Habari za Punde

Dk Shein: Mkinichagua nitaheshimu Katiba na Sheria kwa kuunda Serikali yenye Mfumo wa Umoja wa Kitaifa

·         Mkinichagua nitaheshimu Katiba na Sheria kwa kuunda Serikali yenye Mfumo wa Umoja wa Kitaifa.
Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi kumchangua tena kwa mara ya pili kuongoza Zanzibar ili aweze kutekeleza dhamira yake ya kuendelea kuibadili Zanzibar hatua kwa hatua.

Akizungumza katika mkutano mkubwa wa kampeni katika mji mdogo wa Konde katika Wilaya ya Micheweni, Mkoa Kaskazini Pemba leo mgombea huyo amesema “amekusudia kuibadili Zanzibar hatua kwa hatua”.

“katika kipindi cha miaka mitano ya kwanza ya awamu hii serikali niliyoiongoza imeweza kuweka misingi imara ya kuijenga Zanzibar” alisema Dk. Shein huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Aliwaambia wananchi hao kuwa Serikali aliyoiongoza ambayo ilikuwa chini ya mfumo wa Umoja wa Kitaifa ilifanya kazi nzuri na kuiwezesha Zanzibar kujenga mazingira mazuri ya kuimarisha uchumi wake.

“Katika kipindi cha miaka mitano ijayo ikiwa mtanipa ridhaa ya kuongoza nitaibadilisha Zanzibar kwa mujibu wa uwezo wake kiuchumi ambao tumeweka lengo la kukua kwa kiwango cha asilimia 10 ifikapo mwaka 2020.” Dk. Shein alieleza.

Alisema kuwa uwezo wa kufikia kiwango hicho upo kutokana na mipango kambambe ya kuimarisha miundombinu ya kuchumi ikiwemo kukamilisha jengo jipya la abiria katika kiwanja cha ndege cha Unguja pamoja na ujenzi wa bandari mpya ya Mpigaduri unaotarajiwa kuanza muda si mrefu.

Hatua hizo alifafanua kuwa zitasaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar kutoka 311,000 hivi sasa hadi 500,000 kwa mwaka, wakati bandari mpya ya Mpigaduri itakuwa na uwezo wa kushughulikia mizigo zaidi ya kontena 200,000 kwa mwaka.


Katika mkutano huo Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anaemaliza muda wake alisema akichaguliwa tena ataheshimu Katiba na Sheria kwa kuunda Serikali iliyo katika Mfumo wa Umoja wa Kitaifa kama Katiba inavyoelekeza.

Aliahidi wananchi wa Konde kuwa katika kipindi kijacho pamoja na kuwa kumekuwepo na mafanikio makubwa katika kusambaza huduma za jamii serikali itaendelea kuimarisha huduma hizo.

Kwa upande wa maji safi na salama, Dk. Shein alibainisha kuwa Konde inapata maji kwa asilimia 87 hivi sasa na katika kipindi kijacho vijiji zaidi vitapatiwa maji kikiwemo kijiji cha Misufini kwa Wamanga.

Dk. Shein aliwaeleza wananchi wa Konde kuwa baada ya kukamilisha usambazaji wa umeme katika shehia zote za Konde,katika kipindi kijacho jitihada zataelekezwa katika kuvipatia huduma hiyo vijiji vya Kivumoni, Ungi Sokoni, Kiumbemzito, Mtondoo jeuri na Mnarani.

Aliahidipia kuendeleza ujenzi wa barabara za Kiuyu kwa Manda hadi bandarini na Kifundi hadi Kipangani kwa kuziwekea kifusi huku mipango ikiwa mbioni kuzijenga kwa lami siku za baadae.

Aliwatahadharisha vijana kuhusu kauli rahisi za wanasiasa zinazoeleza kama kwamba suala la ajira ni jambo rahisi na kuwaeleza kuwa serikali haina uwezo wa kutoa ajira kwa kila kijana lakini kinachofanyika ni kuweka mazingira mazuri ili vijana wengi waweze kujiajiri.

Katika kufanya hivyo pamoja na kutoa mikopo kuwawezesha kujiajiri lakini pia Serikali inahamasisha uwekezaji zaidi kwani hiyo ndio njia pekee ya kuzalisha ajira zaidi.


Dk. Shein  kesho anatarajiwa kuendelea na Kampeni zake kisiwani Pemba kwa kuzungumza na wananchi wa Micheweni katika uwanja wa Shaame mata. 

1 comment:

  1. nani akucahaguwe wwe nyie mnaiiuza zanzibar kwa bure ,dhamira mlizonazo hazitakamilika kwani tunataka nchi yetu na tutaijenga wenyewe na hatuna shida nanyie fungeni virago vyenu kwani muda ushafika mumetutia umasikini wa kutoasha na sasa tanachukua nchi yetu tunairudisha mahali inapotakiwa.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.