Habari za Punde

Dk Shein: Nimetekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa vitendo


  
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Pemba                                                                                                           15.9.2015
---
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  amesema kuwa katika uongozi wake ametekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa vitendo huku pia, akitekeleza vizuri uongozi wake katika Serikali yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa kwa amani na utulivu.

Dk. Shein ambaye ni Mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM aliyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye mkutano wa Kampeni wa chama hicho uliofanyika huko katika viwanja vya Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba.

Dk. Shein aliwaeleza maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa endapo atachaguliwa tena ataendelea kuimarisha utulivu, amani na kuendelea kuwahudumia wananchi wa Zanzibar bila ya ubaguzi wa aina yeyote iwe wa kidini, rangi, kabila na hata mahala kwani hayo ndio maelekezo ya chama chake.

Alitaja baadhi ya mafanikio ya uongozi wake kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha ukuaji wa uchumi kutoka asilimia 4.5 hadi 7.2  ambapo kwa upande wa pato la taifa limeongezeka hadi trilioni 1.508 kutoka trioni 2.138.

Kuhusu mfumuko wa bei kiwango alisema kitaendelea kushuka ikiwa ni uthibitisho wa kutengemaa kwa uchumi wa taifa huku akieleza mipango uendelezaji wa maeneo huru ya Kiuchumi ya Fumba kwa kujengwa mji mpya pamoja na viwanda.



Kupambana na umasikini, kituo cha kulelea wajasiriamali ambacho ni kikiubwa katika Afrika Mashariki, ni lazima kuweko na programu maalum na hakuna njia ya mkato kama inavyoelezwa na Wapoinzani.

Aidha, Dk. Shein alieleza mafanikio yaliopatikana katika sekta ya kilimo na kueleza azma yake ya kuendeleza sekta hiyo huku akisisitiza kuendelea kutoa ruzuku na kuendelea kuwasaidia wakulima.

Kwa upande wa karafuu, alisema kuwa uwamuzi wa kuinua zao la Karafuu ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na kwamba hatua zilizochukuliwa la kutolibinafsisha biashara ya zao hilo sambamba na kupandisha bei ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kuimarisha zao hilo nchini.

Dk. Shein alibainisha kuwa uamuzi huo ulifanywa nan yeye mwenyewe na kupewa baraka na Baraza la Mapinduzi na kumtuma Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko kutanganza uamuzi huo.

Alisema kuwa asilimia 80 ya bei ya karafuu duniani wamepewa wakulima huku akieleza kuwa uongozi ni kazi na zaidi ni kuonesha njia.

Hadi sasa alieleza jumla ya tani za karafuu 5340 zimeuzwa na kukomesha magendo ya zao hilo kwa kuhakikisha kuwa taratibu zinafuatwa katika kuuza karafuu na hatua inayochukuliwa hivi sasa ni kuzifanya karafuu za Zanzibar kuwa alama maalum'branding'.

Katika sekta ya barabara Dk. Shein alieleza mafanikio yaliofikiwa kisiwani Pemba na hakuna barabara hata moja inayoungana na barabara kuu za Pemba ambayo haina lami na zilizobaki zinatarajiwa kumaliza karibuni.

Katika kuimarisha miundombinu ya usafiri wa baharini alieleza kuwa bandari mpya ya Mpigaduri itakayokuwa na uwezo wa kushughulikia kotena 200,000 kwa kwa mwaka itaanza kujengwa mara baada ya kukamilika kwa jengo la uwanja wa ndege.

Aidha  aliongeza kuwa Bandari ya Wete itajengwa upya na kuwaomba wananchi wawe wastahamilivu. 

Kwa upande wa wafanyakazi wa Serikali aliwaahidi kuendelea kuiamarisha maslahi yao kama alivyofanya katika kipindi chake cha uongozi kinachomalizika huku aliahidi endapo atachaguliwa tena atapandisha kima cha chini cha mshahara hadi 300,000 kwa mwezi.

kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM alisema utekelezaji umefanyika kwa asilimi 90 ambapo asilimia iliyobaki itaenaendelea kutekelezwa huku akieleza jinsi juhudi zilivyochukuliwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd nae alipata nafasi na kusikitishwa na maneno ya uongo yanazotolewa na kiongozi wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad.

Balozi Seif alisema kuwa Dk. Shein amefuata Ilani ya CCM kwa kuongeza bei ya karafuu pamoja na kuongeza idadi ya miche ya mikarafuu sambamba na kuliimarisha zao hilo.

Alisema kuwa chama cha CUF hakina uzoefu wa kuendesha Serikali na kueleza kuwa Maalim atakuwa mtu maarufu kwa kugombania mara sita urais wa Zanzibar huku akieleza kuwa mwisho wa chama chake ni 2015 kwani chama hicho na yeye mwenyewe hawatoweza kufikia mwaka 2020. "2015 CUF itakufa kifo cha mende miguu juu",alisema Balozi Sif.

Aliwata Wana CCM kuendelea kushikamana na kuwa wamoja kwa lengo la kupata ushindi wa uhakika  huku akisisitiza kuwa CCM ikishinda na Maalim Seif akikataa matokeo Dk. Shein ataunda Serikali ya CCM pekee.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, alisema kuwa wananchi wa Pemba mwaka huu wamedhamiria na wataleta mabadiliko makubwa.

Alieleza kusikitishwa na tabia za viongozi wa CUF za kuwatuma watoto pamoja na vijana kuchana picha za wagombea wa CCM zilizobandikwa huku akivitaka vyama vyote kufanya siasa za kistaarabu.

Nao viongozi wa CCM walipata fursa ya kusalimiana na wananchi pamoja na WanaCCM waliohudhuria katika mkutano huo na kuwapongeza wananchi wa Pemba kwa kuonesha azma ya kukiunga mkono chama hicho.
Mohamed Aboud nae alieleza kuwa chama cha CUF kimemuweka rehani  Makamu Mwenyekiti wao Juma Duni kwa kujiunga na CHADEMA na kusisitiza kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo nongono kuwa Maalim Seif amechoka na nafasi ya Makamu wa Kwanza na anataka kupewa Juma Duni na ndipo akaamua kumpeperusha na kumpelekeka CHADEMA.

Kiongozi huyo alilaani hatua iliyochukuliwa na CUF ya kuwatoa viongozi wao katika Baraza la Wawakilishi huku akieleza athari za kutoka kwao katika kikao hicho ambacho kilikuwa kinapitisha Bajeti ya Serikali.

Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka mitano Dk. Shein amefanya kazi kubwa sana katika kuleta mabadiliko makubwa na kujenga misingi imara ya maendeleo na anafaa kuwa Rais, na kuwahakikishia Wazanzibari kuona Zanzibar mpya katika uongozi wake wa miaka mitano ujao kwani ana mipango kabambe ya  kuondosha  umasikini na kuongeza ajira kwa vijana.

Nae Balozi Ali Karume aliwaomba wananchi wa Pemba kumpa kura zao Dk. Ali Mohamed Shein kutokana na kuwa na uwezo, uzoefu na kueleza kuwa mgombea wa CUF hamfikii Dk. Shein.

Bi Mauwa Daftari nae alieleza mafanikio yaliopatikana katika kuimarisha miradi ya maendeleo ikiwemo maji, barabara, umeme na mengineyo na kueleza jinsi anavyomfahamu Dk. Shein kuwa ni muadilifu, mchapakazi na hana tabia ya kusema uongo.

Alisema kuwa Sera za CCM ni kuwasikiliza wananchi shida zao na kuzifanyia kazi huku akisema anamfahamu sana Dk. Magufuli kwani amefanya kazi nae pamoja na sifa zake zinafanana  na za Dk. Shein na kueleza kuwa akipigiwa Dk. Shein akina mama nao tayari wameshapata nafasi kupitia Mama Samia Suluhu Hassan. 

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Hamad Mberwa, akiwakaribisha viongozi na WanaCCM pamoja na wananchi katika Mkoa huo alisema kuwa Pemba ya mwaka 1995,2000 na 2010 sio ya leo na wananchi wake wamebadikila, kimawazo na kivitendo. Kampeni rasmi za CCM zilifunguliwa siku ya Jumaapili tarehe 13.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.