Habari za Punde

Mabunge Yatakiwa Kusimamia Utekelezaji wa Maendeleo Mapya Endelevu.

Maspika wa Mabunge kutoka mataifa mbalimbali duniani wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Maspika hao  wamepitisha tamko  ambalo  linatambua na kupokea malengo na ajenda mpya za  maendeleo endelevu, na kuyataka mabunge kuhakikisha utekelezaji  malengo hayo yanayochukua nafasi  ya MDGs. Mhe Ann Makinda ni wa tatu kutoka kushoto mstari wa mbele.
Mhe. Spika  akiwa na  Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Katika Umoja wa Mataifa, Balozi  Tuvako Manongi,  wakati alipofika  katika Ofisi za Uwakilishi na kisha kuzungumza na  Maafisa. Mhe. Spika  ameeleza kuwa  moja ya mambo atakayoshauri ni pamoja na  kutaka  Maafisa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  kuwa na fursa ya  kuja katika Umoja wa Mataifa kujifunza na kujijengea uwezo kuhusu   mijadala ya kimataifa inavyofanyika na kufikiwa uamuzi katika Umoja wa Mataifa. Akasema anaamini kabisa kwamba kuna mambo ambayo wanaweza kujifunza. 

Mhe. Spika akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa wa Uwakilishi wa Kudumu, mara baada ya kuzungumza nao. Mhe. Spika  ameushukuru Uwakilishi wa Kudumu kwa   kuiwakilisha  vema Tanzania   Katika Umoja wa Mataifa.

Na  MwandishiMaalum , New York
Maspika wa Mabunge kutoka mataifa mbalimbali duniani, Wamemaliza mkutano wao wa Nne kwa kupitisha tamko ambalo pamoja na mambo mengine, linayataka Mabunge kuhakikisha yanasimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Malengo na Ajenda Mpya za Maendeleo Endelevu (Ajenda 2030).

Akihitimisha mkutano huo wa Maspika ambao hufanyika kila baada ya Miaka mitano, Rais wa Chama cha Kimataifa  cha Mabunge (IPU) Saber Chowdhur amesema, Maspika na wabunge wana wajibu wa kuhakikisha Serikali zao zinatenga bajeti za kutosha ambazo zitahakikisha utekelezaji wa malengo na ajenda mpya ya maendeleo endelevu.

Ajenda  2030 inayochukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Millenia (MDGs)  itapitishwa rasmin na Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali katika mkutano wao wa kihistoria na wa kilele utakaofanyika kuanzia tarehe 25 hadi 26 mwezi huu wa Septemba.

Miongoni mwa mambo  ambayo mabunge yanatakiwa kusimamia ili kuhakikisha kwamba malengo na ajenda hizo mpya zinatekelezwa kikamilifu pasipo ku muacha mwachama yeyote nyuma ni pamoja na kuhakikisha uboreshwaji wa vyanzo vya mapato ya ndani pamoja na kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi.


Spika wa   Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Anna Makinda ndiye aliyeongoza ujumbe wa  Tanzania katika Mkutano huu muhimu na wa aina yake na ambao umefanyika ikiwa ni wiki chache kabla ya Wakuu wa Nchi na Serikali kukutana kwa mikutano muhimu na inayotarajiwa kuzungumzia mstakabali wa maendeleo na ustawi wa watu na utunzaji wa mazingira.

“Maspika wa Mabunge ambao tumekutana hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,  tumepokea kwa kauli moja, Malengo na Ajenda mpya za Maendeleo Endelevu ambayo wakuu wa nchi na serikali watapisha wiki chache zijazo.

Kama wawakilishi wa wananchi na wasimamizi wa Mabunge tunawajibu wa kuhakikisha kwamba, tunakuwa mstari wa mbele katika ,kuhakikisha tunapitisha mipango na sera za utekelezaji wa malengo na ajenda hii mpya, bali pia kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuziba mianya ya ukwepaji kodi” amesema Rais wa IPU  Bwa. Chowdhury.
Rais wa IPU amewaeleza Maspika hao kwamba,  wako katika nafasi zao pamoja na mabunge ambayo ndiyo wawakilishi wa wananchi wanakazi kubwa mbele yao.

“Tuna kazi kubwa ya kufanya sisi kama wawakilishi wa wananchi, lakini  pia kuhakikisha kwamba mabunge yanashirikiana kwa karibu na serikali pamoja na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa ajenda 2030 ambayo inalenga katika pamoja na mambo mengine kuutokomeza umaskini”.

Pamoja na kusititiza haja na umuhimu wa mabunge kusimamia kwa karibu utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu,  mabunge yametakiwa pia kuhakikisha kwamba yanasimamia vema utawala wa sheria,  haki za binadamu na sheria za kimataifa zinazozingatia utawala wa kidemokrasi, unaozingatia fursa sawa na ushirikishwaji wa makundi ambayo yamo katika hatari kubwa.

Vile vile katika tamko hilo ambalo lilikuwa na mvutano mkubwa katika baadhi ya vipengele kama vile  matumizi sahihi na endelevu ya teknolojia ya mawasiliano na mitandao ya kijamii. 
Maspika hao wamesisitiza haja na umuhimu wa kuhakikisha kwamba pasipo kuingilia uhuru wa kujieleza, lakini pia uhuru huo unapashwa kuwa na mipaka na kwamba serikali zinapashwa kusimamia suala hilo kwa mujibu wa sheria za nchi na maslahi mapana ya ustawi, usalama, Amani na maendeleo ya watu wake.

Aidha jambo jingine ambalo pia limezungumzwa kwa mapana yake katika tamko hilo la Maspika wa mabunge ni pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi wanaokimbia machafuko na  vita   na wale wanaotafuta hali  bora ya maisha.

Katika kupunguza wimbi  la wakimbizi wa ndani , tamko linataka serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha inakabiliana na changa moto zinazotishia Amani na usalama,  kutokana na ukweli kwamba bila Amani na usalama hakuna maendeleo.

Maspika wamekubaliana pia kwamba utaaandaliwa utaratibu kwa maspika na wabunge kuhudhuria mkutano mwingine mkubwa wa kimataifa utakaojadili kuhusiana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Mkutano huu utafanyika mwezi Disemba mwaka huu huko Paris, nchini Ufarasa.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.