pili kuwa Rais wa Zanzibar.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais Mohammed Aboud alisema kuwa CCM imefanya mambo mengi katika kipindi cha
miaka mitano iliyopita ikiwa ni pamoja na kuimarisha miradi ya maendeleo.
Aboud alisema kuwa Dk.Shein amejenga
misingi imara ya kuleta maendeleo hivyo kuna kila sababu ya wananchi kumchagua
yeye pamoja na viongozi wengine wa CCM wanaowania nafasi katika uchaguzi wa
mwaka huu.
Alisema kuwa tayari chama cha CUF
kimeshaonesha dalili mbaya ya kushindwa kutokana na kiongozi wake mkubwa Juma
Duni kuanza kuhama hama kwa kutokana na uchoyo wa madaraka na fedha.
Dk. Maua Daftari akimnadi Dk. Shein
pamoja na wagombea wote wa CCM kwa upande wa Zanzibar na wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania alisema kuwa mafanikio makubwa yameweza kupatikana katika uongozi
wa CCM chini ya Dk. Shein katika kipindi chake cha miaka mitano.
Dk. Daftari alisema kuwa juhudi
zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwemo
kilimo zimeanza kuzaa matunda na hivi sasa wananchi walio wengi
wanajishughulisha na kilimo cha mboga mboga hapa Pemba na hivi sasa hawaagizii
tena bidhaa hizo kutoka Tanzania Bara.
Aidha, alisema kuwa tayari miradi ya
maendeleo imekamilishwa ikiwemo miradi ya barabara,afya, elimu, maji, umeme
sambamba na kukua kwa sekta ya utalii kwa kuwepo hoteli yenye chumba chini ya
bahari ambacho ni kivutio kikubwa cha watalii hivi sasa ambao wamekuwa wakija
Pemba.
Dk. Daftari alitumia fursa hiyo kutoa
shukurani kwa Dk. Shein kwa kusimamia amani na utulivu pamoja na maendeleo
makubwa yaliopatikana huku akisisitiza haja ya kuendelea kumchagua yeye na
viongozi wote wa chama hicho wanaowania nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano,
Urais kwa Zanzibar,Ubunge, Uwakilishi na Udiwani.
Nae Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Khadija
Aboud aliwataka wanaCCM kutofanya kosa la kutomchagua Dk. Shein kwani ndio
kiongozi mwenye Sera za kuleta maendeleo pamoja na kuwataka kuwachagua viongozi
wote wa CCM
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment