Habari za Punde

CCM Zanzibar yasisitiza amani na utulivu, yakumbusha vyomba vya dola vipo macho


  
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                              28.9.2015
---

VIONGOZI wa CCM Zanzibar wamewataka wananchi wa Zanzibar kuendeleza amani, utulivu na mshikamano uliopo na kuwaonya wale wote wanaokusudia kufanya vurugu wakati wa uchaguzi mkuu wajue kuwa Serikali pamoja na vyombo vyake vya Dola viko macho.

Viongozi hao waliyasema hayo leo katika Mkutano wa  Kampeni ya uchaguzi wa CCM uliofanyika katika uwanja wa Garagara, Jimbo la Mtopepo, Mkoa wa Mjini  Magharibi uliohudhuria na maelfu ya wanaCCM na wananchi ambapo mgeni rasmi alikuwa mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.

Nae Mjumbe wa Kamati Kuu na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd alisema kuwa vyama vya upinzani hawana Sera na hoja na hivi sasa wamebaki kubwabwaja.

Balozi Seif alisisitiza haja ya kuimarishwa kwa umoja na mshikamano kwa wananchi na wanaCCM kwa jumla na kusema kuwa umoja ndio silaha ya kushinda kwa CCM.

Alisema kuwa kuwepo kwa amani na utulivu ni jambo la lazima na kuwaonya wale wote waliodhamiria kufanya fujo wakati wa uchaguzi kuachana na azma yao hiyo na kuwaonya wanachama wa CUF wasije kujaribu kufanya fujo huku akiwataka wazee wa Darajabovu kutowaachia vijana wao kufanya fujo.

Aidha, Balozi Seif aliwataka wazee wasije kuilaumu Serikali iwapo watoto wao watafanya fujo kwani Dola haijaribiwi wala haichezewi na kueleza kuwa anaetaka kujaribu akale muhogo ajue kama ni mtamu ama mchungu lakini sio serikali.

Alisema kuwa Serikali iko macho kwa kuwadhibiti wale wote walio na lengo la kufanya vurugu siku ya tarehe 25 na 26.


"Wao wanasema watakuja kuingoa na mimi nna jua unaongolewa ni muhogo kama Serikali basi kuna taratibu zake kidemokrasia....kama unataka kungoa aende akangoe kwenye shamba la baba ake", alisema Balozi.

Alisema kuwa huu si wakati wa kuwasemea wananchi, na hakuna serikali ya mkataba kwani serikali ya mkataba lengo  lake ni kuvunja Muungano, na CCM haiko tayari kuwepo kwa serikali ya Mkataba na kueleza kuwa CCM wanachokijua wao ni serikali mbili.

Alisema  kuwa ndani ya miaka mitano maendeleo makubwa yamepatikana Unguja na Pemba huku akitolea mfano miundombinu ya barabara pamoja na kuwepo huduma nyengine za maendeleo.

Nae Spika wa Baraza la Wawakilishi Pandu Ameir Kificho alitumia fursa hiyo kwa kusema kuwa Dk. Shein ni mtu muadilifu, makini, muangalifu na katika maamuzi yake hakurupuki na kwa mwenendo na tabia hizo hakuna mgombea wa urais wa kumpa kura nyingi za ndio isipokuwa Dk. Shein.

Kificho aliwaomba wananchi kuwapeleka Wawakilishi wa CCM na Wabunge wa CCM kwani wao ndio wanaofanya kazi vizuri kwa maendeleo ya Watanzania na wananchi wa Zanzibar kwa jumla na hawana mtindo wa kutoka toka katika nyumba hizo za kutunga sheria.

Nae Waziri wa Maji,Ardhi na Nishati Ramadhani Abdalla Shaaban  alishangazwa na kauli za CUF zinazosema kuwa  ndani ya miaka 50 Zanzibar haina maendeleo na kusema kuwa mbali ya miaka hiyo wanayosema wapinzani tayari ndani ya miaka mitano tu ya Dk. Shein maendeleo yaliopatikana Unguja na Pemba ni makubwa.

Alieleza kuwa tayari wanaCCM na wananchi wameshaamua tarehe 25 kummiminia kura zote Dk. Shein na kusema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya CCM uchumi umeimarika.

Pamoja na hayo, alieleza kuwa  angalau CUF wanakiri kuwa kifungu cha Katiba mpya inayopendekezwa cha 23 na 26 kimeelezea kwamba ardhi, mafuta na gesi yatashughulikiwa na Zanzibar, na kusema kuwa kinachosubiriwa ni wakati wa kuipigia kura Katiba inayopendekezwa ifanye kazi.

Alisema kuwa tayari Rais Jakaya Mrisho Kikwete na  Dk. Shein wameshakubaliana juu ya Sheria ya mafuta na gesi, na tayari sheria hiyo imeshakwenda kwenye Bunge la Muungano kwa lengo la kuwa Zanzibar ishughulikie wenyewe rasilimali hizo.

Nae Bi Fatma Karume mke wa muasisi wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume, alisema kuwa wanawake walidhalilishwa, walitupwa lakini ASP ikaliona hilo na hatimae kuwasimamisha akina mama kwenda katika mikutano ya hadhara na kupiga kura kwani hapo mwanzo hawakupewa fursa hizo.

Bi Fatma, alitoa pongezi kwa akina mama kwa kupokea wito na kujitokeza kwa wingi katika mikutano  ya Kampeni ya CCM ambapo alitumia fursa hiyo kumuombea kuwa Dk. Shein, Dk. Magufuli, Samia, Wabunge, Wawakilishi pamoja na Madiwani wote huku akieleza kuwa Zanzibar tayari imeshakuwa huru tokea  Januari 12, 1964. 

Nae Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mfenesini Yussuf Mohammed Yussuf aliwataka wanaCCM kuzitunza shahada zao za kupigia kura na kuwataka kuwapigia kura wagombea wote wa CCM.

Alisema kuwa CUF hawana hoja na kushangazwa na kauli inayotoa kuwa Zanzibar haina Mamlaka kamili wakati tayari Zanzibar inayo mamlaka Kamili ila nia ya chama hicho ni kurudisha uongozi wa Kifalme.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.